Sina Raha Na Maisha Ya Ndoa Mume Hana Hamu Na Mimi Wala Hanishughulikii

SWALI:

 

Mimi nimeolewa sasa inaenda miaka miwili lakini katika ndoa yangu sina raha kabia mume wangu hana raha na mimi na shida kubwa hana hamu ya kulala na mimi hata akiwa nyumbani hashughuliki na mimi.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu matatizo ya unyumba. Hata hivyo suala lako hili dada yetu halipo wazi kwani kwa kutokuwa na raha katika masiha ya ndoa, hatujui unakusudia raha ya upande upi, na je, mume wako yeye hana raha na wewe kwanini? Kuna tatizo gani hadi asiwe na raha na wewe na kwanini alikuoa ikiwa hana raha na wewe?

 

Ili kuweza kukusaidia ni lazima swali liwe wazi kwani kutoliweka wazi linatupatia sisi mashaka ya kujua tatizo hasa lipo wapi na vipi tutaweza kukusaidia.

 

Hata hivyo, kwa kufikiria kwetu ni kuwa muulizaji unataka nasaha ufanyeje katika hali kama hiyo ili ima udumishe ndoa yako au kupatikane ufumbuzi mwengine wowote ule. Ikiwa ni hivyo basi tutakupatia ushauri wetu baada ya maelezo yafuatayo.

 

Hakika ni kuwa sisi Waislamu tumekuwa na tatizo hili sugu katika jamii yetu jambo ambalo linabomoa jamii hii kwa kiasi kikubwa sana. Sababu za kutokea hayo ni:

 

  1. Huenda ikawa mume au mke amelazimisha kuingia katika mafungamano hayo.

  2. Mume kuwa amepatiwa sifa fulani kuhusu mkewe lakini asizikute.

  3. Mmojawapo ana shida zake mwenyewe ambazo hataki kumfunulia mkewe au mumewe.

  4. Kuona mambo ya ndoa kuwa tofauti na alivyotarajia, na kadhalika.

 

Kabla ya kukupatia nasaha tungependa kukuuliza, je, huyu mume kweli alikuoa kwa ridhaa yake? Je, hali ya kutokupenda ilianza kuanzia mlipooana au imekuja baadaye? Kwa zote hizo, Nasaha zetu ni kama zifuatazo:

 

  • Kama mumeo ni lazima uwe na ujasiri wa kukabiliana naye kwa njia ya ulaini, upole, busara na heshima ili upate kuzungumza naye. Mazungumzo ni lazima yawe ni yenye kufuma na bila kuficha. Zungumza naye kwa uwazi kuhusu mahusiano na matatizo yenu ili kupata ufumbuzi. Inatakiwa katika mazungumzo lile swali nyeti la ndoa lijitokeze na umuulize je, anatakaje? Anataka muendelee na ndoa au hakutaki tena ili msitesane?

  • Ikiwa suala la mazungumzo hayo halikufaulu itabidi uitishe mkutano baina yako, yeye, wazazi wako na wake. Katika kikao hicho inabidi pia uwe wazi kuhusu matatizo yako unayokabiliana nayo. Huenda ufumbuzi ukapatikana, na ikiwa haukupatikana basi itabidi uchukue hatua ya mwisho.

  • Kwenda kwa Qaadhi au Shaykh anayeaminika ili umpelekee mashtaka yako kuhusu mumeo. Ikiwa mume hana sababu ya kisheria ya kukuchukia hivyo, Qaadhi atatoa uamuzi wake ima awasuluhishe au apitishe talaka baina yenu ili kila mmoja atafute mshirika mwengine katika maisha ya ndoa.

 

Tunakuombea kila la kheri katika kupata ufumbuzi katika tatizo hilo ulilo nalo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share