Kumpa Mimba Mke Wa Mtu – Kisha Anamshawishi Amuoe Na Hali Bado Yumo Katika Ndoa – Na Vipi Atubie?

SWALI:

 

 

ASALAM ALEIKUM WARAHMATU LLAHI TAALA WA BARAKATU  MIMI NI KIJANA WA KIISLAMU NA NINA SWALI AMBALO NINGEPENDA KUJUA JAWABU KULINGANA NA MAELEZO YA MOLA WETU  NIKIKUA NAKUTANA NA BINTI AMBAE YEYE PIA AMEZALIWA KATIKA UISLAMU LAKINI AMEOLEWA NA MWANAMUME ALIE SILIMU KWA MASILAHI YAKE TU.

 

BASI TULIFANYA KITENDO CHA ZINA KWA MDA WA MWAKA MZIMA MPAKA AKAPATA MIMBA YANGU LAKINI BADO YUKO KWA MUME WAKE  MIMI NAJUTA SANA NA NIKAMUOMBA SANA AJE KWANGU ILI NIMUOE KWA SHERIA YA KIISLAMU KABLA MTOTO HAJAZALIWA LAKINI AKAKATAA KATA KATA PIA KWA MASILAHI YAKE PIA ANAYO YAPATA KWA MUME WAKE (PESA NA MENGINEO). JE HUKUMU YANGU ITAKUWA VIPI ANA NAWEZA KUTUBU VIPI DHAMBI HIZI SABABU KWA KWELI MPAKA YULE MUME NILIMFUATA NIKAMWAMBIA UKWELI LAKINI HAKUNIAMINI NA AKANIONYA NISIPIGE SIMU TENA KWAKE.

 

NAOMBA WASIA ILI NIPATE KUJUA LAKUFANYA INSHALLAH. NA ALLAH AZIDI KUWATIA IMANI YA KUONYESHA WAISLAMU NJIA YA KISAWASAWA NA AWAPE BARAKA ZOTE HAPA DUNIANI NA KESHO AKHERA PIA AMIN.

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza tunapenda kukutanabahisha kosa katika maamkizi yako kwamba umetaja ‘ASALAM ALEIKUM WARAHMATU LLAHI TAALA WA BARAKATU’ . Hivyo sivyo inavyopasa kutamka bali iwe ‘Assalaamu ‘alaykum wa RahmatuLLaahi wa Baraakatuh’ bila ya kuongeza ‘Taala’. 

 

 

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kuzini na mke wa mtu.

Ama kwa mas-ala ya maslahi hapo hatuwezi kusema kwani hilo ni jambo la moyo wa mwanaadamu nasi hatuna kipimo cha kupima hilo. Maadamu huyo mume amekuwa ni Muislamu sisi tutakuwa na dhana nzuri mpaka aritadi au afanye jambo baya kidini.

 

Hakika ulifanya makosa na madhambi makubwa sana pale ulipozini na mke wa mtu. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Wala msikaribie zinaa” (17: 32). Na kosa jingine ni kutaka kumtoa msichana katika ndoa yake ya halali ili upate kumuoa wewe, jambo ambalo ni kinyume na sheria. Kisheria huwezi kumuoa mpaka aachwe na mumewe kisha baada ya hapo na kumalizika eda yake ndio ufunge naye nikaha. Na kwa sasa ikiwa ataachwa eda yake itakuwa mpaka atakapozaa, ndio wakati utaweza kumuoa.

 

Pia fahamu kuwa huyo mtoto Kiislamu atakuwa ni wa mumewe na sio wako labda mumewe amkane kuwa si wake. Mumewe akimkana pia hatokuwa wako. Kijana huyo akizaliwa hatokurithi wala wewe hutomrithi.

 

Ni vyema kuwa umetambua kosa lako la zinaa na unataka kurudi kwa Allaah Aliyetukuka. Na kurudi hakuna tatizo kwani Allaah Aliyetukuka Anasema: “Hakika Allaah Anasamehe madhambi yote” (39: 53). Hata hivyo, toba ina masharti yake, na ni lazima uyatekeleze ili upate kusamehewa na Muumba wetu. Masharti yenyewe ni kama yafuatayo:

 

1.     Kuacha na kujitoa katika maasiya na madhambi.

2.     Kujuta kwa kutenda madhambi hayo au dhambi hilo.

3.     Kuazimia kutorudia tena kosa hilo katika maisha yako. Kwa hiyo inabidi sasa uachane na huyo mke wa watu haraka kabisa na ukate mawasiliano ya aina yoyote yale na yeye.

4.     Kutaka msamaha kutoka kwa uliyemkosea ambaye ni mume wa huyo mwanamke ambalo tayari unasema ushalifanya, na maadam yeye hakukuamini basi tena wewe ushatekeleza jukumu lako na zidi kumuomba Allaah Maghfirah na kuzidisha kufanya mambo mengi ya kheri.

 

Ukiyafanya hayo kwa nia njema na ikhlaswi basi utakuwa katika wema na uzuri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share