Ubia (Shares )

SWALI:

Je, uko uhalali wa Muislamu kuingia katika ubia (hisa/ Shares)? Kama uko uhalali basi naomba nifahamishwe.

Wabillahi at-Tawfiq.


 

JIBU:


 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Tunamshukuru ndugu yetu kwa kuwa na thiqah na sisi kwa kutuletea swali hilo juu.

Uislamu ni Dini ambayo imemuelekeza Muislamu na mwanadamu anayetaka uongofu katika njia ambazo zitampatia yeye ufanisi hapa duniani na kunali saada kesho Akhera. Katika hilo Uislamu umeweka kanuni kabambe ambazo zinamlinda mwanadamu asije akadhulumiwa au akadhulumu. Uislamu hautaki mtu yeyote adhulumiwe au adhulumu na pia alete madhara au aletewe madhara.

Katika msingi huu Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

}}وَإِن تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُؤُوسُ أَمْوَالِكُمْ لاَ تَظْلِمُونَ وَلاَ تُظْلَمُونَ{{

{{Na mkitubia, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe}} [Al-Baqarah 2: 279].

Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Haifai kudhuru wala kulipana madhara)) [Hadith Hasan iliyopokewa na Ibn Maajah, Maalik na Ad-Daraqutniy].

Na Allaah سبحانه وتعالى Amesema katika Hadithi Qudsiy:

((Enyi waja Wangu! Mimi nimejiharimishia dhulma juu ya nafsi Yangu na nikaifanya ni haramu baina yenu, basi musidhulumianen)) [Muslim].

Sasa tukiangalia kuhusu jambo hili la hisa katika kampuni, mambo matatu yanapatikana:

1.    Faida inapatikana nyingi lakini mwenye hisa anapatiwa kiwango kidogo, hivyo anadhulumiwa katika mgao.

2.    Faida inapatikana kidogo lakini kampuni inalazimika kutoa kiwango kile kile walichoafikiana na mteja. Hivyo kampuni inakuwa imedhulumika.

3.  Huenda kampuni ikapata faida sawa sawa na viwango walivyo kubaliana hivyo hakuna anayepata hasara, lakini hilo si katika matakwa ya kampuni.

Mara nyingi inakuwa mmoja kati yao anadhulumiwa, hivyo kufanya ununuzi wa ubia kuwa haramu katika Uislamu. Kishaa ni yenye kujulikana wazi kuwa daima mwenye kununua hisa anapata faida hata kampuni ikienda hasara kwa sababu moja au nyengine na hili ni jambo ambalo halifai kisheria. Ni jambo linalojulikana kuwa hakuna biashara inayopata faida kila wakati katika ulimwengu huu wetu. Na hutokea wakati mwengine ukapata faida na mara nyengine ukapatwa( yaani hasara).

Lakini ili shughuli hii ikubalike kisheria inatakiwa itemize masharti yafuatayo: -

1. Isitumie (kuchukua au kutoa) riba kabisa katika biashara yenyewe. Riba imeharamishwa kabisa katika Uislamu na anayefanya hivyo basi ameandaa vita na Allaah سبحانه وتعالى na Mtume Wake صلى الله عليه وآله وسلم.

2.  Iwe mteja (mnunuzi wa hisa) atapata hasara pindi kampuni inapopata hasara na kupata faida sawa pindi kampuni inapopata faida.

Lau moja kati ya masharti haya hayatopatikana basi ununuzi wa ubia utakuwa haramu.

 

Wa Allaahu A'alam

 


Share