Mke Kutohisi Chochote Katika Tendo La Ndoa

SWALI:

 

Assalam alaykum warahmatullah, vipi hali zenu? Poleni kwa kazi zenu tunawaombea Allah awajalie wepesi na awalipe pepo, kwa kweli tunaridhika na misaada yenu kwa kutupa elimu ya dini yetu; ndie mana nimechukua hiyi fursa ya kuwaandikieni ili niwaulize maswali ambayo yananitatiza; Swali la kwanza linahusu maisha yangu ya ndoa mimi ni mwanamke nilitaka kufaham kama kuna dua yoyote naweza kupata ao msaada ungine kuhusu tatizo langu ambalo ni hili: nikiwa kwenye tendo la ndoa kwa kweli siwagi na hisi kitu chochote zaidi ya kumridhisha mme wangu tu, mpaka nakua najihisi vibaya sijui ni tatizo gani, tangu niolewa ni hivo hivo, naomba msaada wenu inshaallah Allah atawalipa kheri.

 

Wassalam alaykum warahmatullah


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kutohisi chochote kwako katika tendo la ndoa pamoja na mumeo.

Hakika hili ni tatizo kwa baadhi ya wanawake. Tatizo hilo hupatikana ima kwa hali ya hewa ya baadhi ya maeneo duniani, maumbile ya mwanamke, ugonjwa, bwana kutojua kuendesha na kumpandisha mkewe au kwa ajili ya kukeketwa (kutahiriwa mwanamke akafekwa kila kitu).

 

Katika hali zote hizo inabidi mwanamke aende kwa daktari au kwa twabibu anayetumia madawa ya asili ili aweze kumpatia dawa kuhusu tatizo hilo. Matwabibu ni bora zaidi kwa sababu dawa zao huwa hazina madhara kwa mwili wa mwanaadamu. Na pia mwanamme awe ni mwenye kufundishwa ni njia gani ataweza kutumia ili kuweza kupandisha hisia zake.

 

Na ikiwa ni tatizo kwa upande wa mwanamme, basi mwanamme amefundishwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asiwe ni mwenye kukuingilia tu kama mnyama bali afanye yafuatayo:

 

1.     Azungumze nawe maneno matamu na mazuri yanayohusiana na kitendo chenyewe.

2.     Akubusu busu na vitangulizi vyengine kama kukushika maziwa na sehemu nyeti kabla ya kufanya kitendo chenyewe.

3.     Hisia zikipanda ndio muanze tendo lenyewe.

 

Kufanya hivyo, kutatatua kwa kiasi kikubwa tatizo lako hilo.

Na zaidi utayapata maelezo ya wazi na mengi katika kitabu kifuatacho:

 

Zawadi Kwa Wanandoa

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share