Anataka Kuolewa Wazazi Hawataki Hadi Amalize Shule
SWALI:
Asalaam aleykum
mimi nauliza je nikitaka kuolewa na wazazi hawataki nikalazimisha huku hawako radhi na mimi najua kabisa na naamini kuolewa kwangu ndio njia yangu ya peponi kutokana na sasa jinsi dunia ilivyojaa maasi na vishawishi.wazazi wanataka mpaka nimalize shule na nipate kazi ndio niolewe na hapa nilipo nina miaka 23, sasa nifanye nini? na ndoto zangu ni kuolewa na mtu anaeijua dini na sheria zake akizifata
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Tunashukuru kwa swali lako zuri kuhusu kuolewa.
Katika Uislamu si vyema kutoa hukumu kwa kitu ambacho hakijatokea, kwani tutakuwa tunatoa hukumu ya jambo lisilokuwa na uhakika na hivyo basi huwa halina hukumu; ama likitokea ndio hutakiwa kutolewa hukumu au kutafutiwa
Tunachoweza kufanya na ndio hasa kinachotakiwa kulingana na maneno yako ‘nikitaka kuolewa’ ni kukushauri na kukunasihi kama ni ndugu yetu katika Uislamu kuwa maadamu unachokitaka ni cha kheri na ni katika kilichosisitizwa na dini hasa kwa mwenye uwezo nacho, basi kama hali yako kama hiyo ‘nikitaka kuolewa’ siku za mbele kwa maana kuwa hakutokeza wa kukuchumbia bado lakini una tamaa na una wasi wasi na wazazi wako kwa sababu moja au nyengine au kwa kuwadhania tu -sio kuwa mtu kaja kwa wazazi wako na kutaka kukuposa- jambo la kwanza la kukushauri na kukunasihi ni kutokuwa na dhana mbaya juu ya wazazi wako, la pili ni kuwa ni vyema uelewe kuwa wanachokutakia wazazi wako katika maisha yako yote ni kila la kheri na katika hayo ni kuhakikisha kadiri ya uwezo wao kuwa unaolewa na mtu mwenye sifa zinazotakiwa na Uislamu.
Hivyo basi kama atakuja watakayemridhia dini yake akhlaaq zake sifa zilizopendekezwa na mwenye kupendwa na kila Muislamu, basi wao hawatakuwa na pingamizi kwani ni haramu kwao wao wakati huo kwenda kinyume na ushauri huo wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ni wenye kumuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah.
Hivyo basi katika Uislamu akitokezea mume kama anavyoelezwa na kukubalika sifa zake haitokuwa vyema bali ni haraam kwa wazazi kukataa kumuozesha kwa sababu kuwa mtoto wa kike anasoma; kwani kuolewa na kusoma ni mambo yanayoweza kwenda sambamba bila ya tatizo lolote lile, ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akashauri :
“Atakapokujieni mtakayeridhia dini yake na tabia zake basi muozesheni; na kama hamtofanya hivyo basi itakuwa ni fitina katikia ardhi na ufisadi” wakasema ewe Mjumbe wa Allaah: hata kama atakuwa na ... Akasema Mjumbe wa Allaah: Atakapokujieni mtakayeridhia dini yake na tabia zake basi muozesheni mara tatu” Imepokelewa na At-Tirmidhiy, kitabu cha ndoa, mlango wa katika yaliyokuja atakapokujieni mwenye kumridhia dini yake basi muozesheni.
Umesema, ‘wazazi wanataka mpaka nimalize shule’, Uislamu uko wazi kuwa kumaliza masomo au kuendelea kusoma si katika sababu kutotaka mtoto wa kike asiolewe; wala si katika sababu pia kutotaka kuolewa mpaka upate kazi, kwani si kila mwenye kumaliza masomo hupata kazi na wala si kila mwenye kumaliza masomo huolewa.
Ni vyema tuelewe kuwa ndoa si jambo linalotegemea kumaliza masomo wala kupata kazi, bali ni jambo linalotokea na kupatikana bila ya kuangaliwa yote hayo, na ni vyema tuelewe kuwa kuolewa kuna wakati na ukipita wakati wake huenda ukaondokea bila ya kuolewa, ama masomo au kazi hayana wakati wa kuambiwa kuwa sasa huwezi kusoma au sasa huwezi kutafuta kazi.
Pia ni vyema tuelewe kuwa, mtoto akiweza kufikia kuweza kusoma na kuandika na kuwa na uwezo wa kusoma Kitabu cha Allaah na kukielewa na kusoma Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huwa inatosheleza kwani yaliyobakia ni nyongeza na nyongeza sio muhimu kwa kila mtu, isipokuwa kama itakuwa elimu inayotakikana na jamii na hapana wenye elimu hiyo katika jamii kama vile tabibu na kadhalika basi hilo anaweza mwanamke akashurutisha kwa huyo anayetaka kumuoa vyenginevyo si halali kukataa kuolewa kwa visingizio kuwa bado mtu anasoma au bado hajapata kazi.
Ukaeleza, ‘hapa nilipo nina miaka 23, sasa nifanye nini? na ndoto zangu ni kuolewa na mtu anaeijua dini na sheria zake akizifata’ Allaah Atakupa kila la kheri na mwenye kheri na wewe na Atakujaalia uwe katika wenye kufuata yenye kukuridhishaa wewe na huyu atakayejaaliwa kuwa mwenzako katika maisha. Cha kufanya ni kukaa kikao cha ushauri na wazazi na kuwaelza hayo tuliyokueleza wewe na kama hapatakuwa na maelewano wala mawafikiano ya kuwapelekea kuufuata ushauri wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na sio ushauri wako wewe, basi unayo haki ya kwenda kupeleka mashataka yako kwa Qaadhi kama yupo ulipo, au kwa Shaykh au kiongozi wa dini anayeaminika, na atatoa uamuzi ambao bila ya shaka yoyote ile utakuwa kama huo tulioutanguliza kama hali itakuwa kama ulivyoieleza.
Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:
Wazazi Hawataki Nifunge Ndoa Hadi Nimalize Kusoma Nami Niko Katika Zinaa, Nifanyeje?
Kukosa Radhi Za Mzazi Kwa Kuolewa Na Asiyetakiwa Na Mzazi Bila Sababu Za Kisheria
Na Allaah Anajua zaidi