Mume Ana Ukimwi Nifanyeje Nidumishe Ndoa Yangu. Je Ni Madhara Kuishi Naye?

SWALI:

 

Asalam alekum warhmatullahi wabarakatu,

Mimi nilikuwa nina pendeleya kujuwa sababu nina kera hika sana kwenye nasfi yangu sijuwi nifanye nini ilinipate kujuwa kama ninayo yafanya nikosa awo sikosa na nini adhabu yake. Swali langu ni, mume wangu nina mpenda sana nimezaa naye watoto wane ila ana ukimwi mimi sina ukimwi wala wanangu hakuna anaye ukimwi sasa nifanye nini? Ili nidumishe ndowa yangu na sijuwi madhara yake sijuwi nifanye nini nina omba usaidizi kwenu. Mwenyezi mungu atawalipeni insaallah.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kuishi na mume aliye na ukimwi. Hili hakika ni swali nyeti sana katika maisha yetu sisi binadamu. Kupata madhara au kutoka katika madhara ni kuacha Sunnah na Dini au kuifuata na kuishika kwa magego yetu.

 

Katika suala hili, yapo mambo mawili na wala hakuna la tatu kwa muono wetu ambayo katika hayo unaweza kuchagua. Hayo ni kama yafuatayo:

 

1.     Kwa kuwa unampenda na unataka kumhudumikia katika ugonjwa wake huo, baki naye lakini msiwe mnakutana kimwili mpaka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atakapoamua kumchukua. Kwani katika kukutana kimwili upo uwezekano wa wewe pia kuambukizwa na ugonjwa huo ambao mpaka sasa hauna matibabu.

 

2.     Kuachana na mumeo kwa njia iliyo nzuri ili usije nawe kukumbwa na janga hilo la ukimwi wakati ambapo kwa sasa huna. Njia njema kwako kufuata ni kukaa naye chini na kumueleza hilo kwa usemi mzuri ili kusiwe na utesi.

 

 

Kabla ya kuamua unalotaka kufanya inafaa umuelekee Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kumuomba kwa kuswali Swalah ya Istikhaarah na kutaka ushauri kutoka Kwake.

 

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akuonyesha njia ya sawa nawe ubaki katika hali nzuri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share