Zingatio: Maasi Ni Sababu Ya Kuporomoka Hifdh
Zingatio: Maasi Ni Sababu Ya Kuporomoka Hifdh
Naaswir Haamid
Sehemu ya ubongo wa Muislamu ni makaazi ya fikra njema zenye kuhifadhika kwa kufuata maamrisho ya Uislamu pamoja na kujiepusha yale yaliyokatazwa.
Iwapo akili ya Muislamu itaingizwa mambo yaliyo kinyume na Uislamu, bila ya shaka yoyote itafisidika kama ambavyo hadathi (uchafu) inavyoiharibu twahara (usafi). Muislamu anatakiwa kuwa na fikra njema, nzuri na zenye kuwaza namna ya kuuendeleza Uislamu. Pale akili ya Muislamu inapoingia fikra za uzinifu, beti za miziki na pumbazo nyenginezo inaharibu mfumo mzima wa kuweka kumbukumbu.
Jambo hili la kushuka hifdhi limedhihiri ndani ya jamii zetu, vijana wetu wanaosoma wameshuhudiwa wakipata taabu mno ya kuhifadhi mambo. Ni wenye kupanda milima na kushuka mabonde, usiku na mchana wapo na mabuku, mijadala (group discussions) na madarasa ya ziada (tuitions). Harakati hizi zinakwenda kinyume na vile walivyosoma wacha wa Allaah waliopita. Waislamu ambao walikuwa wepesi wa kuhifadhi mambo.
Imaam Ash-Shaafi'iy (Rahimahu Allaah) alikuwa ni mwepesi wa kuhifadhi, pamoja na kipaji alichopewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) lakini pia alikuwa ni mcha wa Allaah maarufu. Yasemekana kwamba alikuwa akiziba upande mmoja wa kitabu pale anapohifadhi ili asichanganye hifadhi za kurasa mbili kwa wakati mmoja, yaani ahifadhi kurasa moja baada ya nyengine.
Ni kusema kwamba akili yake ilikuwa inakamata vitu mfano wa sumaku. Siku moja katika pirika pirika zake, jicho lake likakutana na mwanamke (mapokezi mengine yanaeleza kinyume na hivi).
Ni tendo lililokuwa halijakusudiwa na hakuendelea kumuangalia kama ambavyo vijana wengine wangefanya.
Aliposhika masomo yake, aligundua hifdhi yake imeporomoka na jambo hilo lilimkera mno hadi kwenda kumshtakia mwalimu wake anayeitwa Wakiy'.
Anasimulia Imaam Ash-Shaafi'iy mkasa huo kwa mtindo wa shairi:
شَكَوْتُ إلَى وَكِيعٍ سُوءَ حِفْظِي |
فَأرْشَدَنِي إلَى تَرْكِ المعَاصي |
وَأخْبَرَنِي بأَنَّ العِلْمَ نُورٌ |
ونورُ الله لا يهدى لعاصي |
Nilimshitakia Wakiy' ubovu wa hifdhi yangu **** Akaniongoza katika kuacha maasi.
Na akanijuza kuwa 'ilmu ni nuru **** Na nuru ya Allaah hahidiwi kwayo mtu 'Aaswi.
Iwapo Imaam Ash-Shaafi'iy hifdhi yake imeathirika kwa tendo hilo tu, ni namna gani akili zetu na zile za vijana wetu zitaathirika? Hili ni vyema likatiliwa mkazo kutoka kwa wazee, vijana hadi watoto. Hifdhi za leo zimekaa ndani ya bongo mfano wa maji na mafuta, ni vitu vinavyokaa mbali mbali. Unapopita kwapigwa miziki, unapoenda kuna wanawake wanaotembea utupu ingawa wenyewe wajiona wamevaa!
Waislamu wanaweza kuliona jambo hili ni jepesi lakini lina ukweli ndani yake, kwani vijana wengi sio wenye hata kukumuta vumbi msahafu seuze kuisoma na kuihifadhi. Hayo mafanikio katika masomo yao shuleni yatapatikana vipi? Na iwapo tunaifananisha hali hii na ile ya Makafiri, basi tumekosea, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameshawafunulia pepo yao hapa duniani na Hisabu yao ipo mbele ya Muumba.
Waungwana wanatwambia: Lima juani na ulie kivulini. Tukumbuke kwamba duniani tumekuja kuchuma na mavuno yake yapo siku ya Hisabu. Hivyo, tumkhofu Rabb wetu kikweli kweli kwa kuacha kusikiliza miziki, kuzini kwa macho na utupu, kusengenya na maasi mengineyo na In shaa Allaah tutapata mafanikio hapa duniani na Akhera.
Tunakuomba Mbora wa 'Ilmu Ambaye Kwako hakuna lisilojulikana wala lisilowezekana: Ututosheleze kwa 'ilmu, utupambe kwa 'ilmu, utukarimu kwa taqwa na uzifanye njema afya zetu.