Mume Hamtoshelezei Matamanio Yake Ya Tendo La Ndoa, Anaomba Ushauri

 SWALI:

Salaam alaykum warahmatullah wabarakatuu, Mimi ni mwanamke mwenye miaka 22 nimejaaliwa kupa ndoa ambayo mpaka sasa imetimia miaka 2 na tumejaaliwa kupata mtoto mmoja ila cha kunishangaza kwa sasa hivi mume wangu kabadilika sana sielewi kwa nini kila ninalojaribu kumueleza hanisikii na ananipangia mpaka siku za kufanya tendo la ndoa na kuniambia kuwa anachoka ndio maana pengine inaweza ikafikia hata siku 5 sijapewa haki yangu na mpaka siku ingine naililia lakini mafanikio yangu hayatokei. Na pengine tunapokuwa faradha huwa anamaliza kabla yangu mimi nakua sijatoshelezeka lakini ninastahmili, sasa sielewi mwenzangu ana nini naomba ushauri


 

JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupata shida katika tendo la ndoa na mumeo. Tufahamu kuwa tatizo hilo huweza likampata mume au mke kwa sababu moja au nyingine.

Kulingana na swali lako inaonyesha kuwa mlikuwa mkiishi baada ya harusi katika hali iliyo nzuri na tendo la ndoa lilikuwa sawa. Tatizo hili limeanza kujitokeza hivi karibuni. Tatizo hili huenda likawa limetokea kwa kupatikana moja wa sababu hizi:

  1. Huenda akawa mumeo ameanza kutumia uraibu wa mirungi au miraa.

  2. Huenda ikawa ni maumbile yake yamebadilika kwa kupungua kwa ashiki yake na nguvu zake za kiume.

  3. Huenda akawa amebadilika tabia na ana uhusiano mwengine wa nje ya ndoa.

Sababu zote hizi ambazo tumezitaja zinaweza kuondoka kwa kutumia dawa ya sawasawa kutegemea na tatizo lenyewe. Ikiwa ni mtumiaji wa miraa/ mirungi, utumiaji huo unamfanya awe ni mwenye kutokwa na madhii anapokuwa akitumia, hivyo anapofika kwako huwa anamaliza haja yake mara moja.

Ama kwa tatizo la pili, ni lazima mumeo aone kuwa ana tatizo na hivyo akubali kufanya dawa. Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza kuwa Allaah Aliyetukuka Hakuleta ugonjwa isipokuwa Ametupatia na dawa yake. Mnaweza kwenda naye kwa daktari mahiri katika magonjwa hayo ili aweze kumpatia dawa kwa ugonjwa wake huo. Na dawa ambazo hazina madhara ni zile za tiba asilia au tiba ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) na tajruba iliyopatikana na matabibu wa Kiislamu waliofanya utafiti kuhusu magonjwa tofauti. Na moja katika dawa ni hawlinjaan, ambayo inatumiwa na mwanamme nusu saa kabla ya kitendo cha ndoa. Kijiko kimoja cha chai hutiwa katika kikombe cha maziwa au maji na kunywa. Lakini itakuwa ni bora aonane na tabibu ambaye atamchunguza na kumpatia dawa muafaka.

Tatizo la tatu, ikiwa utahakikisha hilo kwa dalili mbalimbali, basi ni bora umkalishe na mzungumze kwa uwazi kabisa na umpe onyo aache tabia hiyo chafu kabisa inayomuudhi Allaah na kumchumia madhambi makubwa, na pia umweleze hatari ya magonjwa makubwa yaliyozuka na pia athari anayoweza kupata yeye, wewe na hata mtakachokizaa. Ikiwa kweli tatizo ni hili la tatu, basi baada ya kumketisha na asisikie, jaribu kuitisha kikao cha jamaa zako na jamaa zake ili mlijadili hilo kwa kina.

Tunawaombea tawfiki na kurudi katika hali yenu ya kawaida kama hapo awali.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share