Ndugu Wamembadilishia Yatima Jina La Baba Yake Wakati Wanamtengenezea Cheti Cha Kuzaliwa

SWALI:

 

ASSALAMU ALEYKUM

NAMSHUKURU ALLAH KWA KUPATA FURSA HII YA KUWEZA KUIFAHAMU DINI YETU. NINGEPENDA KUULIZA KUUHUSU KUBADILISHA JINA LA BABA. KWA SABABU NIMESOMA NIKAONA HAIFAI KUBADILISHA JINA LA BABA. MIMI NINA NDUGU YANGU WA KIUME KWA MAMA YEYE NI YATIMA BABA YAKE KISHA KUFA. KUMETOKEA SHIDA TULIPOTAKA KUMTENGEZEA MAKARATASI YA KUZALIWA KWA SABABU HATUNA DOCUMENTS ZOZOTE ZA BABA YAKE TUNAJUA TU JINA LAKE. SISI DADA ZAKE TUKAAMUA TUTUMIE DOCUMENTS ZA BABA YETU PIA NAE ASHAFARIKI ILI APATE KARATASI YA KUZALIWA. LAKINI TULIMUUSIA NDUGU YETU TUKAMWAMBIA KUA ASIJE WAKATI WA MBELENI AKAJA KUDAI URATHI. JEE KUFANYA HIVI ITAKUA NI MAKOSA. ALLAH AWAPE KILA LA KHEIR KATIKA KUELIMISHA WATU.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kubadilisha jina la baba yake ndugu yenu aliye yatima.

Suala hili alikatazwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Mola wake mpaka ikabidi mtoto wake wa kupanga aliyejulikana kwa jina la Zayd bin Muhammad arudishiwe jina lake la awali la Zayd bin al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

Allaah Aliyetukuka Ameteremsha Aayah kuhusu hilo pale Aliposema: “Waiteni kwa ubini wa baba zao, maana huo ndio uadilifu mbele ya Allaah. Na kama hamuwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini na rafiki zenu” (al-Ahzaab [33]: 5).

 

 

Hata kama baba yake amekufa na hana makaratasi inafaa nyinyi mfanye juhudi kumfanyia cheti kwa jina la baba yake mzazi hata ikiwa mtakwenda kwa wahusika katika serikali ili kuwajulisha hayo. Hata kama hana nyaraka, mnaweza kwenda kwa serikali mkawaelezea au kwa jamaa za baba yenu wa kambo na kumuulizia. Hakutakosekana njia ya kuweza kumsaidia bila ya kutumia jina la mtu mwengine. Hata kama hamtapata hayo maalumati ya babake itabidi tu mumuite jina la baba yake halisi.

 

Hakuna ruhusa kwa nyinyi kumuita jina la baba asiye wake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share