Ametenda Naye Maasi Ya Liwati Kisha Wametubia Sasa Anataka Kumuoa Je Inafaa?

 

SWALI:

 

Assalaam-aleykum, hakika hakuna Mola apaswaye kuadudiwa kwa haki isipokuwa ALLAAH subhanna wattaala na nakiri ya kwamba Muhammad s.a.w ni mja na ni mtume na nimjumbe wake. haki zote anazimiliki yeye Muumbaji wa mbingu na ardhi na kila kile kilichopo duniani.

nilikuwa na mpenzi wangu wa kike ambaye alikuwa na tabia ya kufanya kinyume na maumbile tendo ambalo nilijikuta na mimi nimefanyishwa, nilikuja kujua LAKINI nikaendelea kufanya..nimemuomba MOLA anisamehe na kuniepusha pia huyo binti ametubu na kuomba kuepushwa. NA tunataka kufunga ndoa ilikuepuka zinaa.    SWALI LANGU; JE WARUHUSIWA KUFUNGA NDOA NA BINTI AMBAYE MLITENDA NAYE KINYUME NA MAUMBILE????.

Natumai nitapata jibu la kheri ambalo ndilo nitakalolitumia kati ya mimi na binti huyo.

Maa'salaam".. ahsante


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ni jambo la kheri kutubia na ndio tulivyoamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama Anavyosema:

“... Na tubuni nyote kwa Allaah, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.” An-Nuur: 31

 

Ni tegemeo la kila Muislamu kuwa Allaah Atakubali tawbah zetu na za Waislamu wote kwa ujumla na huko ndiko kufanikiwa.

 

Ndugu yetu unahitaji tawbah kwa yote uliyokuwa nayo kuanzia ulivyosema kuwa, ulikuwa na mpenzi, na sio kwa hilo tendo pekee kwani hili pia lilikuwa ni kosa katika Uislamu.

 

Tawbah kama ilikuwa ya kweli bila ya shaka yoyote ile hufuta yaliyotangulia na inshaAllaah hukubaliwa na Mola; hivyo basi huwa hakuna pingamizi kutekeleza jambo la halali baada ya kuleta tawbah nasuuhah.

 

Ilikuwa vizuri na jambo jema uepukane na huyo mwanamke aliyekupeleka kufika kutenda maasi kama hayo uliyoyatenda na kama unaona kuwa huna njia isipokuwa umuoe na kuhakikisha kuwa uchafu wenu hamtourejea tena basi hakuna pingamizi katika kuoana kwenu baada ya kufanya tawbah ya kweli kweli na kupita kipindi cha kuonekana athari za mabadiliko yenu baada ya tawbah.

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Mwenye Kufanya Maasi Ya Liwati Anaweza Kurudi Kwa Allah Kutubia?

Mume Mwenye Tabia Chafu Ya Liwati Anafaa Kuwa Imaam? Je, Inafaa Kumuozesha Mke?

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share