Waislamu Wanafaa Kuwaombea Du’aa Wasio Wailslamu?

SWALI

 

 

Assalamu Aleikum warahmatullahi wabarakatuhu, mimi ni mwanafunzi katika chuo kimoja cha elimu ya juu hapa nchini Kenya, wakati wa kujisomea huwa tunajumuika na wanafunzi wenzetu ambao si waislamu na tukimaliza majadiliano yetu ya kimasomo ya kila siku huwa tuna utaratibu wa kuomba dua na huwa tunapea zamu ya kuomba dua yaani kwa mfano leo waislamu na kesho wakristo. Pia wakati wa kuombeana huwa tunaombeana wote, jee inafaa kwetu sisi waislamu kuwaombea dua wasiokuwa waislamu?

 

Wabillahi Tawfiqi

 


 

 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwaombea Du’aa wasio Waislamu. Hakika hilo ni suala ambalo halina utata katika Dini yetu. Unaruhusiwa kuwaombea wasio Waislamu kuongoka ikiwa bado wapo hai lakini wanapokufa Du’aa kwako inakatika. Na Du’aa sahali na nzuri ni kusoma tafsiri ya Suratul Faatihah (Surah ya kwanza).

 

Kuwaombea wasiokuwa Waislamu ili waingie katika Uislamu na wapate uongofu ilifanywa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale alipokuwa Makkah. Alimuomba Allaah Aliyetukuka Autie nguvu Uislamu kwa kusilimu mmoja kati ya ‘Umar wawili (yaani ima ‘Umar bin al-Khatwtwaab au ‘Amr bin Hishaam).

 

Ama hilo la nyinyi na wao la kukusanyika pamoja na kuombeana kwa zamu; leo nyinyi mnawaombea na kesho wao wanawaombea, hilo halina asli na sijui wao wanawaombea nini nyinyi? Je, wanawaombea kuongoka? Ilihali wao ndio wanaotaka uongofu! Au ni kuombeana kupasi mitihani?

 

Kwa kifupi mnaweza kuwaombea mkiwa pekee, na du’aa ya faragha ndiyo bora zaidi kuliko du’aa ya kumsikizilisha yule unayemuombea.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share