Mahshi (Mjazo) Ya Pilipili Boga (Shaam, Misr)
Mahshi (Mjazo) Ya Pilipili Boga (Shaam, Misr)
Vipimo
*Pilipili Mboga Za Kijani - 10-12
Mchele - 1 kikombe
Nyama ya kusaga - 1 kikombe
Kitunguu kilichokatwakatwa (chopped) - 1 kidogo
Nyanya iliyokatwakatwa - 1
Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa - 1 kijiko cha chai
Parsley iliyokatwakatwa - 1 msongo
Garama masala (bizari mchanganyiko) - 1 kijiko cha chai
Pilipilimanga ya unga - 1 kijiko cha chai
Chumvi kiasi
Kidongo cha supu (stock cube) - 1
Nyanya kopo - 1 kijiko cha chai
Samli - 1 kijiko cha supu
Namna Ya Kutayarisha Na Kupika
- Osha na roweka mchele kwa muda mdogo tu.
- Kata mapilipili kwa juu kabisa iwe kama ni vifuniko vyake.
- Toa kokwa na safisha mapilipili weka kando.
- Mwaga maji mchele, uchanganye pamoja na nyama na viungo vyote iwe ndio mjazo wa mapilipili.
- Jaza kila pilipili boga moja kwa mjazo. Usijaze hadi juu kabisa kwa vile mchele utavimba na utapanda juu.
- Ukimaliza funika kila kifuniko na pilipili lake.
- Tia maji ya moto kiasi katika sufuria kubwa yakufunike mapilipili nusu yake tu.
- Yeyusha kidonge cha supu katika maji, nyanya kopo, na samli kisha Yapange mapilipili katika sufuria.
- Funika vizuri kabisa upike kwa moto mdogo mdogo hadi maji yakauke na wali uwive ndani ya mapilipili.
- Epua, subiri yapowe uyatoe na upange katika sahani yakiwa tayari.
Vidokezo
- Chagua mapilipili yaliyo saizi moja na yaliyo ya duara na mafupifupi ili yakae vizuri katika sufuria.
- Ukipenda ongeza kipimo cha mchele na nyama kidogo ili ubakie mjazo na uongoezee mchanganyiko wa mboga za barafu (frozen mixed vegetables) na utie katika sufuria upike katika kisufuria kingine. Utakapowiva pakua katika sahani na upange mapilipili kama kwenye picha.
- Ikiwa wali haukuwiva baada ya maji kukauka, ongeza tena maji urudishe kufunika na kupika tena hadi uwive.