Zingatio: Ewe Nafsi Mche Mola Wako
Zingatio: Ee Nafsi Mche Rabb Wako
Naaswir Haamid
Ee nafsi mche Rabb wako kabla ya kufika mbele ya Hisabu. Utataka ardhi ipasuke ujifukie wala hutaweza, utahitaji kuitenganisha nafsi na umbo lako hutapatiwa nafasi hiyo na wala hutaonja mauti wala uhai. Ni adhabu juu ya adhabu.
Nafsi huwezi kuhimili vishindo vya siku hiyo, basi ni kwanini unamuasi Rabb wako? Ni kwa neema gani ambayo Rabb wako kakunyima? Nafsi tubu kabla ya siku isiyoshikika wala isiyo na msamaha haijakufikia.
Nafsi unahadaika na dunia? Ni kwa kipi ambacho kinakuhadaa ndani ya dunia hii? Vyote hivyo ni pumba zitakazokuja kupeperushwa, sio mali wala watoto wako. Nafsi mukhofu Mwenye Kiburi Ambaye Hana kimshindacho. Muogope Mwenye Enzi Ambaye Alikuwepo kabla Yako na Atakuwepo milele kukuchunga wewe na nafsi nyengine. Naye Ndie Ajuaye kuadhibu hakuna mwengine mfano wake. Basi ni kwanini umuasi Rabb wako?
Ee nafsi, utakuja kulaumu siku ambayo haitafaa lawama, umshike Ibilisi na akakuruka mita alfu juu. Nafsi tubia kwa Rabb wako kabla ya kaburi halijakubinya, mbavu zako za kushoto na kulia zikakutanishwa pamoja!
Rahmah za Rabb zisizo na kifani kutwa zakumurika, nazo ndizo zinazokupelekea kutomuasi Rabb wake. Ee nafsi unapojiweka mbali na rehema hizi, naye Muumbaji Anajiweka mbali na wewe, ni hasara iliyoje kujiweka mbali na rehema za Yule Ambaye nafsi yako imo Mikononi Mwake.
Ndani ya Suwrah-Yuwsuf tunakutana na kisa maarufu cha mke wa Mheshimiwa kumhadaa Nabiy Yuwsuf, naye mwisho alikiri kwamba nafsi ndiyo iliyompotosha isipokuwa ile ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameirehemu. Tafsiri ya aya hiyo ni kama ifuatavyo:
وَمَا أُبَرِّئُ نَفْسِي ۚ إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ إِلَّا مَا رَحِمَ رَبِّي ۚ إِنَّ رَبِّي غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥٣﴾
Na siitoi hatiani nafsi yangu. Hakika nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu isipokuwa ambayo Rabb wangu Ameirehemu. Hakika Rabb wangu ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Yuwsuf: 53]
Nafsi zote ni zenye kukosa, na mbora wa mwenye kukosa ni yule ambaye atarudi kwa Rabb wake. Ikamate nafsi yako na uzungumze nayo asubuhi, mchana na usiku. Hiyo ni nafsi ambayo itakuja kuwa ni adui yako namba moja Siku ya Qiyaamah.
Basi elekea kwa Rabb wako na muombe msamaha wa makosa ya nafsi yako kama Alivyokufunza kupitia ndani ya Qur-aan na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ۗ رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ ۖ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنتَ مَوْلَانَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴿٢٨٦﴾
Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake. Itapata (thawabu) iliyoyachuma, na ni dhidi yake (kwa maovu) iliyojichumia. Rabb wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Rabb wetu, Usitubebeshe mzigo kama Ulivyoubebesha juu ya wale waliokuwa kabla yetu. Rabb wetu, Usitutwike tusiyoyaweza, na Tusamehe, na Tughufurie na Turehemu, Wewe ni Rabb Mlinzi wetu, basi Tunusuru dhidi ya watu makafiri. [Al-Baqarah: 286]
“Ee Allaah! Wewe ni Rabb wangu, hapana Rabb Apasaye kuabudiwa kwa haki ila Wewe, Umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najilinda Kwako kutokana na shari ya nilichokifanya, nakiri Kwako kwa Kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba Unisamehe kwani hasamehe madhambi ila Wewe.”