Kuzini Na Kushika Mimba Nini Hukmu Yake
SWALI:
Assalam aleykum warahmatuLLAH wabarakaatuh. shukran ndugu zetu kwa kutuelimisha mengi na inshALLAH Mungu atakulipeni kheri kwa jitihada zenu.
Amma baad. Mimi napenda kuuliza, je kama mwanamke hajaolewa na akabainika amepata ujauzito bila ya mume je ujauzito huu unaweza ukasimama kama ni ushahidi wa kuwa yeye ni mzinifu? Na kama jibu ni ndio, je kama nchi anayoishi ni nchi inayohukumu kiislam atapaswa kupata adhabu ya kiislam ya mzinifu? Pia kama ni kesi ya mke wa mtu ambae mume wake anaishi mbali na yeye, lakini mke wa mtu huyu akapata ujauzito bila kuwepo mumewe jee ujauzito huu utamfanya mwanamke ahukumiwe kifo cha mawe katika nchi zinazohukumu kiislam? Wassalam aleykum.
WABILLAHI TAWFIQ
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hukumu ya kuzini na kushika mimba.
Ni jambo linaloeleweka kuwa Shari‘ah ya Kiislamu ni samehevu kwa kiasi kikubwa na ikiwa upo uwezekano wa kuondosha adhabu basi hakimu anatakiwa afanye hivyo. Yapo mambo kadhaa ambayo yanatakiwa yafahamike ile tuweze kupata uamuzi muafaka kwa suala hili bila ya kubakisha utata wa aina yoyote ule. Mambo yenyewe ni kama yafuatayo:
1. Inatakiwa mwanzo tuelewe maana ya uzinzi. Nayo ni kujamiiana kati ya mwanamme na mwanamke bila ya kuwa na uhusiano wa kishari’ah wa mume na mke kati yao kwa hiari yao bila ya kutenzwa nguvu. Wawili hao waweza kuwa wameoa au kuolewa au hawajahi kuoa au kuolewa.
2. Kiislamu zinaa ni uovu na uhalifu wenye kustahiki adhabu kinyume na nadharia nyingine zote.
3. Uislamu hautegemei sharia ya kuadhibu ili kuokoa ubinadamu kutokana na hatari ya zinaa bali umeweka mikakati na hatua za marekebisho na kuzuia kwa kiwango kikubwa. Ki Shari‘ah, unatoa adhabu kama hatua ya mwisho baada ya kuwafundisha na kuwahimiza watu warekebishe tabia zao na unawachukulia hatua madhubuti za kuwazuia watu wasizini. Lengo halisi la Uislamu, ni kwamba watu wasizini kabisa, na kamwe lisitokee tukio la kulazimisha kuitumia hiyo adhabu kali sana. Kwa ajili ya lengo hilo, Uislamu kwanza kabisa unamtakasa mtu: humjaza mtu hofu ya Allaah Aliyetukuka, Mwenye uwezo wa kila kitu na kumpatia matarajio ya kuwa mahali pema lau atafuata maagizo na kuacha makatazo.
4. Zinaa yenye kuhukumiwa adhabu ni ile ambayo kichwa cha mwanamme cha dhakari yake itaingia kwa mwanamke hata kama ni kidogo. Kukutwa mwanamme na mwanamke kitandani kuwa wamekumbatiana, wako uchi, wanapigana busu, haya yote hayatoshi kuamua kuwa wao wamezini.
5. Ukweli tu kuwa mtu amezini hautoshelezi kumchukulia kuwa ni mhalifu. Kwani yapo masharti ambayo lazima yatekelezwe na yatimizwe. Ama akiwa hajaoa au kuolewa, mkosa awe ni baleghe, na awe na akili timamu, kwani mtoto au mwendawazimu akizini hakuna adhabu. Ama kuhusu zinaa ya waliooa au kuolewa, yapo masharti ya ziada, nayo ni awe huru (mjakazi anapata adhabu nusu), awe ameoa au kuolewa kihalali, awe pia amejamiiana na mkewe baada ya ndoa na mkosa awe Muislamu (japokuwa Maimaam wengine wamelipinga hilo).
6. Ili kuweza kumhukumu mtu kwa kosa la zinaa ni budi kuthibitisha kuwa amekifanya kitendo hicho kwa radhi yake. Kama mtu atalazimishwa kuzini, yeye si mhalifu wala hastahiki adhabu.
7. Shari‘ah ya Kiislamu haimpi yeyote madaraka isipokuwa serikali kumhukumu mzinzi, na si kingine ila mahakama ya Kiislamu ndiyo yenye mamlaka ya kuwaadhibu wahalifu hao. Ni kongamano la wanachuoni wote kuwa amri iliyomo katika Aayah ya 2 ya Suratun Nuur (24): “Wapigeni mijeledi”, haikuelekezwa kwa watu wa kawaida kuwa ndio wana mamlaka ya kupiga wengine mijeledi.
8. Chini ya Shari‘ah ya Kiislamu, adhabu ya zinaa ni sehemu ya Shari‘ah ya nchi. Hivyo, basi itawathubutikia watu wote katika nchi ya Kiislamu. Ni Imaam Maalik pekee ndiye mwenye rai tofauti na hiyo.
9. Shari‘ah ya Kiislamu haimlazimishi mtu kukiri (kuungama) kosa la zinaa, wala haiwalazimishi wale wenye habari ya tukio hilo kwenda kuiarifu serikali. Lakini kosa likibainika kwa serikali, hapo hamna tena nafasi ya kusamehe. Hiyo ni kutokana na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kama yeyote miongoni mwenu ni mhalifu wa maadili, bora abaki katika sitara ya Allaah, lakini akitubainishia kosa lake, bila shaka tutamhukumu kwa Shari’ah ya Allaah” (Abu Daawuud).
10. Chini ya Shari‘ah ya Kiislamu, zinaa si kosa la kulipiwa fidia ya pesa au mali.
11. Serikali ya Kiislamu haitomchukulia hatua yoyote mtu yeyote kwa kosa la zinaa hadi pale utakapothbitishwa uhalifu wake. Bila uthibitisho serikali haitoweza kutoa adhabu. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya al-Bukhaariy na Ibn Maajah juu ya mwanamke aliyekuwa akiendesha umalaya Madiynah, kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Kama ningekuwa wa kumpiga mawe mtu yeyote hadi kufa bila uthibitisho, kwa hakika ningehakikisha kuwa mwanamke huyu amepigwa mawe hadi kufa”.
12. Uthibitisho wa kwanza unaowezekana wa zinaa, ni kwamba ushahidi madhubuti uhakikkishwe dhidi ya mhalifu. Vipengele muhimu vya Shari‘ah ni:
i. Qur-aan inaamuru wazi wazi kuwe na angalau mashahidi wanne walioshuhudia kwa macho yao ili kuthibitisha kosa hilo.
ii. Mashahidi wawe wa kuaminika kufuatana na Shari‘ah ya Kiislamu ya ushuhuda, yaani wasiwe ni waongo.
iii. Mashahidi wote watoe ushuhuda kuthibitisha kuwa wamewaona mwanamme na mwanamke katika kitendo chenyewe cha kujamiiana, kama kidole ndani ya pete.
iv. Uafikiane ushahidi wa mashahidi kuhusu wakati, mahali na watu waliofanya kitendo hicho.
13. Kuna hitilafu ya maoni kuhusu mimba ya mwanamke huru asiye na mume anayejulikana, kuwa mimba hiyo ni ushahidi tosha wa uhalifu wa uzinifu au la. Kwa rai ya ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) huu ni ushahidi tosha na Imaam Maalik ameifuata rai hiyo. Hata hivyo, wengi wa wanachuoni wana rai kuwa mimba tu si thibitisho la kumpelekea mwanamke kurujumiwa au kupigwa mijeledi mia moja. Ni lazima adhabu kali kama hiyo zijitegemeze aidha juu ya ushahidi au kukiri kosa kwa mtuhumiwa mwenyewe. Moja kati ya kanuni za msingi za Shari‘ah ya Kiislamu ni kwamba faida ya shaka imwendee mshitakiwa. Na hili linaungwa mkono na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Epukeni adhabu kila mnapokuta mpenyo wa kuiepuka” (Ibn Maajah). Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Jaribuni kuepuka kuwaadhibu Waislamu kila inapowezekana, na kama kuna njia ya mshitakiwa kuiepuka adhabu, mwachilieni. Kosa katika hukumu ya kumwachilia mshitakiwa ni bora kuliko kosa katika kumwadhibu bila haki” (at-Tirmidhiy). Kufuatana na kanuni hii, kuwepo kwa mimba si ushahidi thabiti wa zinaa, japokuwa una nguvu sana upande wa shaka, kwani upo uwezekano wa mbegu ya kiume kuingia hata bila ya kujamiiana, na hivyo kumfanya mwanamke kupata uja uzito. Hata uwezekano huo mdogo wa shaka unatosha kumwepusha mshitakiwa na adhabu ya kutisha na kali ya zinaa.
14. Badala ya ushuhuda, kitu kingine kinachoweza kuthibitisha hatia ya zinaa ni kukiri kwa mhalifu mwenyewe. Kukiri huku ni lazima kuwe kwa maneno wazi na rahisi, na mhalifu ni lazima akubali kuwa amezini na mwanamke au mwanamme aliye haramu kwake. Pia ni lazima akiri kuwa kitendo cha zinaa kilikamilika kwa hali zote. Mahakama nayo iridhike kwamba mhalifu anakiri kosa kwa hiari na kuwa akili yake ni timamu wala si mlevi. Jambo la kujitolea ushahidi mwenyewe lilifanyika katika uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe naye akaamuru wahalifu watiwe adhabu ya kishari’ah. Mfano ni mwanamme Ma‘iz bin Maalik al-Aslamiy na la yule mwanamke wa Ghaamidiyah.
15. Kulingana na kesi hizo mbili zilizotajwa kwa muhtasari hapo juu ni wazi kuwa aliyekiri kuzini hatasailiwa kuhusu mtu aliyezini naye.
Hizi ni baadhi ya nukta na vipengele muhimu ambavyo vitatusaidia kuhusu masuala ya kuadhibiwa kwa mzinifu mwanamme au mwanamke. Kwa muhtasari ni kuwa ujauzito si ushahidi tosha kwa uhalifu wa zinaa kwani mwanamke akileta tashwishi ndogo sana basi adhabu ni lazima iondolewe kwake.
Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:
Nini Hukmu Ya Kuzini Ndani Ndoa?
Nini Hukumu Ya Mwenye Kuzini Kwa Siri?
Nini Hukmu Ya Watoto Wa Nje Ya Ndoa?
Na Allaah Anajua zaidi