Baada Ya Kusilimu Alitahiriwa Akakosewa Inamletea Madhara Mke; Hataki Kurudi Kutahiriwa

SWALI:

 

Asalaam alykum.

Mume wangu alikua mkristo miaka 9 kabla yakunioa mie mwaka jana.

Nimemkuta hajatahiriwa nikamshauri baada ya miezi 6 akaenda kutahiriwa, Lakini wamemtahiri vibaya kwamaana govi bado limebaki kiasi kwamba kumradhi Kama hana ashki govi lafunika koto nakuacha sehemu ndogo tu.

Nimejaribu kumshauri akatahiriwe tena

na Dr
anaejua lakini hukasirika Nikimwambia na kumfafanulia kua wamemtahiri vibaya, namie inanletea madhara Yakupata maradhi ya muwasho kila tukikutana kwa sababu govi laweka uchavu na Hutoa harufu mbaya kama hajakoga.

Sina raha na tendo la ndoa,siku hizi nikimwambia asema ataenda lakini Haendi!Naombeni ushauri ndugu zangu waislam nirudi kwetu mpaka atakapo Rudia tena au nifanyaje au nimwambiaje ili mume wangu arudie tena tohara?

Nashukuru. Asalaam alykum.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kutahiriwa vibaya na hivyo kuona shida katika tendo la ndoa. Kwa hakika hilo ni tatizo kubwa kwa wanawake, ndipo Uislamu ukawa ni wenye kuweka njia kabambe ili mume na mke wawe ni wenye kufurahika katika tendo la ndoa wala wasiwe ni wenye kuona karaha.

 

Mbali na ushida unayopata dada yetu inatakiwa uvumilie kwa muda mwingine kwani mume wako alikuwa si Muislamu na huenda bado hajapata mafunzo katika maumbile ya Kiislamu na Sunnah zake. Kwa kuwa kutahiri kwa wanaume ni jambo lililo la maumbile Waislamu wanatahiriwa wakiwa wadogo ili wasipate taabu baadaye.

 

Nasaha ambazo tunaweza kukupa ni kwua wewe uko katika Da’wah ya kumbakisha mumeo katika Dini hii ya Uislamu. Hivyo, tunaomba ufanye yafuatayo:

 

  1. Mwingishe katika madarasa ya yeye kuweza kujua Dini yake. Ikiwa kuna Msikiti au Madrasah ambayo inafundisha waliosilimu mwambie akajiunge ili apate kujua Dini yake sawa sawa.

 

 

  1. Nunua kanda za video, VCD, DVD au za tepu ili mpate nyote wawili mafundisho ya Uislamu yaliyo sahihi. Na miongoni mwa mafunzo ni kupata mas-ala ya kujitwahirisha kwa Muislamu.

 

 

  1. Kuweni na kikao nyumbani ya kuweza kusoma pamoja vitabu vya Dini ili pia nyumba iwe hai katika suala hilo.

 

 

  1. Mfundishe mumeo kimatendo jinsi ya kujisafisha na kujitwahirisha na haswa akiwa ana govi lake. Nadhani ukimpitisha katika jambo hili ataamua kutahiriwa kama walivyokubali kutahiriwa waliosilimu katika baadhi ya makabila ambao hawatahiri. Kwa kuwa kujitwahirisha ukiwa na govi ni shida na uchungu. Mwambie kuwa Swalah zake hazitokubaliwa ikiwa hatofanya hivyo, kwa kuliinua govi lake na kulisafisha barabara. Na kufanya hivyo itamueka katika hali safi na viini ambavyo vinabaki katika sehemu hiyo havitokuwepo na hivyo kukuondolea maumivu.

 

 

  1. Mfundishe adabu za jimai katika Uislamu. Miongoni mwa adabu ni kama alivyosema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa yeye humpambia mkewe kama mkewe anavyo jipamba kwa sababu yake. Hivyo, onyesha mfano kwa kwenda kuoga kabla ya jimai na umwambie mwenzio kuhusu adabu hiyo kwa hiyo naye aoge. Au ingieni chooni pamoja muoge mukiwa pamoja kwa wakati mmoja.

 

 

  1. Pata makaratasi ya kidaktari ambayo yanayoeleza kuhusu madhara ya govi kubakia.

 

Tuna matumaini makubwa sana kuwa kwa kufanya hivyo mumeo atabadilika na hivyo kuishi katika hali nzuri.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share