Swalaah Ya Jamaa Baina Ya Mume, Mke Na Mtoto Wa Kiume

 

 

Swalaah Ya Jamaa Baina Ya Mume, Mke Na Mtoto Wa Kiume

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI

 

 

Nilitaka kujua tu kama nitasali jamaa watu wawili lakini mke na mume au mtoto wa kiume na mama yake, jee ni vipi tunatakiwa tujipange?  ukizingatia mmoja (mwanamke) atakua nyuma pekee yake hakuna ubaya wowote?

 

 

 

JIBU

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Katika Swalaah ya jamaa‘ah ambayo ina mchanganyiko wa wanawake na wanaume, inatakiwa wanaume wawe mbele na wanawake nyuma yao na watoto wa kiume wanakuwa baina ya jinsi hizo mbili.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)    alikuwa akiwapanga wanaume nyuma yake, na nyuma yao watoto na nyuma ya watoto wanawake [Ahmad na Abuu Daawuwd]

 

Pia,

Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    amesema: “Safu bora kwa wanaume ni za mbele (mwanzo) na zilizo mbaya zaidi ni zile za mwisho. Na bora ya safu za wanawake ni zile za nyuma na zilizo mbaya kwao ni zile za mbele”  [Al-Jamaa‘ah isipokuwa Al-Bukhaariy].

 

 

Na hadithi nyengine ni ile iliyopokewa kwa Anas  (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: “Tuliswali mimi na yatima katika nyumba yetu nyuma ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)     na mama yangu, Umm Sulaym (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)    alikuwa nyuma yetu”.

 

Na katika lafdhi nyingine:

“Tukapangwa safu nyuma yake (yaani nyuma ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mimi na yatima na mkongwe mwanamke nyuma yetu.”  [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Kwa mujibu wa Hadiyth hizi ni kuwa inatakiwa mwanamke awe nyuma ya mtoto wa kiume ikiwa amefika miaka ya tamyizi (kuanzia miaka saba mpaka kubaleghe). Ikiwa yuko chini ya miaka hiyo wanaweza kuswali safu moja bila ya matatizo. Hivyo kulingana na swali hilo mume atakuwa Imaam, mtoto wao atakuwa nyuma yake na mke atakuwa nyuma ya mtoto peke yake. ikitokea akaingia mwanamume basi atafunga safu na mtoto huyo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share