SWALI LA KWANZA:
a.a.m ndugu waislamu mimi nataka kujua kama ukitumia mafuta ya nywele yaliotiwa isoproyl alcohol na alcohol denat ni najis yafafaa kutumia au hayafai kutumia. Nafurahii sana kupata mahali kama hapa kuuliza maswali ya kiislamu inshl ALLAH awazidishie imaan zenu shukran
SWALI LA PILI:
Assalam alaykum.
Nimesoma jawabu kuhusu mafuta, lotion na dawa za nyele zenye alcohol. Tafadhali nifafanulieni asli mia ngapi ndio kiwango kidogo? Na je kama hatujui kiwango gani kimetumika tutajuwa vipi yafaa au haifai. Kuna tafauti baina ya alcohol na "alcohol denat" na "isopropyl alcohol". Zote ni najis au laa. Mungu awajazi kheir
JIBU :
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.
Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mafuta yenye alcohol. Mwanzo tungependa kufahamisha kuwa alcohol yenyewe (yaani methanol na ethanol) sio najisi kama tulivyotangulia kusema katika jibu letu kuhusu hilo. Ingia kwenye viungo hivi hapa chini:
Je, (pombe) Pombe Ni Katika Vitu Najisi?
Kutumia Lotion au Mafuta Ambayo Ingredient Yake Ina Alcholol
Isopropyl alcohol ina majina mengi mbali na hilo, baadhi yake yakiwa Isopropanol, 2-propanol, propan-2-ol, sec-propyl alcohol, dimethyl carbinol, isohol, petrohol, na kadhalika. Kulingana na jina inaonyesha kuwa alcohol aina hii ni tofauti na ethanol kwa kuwa hii ina C tatu na –OH yake iko katika C nambari 2, yaani ya katikati. Alcohol hii inawaka, haina rangi kama vile maji, ni maji yenye harufu inayofanana na ethanol. Na kulingana na utafiti uliofanywa kuihusu ni kuwa ina madhara mengi na makubwa kwa binadamu, hivyo kuifanya utumiaji wake kuwa haramu.
Kama tulivyoeleza hapo awali ni kuwa inaweza kutumiwa katika nywele lakini kuacha kutia ni bora zaidi kwani kule kunusa kunaweza kukuletea madhara na hata huenda kule kupaka kwenyewe. Kukiwa na utata katika jambo basi sheria inatuamuru kuliacha jambo hilo. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Hakika halali iko wazi, na haramu iko wazi, na baina ya vitu viwili hivi kuna mambo yenye shaka, watu wengi hawayajui. Basi mwenye kuepuka mambo yenye shaka, hakika amehifadhi Dini yake na heshima yake. Na mwenye kuingia katika mambo ya shaka ameingia katika haramu…” (Al-Bukhaariy na Muslim).
Ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:
Kutumia Lotion au Mafuta Ambayo Ingredient Yake Ina Alcholol
Ama jibu la Swali la pili ni kwamba kiwango ambacho kinaweza kutumika hakipo katika Uislamu. Hata hivyo, kiwango kinachotumika ni kule kuwepo kwake hata ikiwa ni asilimia ndogo na namba. Uislamu una kanuni: ‘Kiliweshacho kingi hata kidogo chake ni haramu.’ Hivyo ni bora kutotumia lotion na dawa za nywele zenye alcohol kama alivyosema Mwanachuoni Ibn ‘Uthaymin. Ama Isopropyl alcohol tafadhali tazama jawabu letu kuhusu hilo kwa swali lililo juu.
Kuhusu alcohol denat ni ethyl alcohol (au ethanol) ambayo imeongezwa kemikali zilizo sumu kama acetone au methanol kuifanya isiweze kutumika na watu kwa njia ya kunywa. Kwa ajili ya ile sumu inafanya matumizi yake yenye athari zaidi hata ikiwa ni kutiwa kwenye nguo. Tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Anatuambia:
“Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizi” (2: 195).
Hivyo, kama Waislamu inatakiwa tujiepushe na alcohol, isopropyl alcohol na alcohol denat mbali na kuwa zote si najisi lakini ni haramu kutumiwa.
Na Allaah Anajua zaidi