Mtoto Aliyezaliwa Nje Ya Ndoa Nani Walii Wake Na Mwenye Jukumu Naye? Allaah Atamsamehe?

SWALI:

 

Asalamalkum,

 

Nina maswali matatu kuhusu mtoto wa nje ya ndoa (mtoto haramu).

 

1. akitaka kuolewa au kuoa nani anaetoa idhini?

 

2. je kama alishaolewa na akaachika kuolewa tena mara ya pili anaweza kuolewa bila kutaarifu kwao?

 

3. kama mtu aliolewa akiwa ana uja uzito mchanga wa week 4 kwa kuficha aibu yake lakini bila kujua kama hairuhusiwi kuolewa ukiwa na uja uzito na wakazaa watoto 2 na kisha akatengana na mumewe ndipo alipotambua kwamba hawakutakiwa kuowana wakati akiwa na uja uzito je? watoto hawa 2 wote ni wa haramu? Na nani mwenye haki ya kuishi na hawa watoto? Je kuna msamaha juu ya jambo ili mbele ya Allah subuhana wa taala.

 

naomba sana ufahamisho katika maswaala haya

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa maswali yako kuhusu ndoa.

Muislamu kwanza anapaswa kufahamu kuwa hakuna mtoto haramu kwa kuwa kishari’ah mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa si mwana haramu bali kitendo ndicho kilicho haramu.

 

Mtoto hana makosa kabisa mbele ya shari’ah na anapokuwa mkubwa na akawa mwema basi wema wake utamuingiza yeye Peponi. Huyu mtoto anaitwa mtoto wa kitanda.

 

Mtoto huyo aliyezaliwa kwa watu wawili waliofanya zinaa akiwa ni mvulana akitaka kuoa hahitaji idhini ya yeyote. Anaweza kupelaka posa mwenyewe au akapelekewa na jamaa zake upande wa mama. Ama msichana anapotaka kuolewa basi kwa kuwa hana wazazi wa kuumeni, Qaadhi akiwepo hapo alipo atakuwa ndiye walii wake au Imaam au Shaykh.

 

Ikiwa mwanamke huyo ameolewa kisha akaachwa akiwa anata kuolewa mara ya pili itabidi asirudie kosa la mara ya kwanza afuate njia zilizowekwa na shari’ah. Miongoni mwazo ni yeye kukubali kuolewa na huyo mume, kuwepo kwa walii na mashahidi wawili waadilifu.

 

Kuolewa akiwa mwanamke ana uja uzito haifai lakini ikiwa kumefanyika kwa kutokujua Allaah Aliyetukuka Anasemehe hilo.

 

Hata hivyo, baada ya kujua ni lazima mke huyo amwambie mumewe kuwa walifanya makosa kuoana akiwa na mimba, kumaanisha huyo mtoto aliyezaliwa si wa baba huyo kabisa. Ama hiyo Nikaah iliyofungwa katika hali hiyo ya uja uzito itakuwa sio sahihi na hivyo mnapaswa mjivue kwenye ndoa hiyo, mtubie na kisha baada ya toba ya kweli mtaweza tena kufunga ndoa upya.

 

Baada ya kujulikana hilo, ingawa mume hatokuwa na madhambi kwa kufichwa jambo hilo, ila mke atapata madhambi kwa kumficha mumewe.

 

Ama watoto waliozaliwa baada ya hapo watakuwa ni watoto wa wanandoa hao wawili. Ikiwa mtoto mmoja kati ya hao wawili ni yule aliyekuwa tumboni wakati wa ndoa huyo ndiye atakayekuwa si mtoto wa huyo baba lakini ni mtoto wa mama. Hivyo huyo wa pili ndiye atakayekuwa wa huyo baba.

 

Mama ana haki ya kuishi na yule aliyekuwa tayari matumboni wakati wa ndoa na huyo wa pili pia akiwa ni mdogo. Mwanamke huyo akiolewa huyu baba atakuwa na haki ya kukaa na huyu mtoto wapili.

 

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Watoto Baada Ya Ndoa Ya Uzinifu

 

Nini Hukmu Ya Watoto Wa Nje Ya Ndoa?

 

Nimeolewa Huku Nina Mimba Nini Hukumu Ya Mtoto Wa Kitendo Cha Zinaa?

 

 

Mtoto Aliyezaliwa Nje Ya Ndoa Vipi Anaweza Kutambulishwa Kama Ni Mtoto Wa Nani Kwenye Ndoa Yake, Na Ataandikishwaje Kwenye Cheti

 

 

 

 Ama kuhusu kutubia maasi haya ni kwamba Allaah Hupokea toba ya mja Wake kwa maasi yoyote kwani yeye ni Mwingi wa Kughufuria.  Linalopasa ni kufanya toba ya kweli ambayo mashari yake kama yafutayo:

1.    Kuomba maghfira  

2.    Kuacha  hayo maasi

3.    Kujuta na kuweka nia (azma) kuwa hatorudia tena

4.    Kuzidisha vitendo vyema

5.    Kama kaidhulumu haki ya mtu basi ni kuirudisha hiyo haki.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Tawbah

 

Tawbah Ya Kweli Na Masharti Yake

 

Ndoa Baada Ya Kutubu Zinaa

 

Kumuoa Aliyezini Baada Ya Kutubia

 

Wazinifu Waliotubu Wanaweza Kufunga Ndoa Na Waliotakasika

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share