Kufanya Kazi Kunakouzwa Picha, Timthali, Nembo Za Viumbe Inafaa?
Kufanya Kazi Kunakouzwa Picha, Timthali, Nembo Za Viumbe Inafaa?
SWALI:
Assalam Alaykum! In sha Allah nauliza swali langu kama ifuatavyo? Mimi nafanya kazi za kuuza vitu vya kuvaa yaani jewerly shop na katika shop hii kuna baadhi ya vitu vimetengenezwa kwa nembo ya wanyama kwa mfano pete unakuta imetengenezwa kwa tembo, twiga, tiger na wanyama mchanganyiko nauliza kwa kufanya kwangu kazi sehemu kama hii ni haramu tafadhali naomba mnifahamishe.
Nawatakia kila la kheri na ALLAH KARIM awajaze jaza yake in sha Allah wa hadha Assalam Alaykum.
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Tufahamu ndugu zetu kuwa upigaji picha, uchoraji wa sura yenye uhai au timthali zote zimekatazwa. Kwa dharura upigaji wa picha umeruhusiwa kwa ajili ya kitambulisho au pasipoti na mfano wa hizo.
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza hilo kwa kauli zake nyingi. Mfano,
“Hakika wale wenye kutengeneza hizi picha wataadhibiwa siku ya Qiyaamah, wataambiwa: ‘Vihuisheni mlivyoviumba’” [Al-Bukhaariy, Muslim, Maalik na an-Nasaa’iy].
Na akasema:
“Kila mchoraji sanamu ataingia Motoni. Atawekewa mtu – kwa kila sanamu aliyoichora – atakayemuadhibu katika Jahanamu” [Al-Bukhaariy na Muslim)].
Na akasema:
“Hakika watakaokuwa na adhabu kali Siku ya Qiyaamah ni wapigaji picha” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ikiwa basi huna budi kuchora au kupiga picha, basi fuata agizo lifuatalo la Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pale aliposema:
“Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesema: ‘Ni yupi aliyedhalimu kumshinda anayeumba kama Niumbavyo! Basi waumbe dharrah (atomu), au waumbe punje ya nafaka, au waumbe shayiri” [Al-Bukhaariy na Muslim[.
Yaani unaweza kupiga picha au kuchora viumbe visivyo na uhai kama miti, anga, nyumba na kadhalika.
Kwa hiyo, ikiwa ni haramu kuchora au kupiga picha kuuza vitu ambavyo ni haramu pia kumekatazwa. Hii ni kwa kauli ya Aliyetukuka:
“Na saidianeni katika wema na taqwa wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuadhibu” [Al-Maaidah [5]: 2]
Kwa hivyo, kusaidia katika madhambi ni madhambi.
Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:
Hukmu Ya Kuchora Au Kupiga Picha Za Viumbe Vyenye Roho
Masanamu Ya Michezo Ya Watoto Yanafaa Kuwekwa Nyumbani?
Na Allaah Anajua zaidi