Fulana Zenye Nembo Ya Klabu Za Mpira
SWALI:
Asalam aleykum
ni nini hukumu ya kuvaa fulana zenye nembo ya klabu za mpira
JIBU
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Jazakallahu khayran kwa swali hili kutoka kwa kikundi chenye jina hapo juu.
Ikiwa fulana zina nembo ambazo zinaruhusiwa kisheria basi hazina neno wala hakuna tatizo lolote kuhusu
1) Tangazo la kitu au vitu haramu mbele au nyuma yake.
2) Maandishi nyuma ya fulana kwani humshughulisha mtu anayeswali nyuma yake na kumwondolea khushui (unyenyekevu). Na katika hili Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam ) amekataza kuswali na nguo yenye picha au marembo mbali mbali (Al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Mama ‘Aishah [Radhiya Allaahu 'anhaa]). Na mara nyingi huwa tunavaa fulana hizi kwa kuwa sisi ni mashabiki wa timu hizo na zikiwa zinacheza basi huwa tunaswali na huku tumezivaa.
3) Mavazi hayo hayatakiwi yafanane na mavazi ya kikafiri kwani
((Enyi mlio amini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa vipenzi vyenu ikiwa wanastahabu ukafiri kuliko Imani. Na katika nyinyi atakaye wafanya hao ndio vipenzi vyake, basi hao ndio madhaalimu))
((Sema: Ikiwa baba zenu, na wenenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyo yachuma, na biashara mnazo ogopa kuharibika, na majumba mnayo yapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Allaah na Mtume wake na Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Allaah Alete amri Yake. Na Allaah Hawaongoi watu wapotovu)) (At-Tawbah: 23 -24)
Hivyo, ni bora tujiepushe kuvaa fulana hizo ili tusije tukaingia katika matatizo tuliyoyataja.
Na Allah Anajua zaidi.