SWALI:
Assalaam alaykum. Assalatu wassalaam ala rasulillah. Napenda kupata maelezo toka kwako(kwenu) kuhusu haki ya mzazi na haki mwana na yafuatayo ni maelezo ambayo nimejaribu kuyaeleza kwa jinsi yalivyotokea upande wangu, baba yangu na wenzangu(ndugu zangu) ni kisa cha kweli na huenda kikawa cha kushangaza kwangu na kwenu pia.
Mimi ni mmoja wa vijana ambao najaribu kulinda haki za wazazi wangu nikizingatia na kufuata maelekezo ya kitabu chetu Qur’an na hadithi za mtume(S.A.W). Najua umuhimu wa wazazi wangu wawili katika maisha yangu ya hapa na kesho akhera. Lakini, imefikia kiwango cha baba yangu kufanya mambo hata ndugu zake na jamaa zake kutoelewa nini malengo yake. Na ninapowafuata ammi zangu(ndugu zake) baadhi wanasema kuwa sio yeye bali ni mkewe anayemwendesha, na baadhi wanadai kuwa ni kafanyiwa mambo ya ushirikina na mkewe ili afuate anavyotaka mkewe lakini mimi nasema Allaah ndio anayejua yakini zaidi yetu.
Mimi ni kijana wa kiislamu nimeoa nina mke mmoja na nimejaaliwa naye watoto wanne(2 wakiume na 2 kike). Najaribu kwa kila hali kuwa mwenye subira ya hali ya juu na kufuatilia dini yetu ipasavyo kwa kadri ya uwezo wangu katika maisha yangu na familia yangu. Mke wangu ni mama wa nyumbani lakini alhamdullillahi ni mwanamke mwenye kumuogopa Allaah(SW) kuliko mtu mwingine au chochote. Wote tunaishi sasa karibu zaidi ya miaka kumi katika mafundisho Allaah(SW) na uwongo sio tabia zetu sote na nashukuru hata watoto wetu wanachipukia kwa kuwa mbali na tabia ya uwongo. Hivyo, nashukuru Mola (SW) na namuomba aiongoze familia yangu katika mema na aiongoe na mabaya na machafu yote inshAllaah- Ameen.
Baba yangu amepata bahati ya kuoa wake zaidi ya watatu lakini alikuwa ni mwenye kubaki na kati ya wawili au watatu katika ndoa nao. Na alibahatika kupata watoto na wake watatu tu na kila mke alikuwa na watoto naye kuanzia watatu, wanne na wanane kwa mke wa mwisho.
Mke wa kwanza alimtelekeza kwao, na wawili aliwaoa nje ya kwao. Mimi kama mtoto kubwa kwa mke wa pili(kati ya wanne) nilikuwa nikukuwa ki umri huku nikiona muamala kati yao ilikuwa sio sawa wala hakuna mizani(adala) kati ya wake zake hadi watoto zake. Mfano, mke wa kwanza mpaka leo inaweza kufika zaidi ya miaka 20 hajampa haki ya mapenzi ya mume na mke na alikuwa mbali naye sana kipindi kirefu. Sasa zaidi ya miaka 4 yupo karibu naye pia hakuna haki ya mapenzi aliyompa pia, siyo hivyo tu hata matumizi yake na watoto wake hawakuwa anawapa bali kuna baba zangu wakubwa na wadogo walikuwa wakifanya kuwasaidia matumizi lakini nao familia zao zilipozidi kukuwa walishindwa kuendelea kuwasaidia, naweza kusema kuwa anachojali baba yangu na muhimu ni maisha yake na raha yake kuanzia kula mpaka kulala yake ndio muhimu sana kuliko chochote kile. Watoto pia hali ni mbaya kuliko anavyowachukulia wake zake kuna wale afadhali na wale maskini wanaosukuma siku ili ufike wakati wakajitegemee. Watoto wa mke wa pili(mimi na wadogo zangu) baadhi walikuwa wanaishi kwa mama yao wakambo(mke watatu-mwisho) sababu ya mama yao mzazi aliachika na baadhi yao walikuwa wadogo kiasi ilibidi waishi na mama yao mzazi lakini pesa aliyokuwa anayotoa kwa hawa watoto waliopo kwa mama yao ilikuwa sio ya kutosha kuendesha maisha ya mwezi na kuwacha mama(aliyowachwa) kuuuza baadhi ya vitu vyake vya thamani ili kutosheleza matumizi ya mwezi ya watoto wake. Mimi na mdogo wangu anayenifuata tulikuwa ni kati ya wale tuliokuwa tunaishi kwa baba(mama wa kambo) mjini ili kujaribu kupata elimu ambayo itaweza kutusaidia katika kututafutia maisha. Maisha yalikuwa magumu sana kwa mama wa kambo. Baba yetu naye alikuwa hawezi kuyarekebisha ugumu wa maisha yetu hapo kwa hali yeyote ile kwani hapa ilikuwa Annisaa qawamamuuna ala rijaalun na sio Arrijalun qawamuuna ala nisaaun. Mimi ikanilazimika kuanza kutafuta kufanya kazi baada ya kumaliza kidato cha sita(High School) japo nilikuwa naenda kupata nafasi ya kusoma elimu ya juu nchini IRAN lakini ili kumuhudumia mama yetu kwani nilihisi kuwa baba huenda akakata matumizi aliyokuwa anawapatia wadogo zangu pindi watakapo toka chini ya mama kama vile mtoto wa kike kuolewa na mwingine kuhamia kwa mzee ili kupata elimu ya sekondary. Na kweli hayo yalitokea kama nilivyokuwa nashuku(baba alikata matumizi alipoolewa mdogo wangu wa kike na wakiume kuhamia kwa baba ili kupata elimu ya secondary).
Hivyo nilianza kubeba jukumu la kumuhudumia mama yetu baada ya baba kukata matumizi. Pia nilikuwa napata mashtaka toka kwa wadogo zangu waliokuwa wamebaki kwa baba(chini ya malezi ya mama wa kambo) wakinilalamikia dhidi ya baba kutokuwa na uadilifu na mateso(kulikuwa na wafanyakazi/wasadizi nyumbani 2-4 lakini hawakuruhusiwa kusafisha chumba wala nguo zetu) , kero na dhulma ya kila aina ilikuwa inafanywa na mama wetu wakambo dhidi yao, lakini nilikuwa sina lakufanya zaidi ya kuwausia wasubiri kwani kila matatizo yana mwisho na waishi kama wageni japo kwa baba yao ili wamalize elimu ya secondary tu kisha wakatafute riziki zao nao kama nilivyofanya mimi.
Allaah(SW) alinijalia kupata ajira nzuri ya kutosheleza matumizi hata ya mama na familia yangu ikapita zaidi ya miaka 10 hivi mzee kwa bahati mbaya akawa amefanya vibaya kimaisha ikabidi auze duka na nyumba na vyote anavyomiliki na arudi kwao na ndipo ninapoishi na kufanya kazi sasa mimi. Baba alikuwa na pesa kiasi cha kufanya biashara na kuendesha maisha bila ya kumtegemea mtu lakini alijaribu kunieleza kuwa hana kitu wakati sio ukweli, na pindi anapohitaji vitu vya gharama vya nyumbani ananua na inaniwacha nishangae na kushindwa hata kumuuliza kwani sio tabia yangu kudadisi ya mtu. Kabla ya kuja baba na baadhi ya wadogo zangu wengine. Nilianza kuwapokea ndugu zangu kwa baba(kwa mama wa kambo)wawili wa kiume walikuwa na umri 20(mapacha) na mmoja wa kike umri wake ulikuwa 15. Nikawa naishi nao pamoja na familia yangu. Nilijaribu kwa kila hali kuhakikisha uadilifu juu yao na hata ikafikia wakati kutonunua mavazi mapya ya Eid kwa ajili yangu mimi na mke wangu ili kuhakikisha wadogo zangu wanapata mavazi ya Eid na kutojisikia unyonge au tofauti kimaisha na kuhakikisha wapo katika furaha kama vile wapo kwa wazazi wao. Sikuwa nawabagua kwa hali yoyote wala sikuwa na kinyongo na niliyofanyiwa na mama yao hata na baba yangu kwani nilikuwa naamini kuwa wao sio wahusika na niliyotendewa. Lakini vijana walilelewa katika maadili ya kuwa udugu ni kwa mama tu, kwa baba sio udugu halisi na hii walikuwa wanazungumza mbele yangu nikawa nawachulia kama akili ya ujana. Lakini mambo yalikuwa yakizidi kuwa mabaya siku baada ya siku huku mimi nikistahamili na kusema bora wazazi wao waje niondoke nikaishi na familia yangu katika nyumba nyingine. Mmoja wa mapacha alipata ugonjwa wa TB na akazidiwa hadi kufikia moja ya mapafu yake kusimama. Nasikitika kusema kuwa nilitumia uwezo wangu wote kimali, kiakili na hata nguvu zangu kumsaidia. Nikaomba mama yake au waliobakia pamoja na mzee waje haraka kwani ilibidi wazazi wake wote wawepo karibu naye kunisaidia kumhudumia kwani nilikuwa nakwenda mwezi kazini na mwezi nipo livu. Baba yangu katika mawasiliano naye ili waje akaanza kutumia udanganyifu kuwa hana uwezo wa kusafirisha wote ili ajaribu kuniwacha nitoe pesa za nauli zao za kuja kwao huku, kutokana na mikakati yao kuwa waokowe pesa zao na zitumike zangu. Wakati ananijaribu kwa hilo wao walikuwa watalazimika kuja(kwa kuhama) kimaisha yaani daima sio baada ya miezi mitatu tokea sasa.Nikamueleza wazi sina uwezo huo na sioni kama kuwa ni wakati wa kujaribiana kwani mimi nipo serious hivyo sioni sababu ya kujaribiana bali fanyeni haraka sana kwani kundelea kuchelewa kwenu kutasababisha kuteketea zaidi afya yake mgonjwa. Hivyo, baada ya mfupi tu walikuja mama yangu wa kambo na wadogo zangu waliobakia watano kasoro baba alikuwa anamalizia makaratasi ya mikataba ya mauzo ya mali zake. Niliwapokea na nikawapa huduma zote kwa kadri ya uwezo wangu nilisimamisha ujenzi wa nyumba yangu na kutumia hata akiba yangu ili kuongoza nyumba badala ya baba yangu. Muda wa siku chache tu mama yangu wakambo na wadogo zangu(watoto zake) walianza vituko na kero kwa mke wangu na watoto wangu(mimi nikiwepo au sipo) na ikafikia hata mwishoni mmoja wao kumwagia mafuta ya kupikia(uzuri hayakuwa ya moto) mke wangu akiwa chumbani (bed room) nah ii ilikuwa kabla ya siku mbili tu kujifungua mke wangu na mimi nikiwa kazini(mbali). Alivyojaribu mke wangu kunipigia simu kunieleza yaliotokea nyumbani walimkatia simu.
Nikapigiwa simu na majirani na nikawaeleza basi ande kwa wazazi wake ili kuepusha shari, japo kwa wazazi wake palikuwa mbali na tunapoishi na hakuwa mtu wa kumpeleka inavyobidi katika uislamu na ilitakiwa ajifungulie hospitali kwa sababu inabidi apigwe sindano ya anti-D kama mtoto aliyezaliwa kafuata damu yangu. Muhimu alielekea kijijini kwa wazazi wake baada ya siku mbili nilipigiwa simu kuwa nimepata mtoto wa kiume(Alhamdulillah) nyumbani kwao na sio hospitali kama inavyotakiwa kwani ni mbali na hospitali.
Baba alikuja na nilitegemea angemaliza matatizo yaliofanywa na wadogo zangu na mama yao. Lakini nilisikitika sana kuona baba yangu hatambui matatizo yangu na kuanza kunitaka pesa za matumizi yake na wadogo zangu nyumbani kwake. Nikamuomba anirudishie mke wangu ambaye aligoma kurudi mjini tunapoishi sababu kuwa mimi si mwanamme wa kuishi/kutunza mke bali ni mwanamme wa kuishi/kutunza ndugu na wazazi wangu tu. Pia baba mkwe wangu aligoma kumwacha mke wangu kurudi nyumbani baada ya kusikia matatizo yaliotokea kwa binti yangu. Yote haya yanatokea malengo ya mama wangu wa kambo kuona mimi ninagharamia familia ya mzee na yangu ili nishindwe kumtumia mama yangu matumizi yake na hata kushindwa kuendelea na ujenzi wa nyumba yangu. Nikasema sio kitu ngoja nijaribu kuwatia wakubwa kwani huenda mambo yakatengemaa. Nikamleta kaka yake baba(ammi yangu) ili nijue kama nyeupe au nyeusi kwani mwanzo nilikuwa nimewekwa kwenye rangi ya majivu(grey). Ammi yangu akatupatanisha kuwa mimi na familia yangu nikae chini(basement) kama anavyotaka baba yangu japo hapafai kimaadili ya kiislamu kwani kila anayepita anaona familia yangu ndani na kihewa ni joto sana mtu kuishi chini huku ukilinganisha na hali ya hewa ya huku wakati wajoto temperature inafikia 45-49C na mzee akae juu na familia yake. Na nimpatie pesa za matumizi (idadi kubwa kiasi kwangu ilikuwa lakini Nilikuwa naamini subira ni bora) mpaka baba au mmoja wa wadogo zangu atakapoanza kazi basi itabidi mkataba ubadilike. Nilianza kuwatafutia kazi wadogo zangu baada ya mwaka na nusu nikafanikiwa kuwaingiza kazini mmoja baada ya mwingine.
Nilivyoona wametulia kazini nikamuita baba nikakaa kitako naye na mke wangu(mtoto wa ndugu yake) nikamueleza kuwa wadogo zangu sasa wanafanya kazi, naona bora munipatie fursa sasa ya mimi kuendelea kujenga nyumba yangu kwa kunipunguzia(sio kukata zote) pesa za matumizi ninayowapeni na ukijali miaka miwili sasa mimi nimesimamisha ujenzi. Mzee aliruka kama amechomwa na mwiba, alidai kuwa anataka kuona wana save pesa zao zote wadogo zangu ili wapate kuoa. Nikamueleza baba yote kuoa ni kheri na kujenga ni kheri na usisahau wakati wa harusi zao bila shaka watahitaji mchango toka kwangu na mimi sina budi kama kaka yao niwapatie mchango kama nitaendelea kuwa hivi basi hata huo mchango nitautolea wapi?, ukijali vijana bila pesa udugu utakuwa umeyeyuka kwa jinsi ya maadili ya malezi yao. Hakunielewa kabisa na hakutaka kufanya adala kati yetu ya kusaidiana katika kumpatia matumizi japo hivyo ndivyo ulivyokuwa unasema mkataba aliouweka ammi yangu kati yetu.
Nikamueleza kuwa kama hakuna adala basi baada ya miezi mitatu kutoka leo nitapunguza pesa za matumizi ninazolipa na nitalipa nusu na nusu watoe wadogo zangu kwani wao wanaishi na nyinyi na wanafanya kazi sasa, hakuridhika kabisa na akaanza kupanga mikakati kunifungulia kesi ya kuwa nimechukua pesa za mkewe na kuwa eti sitaki kurudisha akaanza kesi hiyo kwa wakubwa wa kabila letu bila kupitia ndugu zake(ammi zangu) huku akiniahidi kuwa nitakuchafua jina lako na kukufitinisha na jamaa zetu wote!!!!. Akawa ananiahidi na kunitishia kunitia uchizi kama alivyomtia mama yangu na mdogo wangu baada yangu!!. Nilichofanya ni kusubiri na kuendelea kufuatilia kesi yake. Nilithibitisha kwa barua na e-mails nilizokuwa nimezihifadhi nilivyokuwa nawasiliana na mzee na mama yangu wa kambo kuhusiana na pesa na nikathibitisha sio ukweli madai yake na pesa zilikuwa zake alinipatia ili nifanyie matengenezo nyumba aliyonunua na hesabu na risiti nilimtunzia na kuzikabidhi kwa mkuu wa kabila. Hatima yake ikawa ni fedheha kwa baba alipoambiwa kuwa kabla ya kutekeleza hukumu basi alitakiwa aape kiapo cha yamini kuwa pesa sio zake na ni za mkewe, na mimi nitatakiwa kuapa yamini pindi hatapoamini kuwa hesabu nilizotumia katika ujenzi tokana na hizo pesa ni sawa na kweli. Muhimu aliruka baba na kusema “sikubali kuapa na sitambui hukumu yako kabisa”. Hapo ikathibitika kuwa alikuwa anajaribu kutaka kunichafulia jina langu wakati kesi haina ukweli hivyo alishindwa na kuondoka. Haya bila shaka mama yangu wa kambo hayakumridhisha kabisa na baba akawa anajaribu kutafuta kila njia ya matatizo lakini hakupata. Ikawa ananikosea heshima(kunitukana na kunifedhehesha) wakati mwengine mbele ya majirani na hata mbele ya marafiki zangu na zaidi ya mara tatu kunitukana mimi na marafiki zangu hata kufika baadhi yao kunieleza kuwa “baba yako anahaki ya kukufanyia haya wewe lakini sio sisi”. Nikawaomba msamaha wakanielewa. Maisha yakawa ni vituko na vitimbi visivyo simulika na kwa mwenye kujua haramu au aibu basi hawezi kufanya hata kidogo. Mimi nikaanza kupiga hatua kidogox2 katika ujenzi wangu. Nikawa napata shinikizo la kumaliza haraka nyumba yangu kutoka na vituko na kero za ajabu ajabu tokea kwa familia ya mzee. Nikaamua kuchukua deni kubwa kutoka kwa matajiri wanaouza vitu vya ujenzi na baadhi ya pesa toka kwa marafiki zangu ili kupiga hatua kubwa katika ujenzi(kuweza kumaliza 90% ya ujenzi wote sasa), huku nikianza kulipa madeni kama nilivyowaahidi wanaonidai. Baba yangu alienda na mimi kuona ujenzi nilipofikia, naamini nilifanya kosa kumuonyesha kwani nilivyoshuka livu tu nilifuatwa baba na mmoja wa wadogo zangu kwa baba. Mzee ananitaka nitoke nyumbani kwa madai ya kuwa anataka kuoza watoto wake!!!!, na amenipa miezi mitatu tu nisipotoka atatupa vifaa na familia yangu nje ya nyumba!!. Nikamueleza katika miezi mitatu uliyonipa ni mwezi tu nitawa nipo livu na miezi miwili nitakuwa kazini vipi nitadhamini(kuhakikisha) kupata nyumba ya kupanga!!, nikamuomba anipatie miezi sita badala ya mitatu na nisipopata nyumba basi nitabeba lawama mimi.
Alikataa kabisa. Siku ya pili tu akelekea polisi na wizara ya mambo ya ndani kunishtaki katika masuala mengine kabisa kuwa anataka nimpatie pesa kima chake ni kama tulivyopatanishwa na ammi yetu hapo awali kama nafaka yake toka kwangu na kudai kuwa kama siwezi basi niuze nyumba ninayojenga ili nimlishe yeye na watoto wake. Nikashanga sana na kumuuliza mbele ya mkuu wa polisi vipi niuze nyumba yangu wakati wewe yako hukuuza?, ungeanza kuuza baba ningeamini sasa huna kitu na bila shaka nami ningeuza ili nikusaidie kuendesha maisha na familia yako. Muhimu hata mkuu wa polisi amehisi baba yangu anakereka na mimi kujenga nyumba yangu. Akamuambia lazima ufurahi unapoona mwanao anajitegemea na kuweza kukusaidia na sio kukereka kwani leo kuna wazazi wengi wanaomba Allaah(SW) usiku na mchana awajaalie watoto zao waweze kujitegemea tu na sio zaidi. Nikamueleza mkuu wa polisi kuwa ninavyoona Baba yangu na familia yake wanakampeni ya kunifelisha mimi kimaisha na hata kuona nashindwa kumsaidia mama yangu na kumaliza nyumba yangu kwani anaelewa fika nina madeni kiasi hata nakosa usingizi wa raha. Hivyo amenipa muda nitoke nyumbani na nikitoka kwa kuwa nina madeni mengi na kubwa sitaweza kumpatia pesa ninazompatia sasa bali nitatumia pesa ninazompatia sasa kulipia kodi, maji na umeme mpaka nimalize ujenzi na nikihamia katika nyumba yangu bila shaka nitampatia kama awali au hata zaidi inshAllaah. Mwisho mkuu wa polisi akatusulihisha kwa kutuwekea mkataba kati yetu wa mimi kumuongezea mzee pesa kiasi kidogo na mimi nikae miezi sita kisha nikitoka nimpatie kama awali kabla ya ziada alioniomba mkuu wa polisi na mzee azuie na akikishe hakuna maudhi kero au uadui unafanyika kwangu na familia yangu(walianza kupiga mawe na kurusha michanga ndani kwangu wadogo zangu kwa baba mpaka sasa wameshafanya hivyo zaidi ya mara tatu). Siku ya pili tu baada ya mkataba wadogo zangu walimpiga mtoto wangu na kupiga mawe chumba kizima kimoja. Nikampigia simu mkuu wa polisi kumueleza hayo kisha akamuita mzee polisi na kumtaka afuate masharti ya mkataba. Nilivyokwenda kazini siku ya pili tu walipiga mawe nyumba nzima(vyumba vyote) na kumuacha mke na watoto wangu kutoka kama wendawazimu kukimbilia kwa majirani. Mke wangu akanipigia simu, nami nikamueleza mkuu wa polisi kuwa hakuna masharti yanayofuatilizwa kwa upande wa baba yangu naona ni mimi tu ninayefuatiliza masharti katika mkataba uliotuwekea. Mkuu wa polisi kwa kuwa ni heshima kwa umri wa mzee na sio tena vitendo vyake wala kauli, akanieleza nimemshindwa na mzee wako hivyo sasa unaweza kufanya unaloona wewe bora kwako na familia yako. Mimi ni mtu nisiopenda matatizo na baba na familia yake wanaishi wakipanga kufanya vitimbi vya kuniacha nishindwe kufanya yangu ama kunipotezea muda au kunizidishia ghrama zisizo za lazima. Anataka nyumba yake nitoke na pesa anataka huku akijua sintaweza kumpatia kwa jinsi nilivyo kabwa na madeni gharama na wajibu mwingi. Na mengi ninayoyabeba kichwani kwangu ni yeye sababu ya haya na mimi najaribu kuziba makosa yake kama kumtumia mama yangu matumizi ni makosa yake ya uwamuzi wa kuoa na kuacha bila sababu za msingi zinazokubalika katika uislamu mtu kumuacha mke. Kuwasaidia wadogo zangu, khale zangu kifedha, Japo leo mimi ninabeba mzigo huo wote lakini hataki kutambua hilo. Vile vile ujue kuwa tangu waje wote hakuna msaada wowote ninapata toka kwao mimi au familia yangu hata ninapokwenda kazini mwezi mzima hakuna anayewaletea familia yangu chochote toka sokoni zaidi ya jirani hata baba alilaumiwa na mkuu wa polisi kwaninini anawaacha mke na watoto wangu bila kitowewo au mboga wakati anakwenda kuwachukulia familia yake?!!!!.
Hivyo kufunga suala hili naweza kusema kuwa huyu mama wa kambo sio kuwa hanipendi mimi tu bali hapendi kuona yeyote kati ya watoto, ndugu wa baba au jamaa zake wanafaidika hali au mali ya baba, ila anachojaribu kufanya kuona kuwa watoto wake na ndugu zake tu wanaofaidika na hali na mali ya baba.
Kwani amefikia kuwafuka kwa kauli ya wazi jamaa zake baba walipokuja kukamilisha wajibu wa kuhudhuria harusi ya mmoja wa wadogo zangu wa kike(mtoto wake wa kike), ikiwa ni jambo la aibu lisilo pimika kutokana na katika mafundisho ya dini yetu na hata utamaduni wetu wa huku nadhani ni vibaya zaidi pia. LAKINI SINA LA KUSEMA WALA LA KUFANYA ZAIDI YA KUTAZAMA NA KUSHIKA TAMA HUKU NIKIJIULIZA YUKO WAPI NAHODHA(BABA) WA JAHAZI LETU!!, NA WAPI TUNAELEKEA?!!!!!!!.
Sina zaidi ya kutaka ushauri wako kwa yafuatayo:
1. Nini hukmu ya mzazi asiye hukumu sawa kati ya watoto wake na wake zake?
2. Je nini hukmu ya baba yangu kama ananidai matumizi na wakati yeye anauwezo kimali huku akiuficha na akiutumia tu bila ya kuundeleza.
3. Nini hukmu juu yangu kama nitakata matumizi (nafaka)ninayokuwa nampa ili kumaliza nyumba yangu na kisha kuendelea kumpa nikimaliza nyumba
4. Je, nini hukmu ya uadui anaoufanya baba yangu na wadogo zangu juu yangu na familia yangu?
5. Je, sina haki ya kujaribu kuendeleza maisha yangu na watoto wangu na hata kuwatengea pesa ya masomo kwa mustaqbal wa watoto wangu kimasomo ukijali ni mimi tu wanaonitegemea na sitegemei jema au msaada toka kwa wadogo zangu hawa kesho kwani dalili ya mvua ni mawingu.
6. Nini hukmu mama wa kambo na watoto zake(wadogo zangu) wanapomtumia mzee kwa maksudi kama ngao na wao wakiwa ni sababu ya matatizo yote kwa kumshiniza baba yaani wao wakicheza mbali kama sio wahusika mbele za watu lakini kwangu hawajifichi kwa hilo.
Tafadhali nilikuwa naomba nitumie jibu haraka kwani nipo katika msongamano huu bado, kupata jibu haraka kutanisaidia mimi kujua mkondo upi ni bora kuufuata kama kuna mabadiliko katika ninayotaka kufuata ili kuhitimisha kesi hii
Inna lillahi wainna ilahirajiuun
Ndugu yenu katika uislamu.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza tuwe radhi sana kuchelewa kukujibu Swali lako kwa sababu ya maswali mengi yanayomiminika humu na kutokana na upungufu wa mashekhe wetu waliokuwa wakijibu maswali kipindi cha nyuma. Hili ni jambo ambalo lilitushinda nguvu na hatukuweza kufanya lolote ila kusubiri tu. Tunatumai utafahamu hali ilivyokuwa ngumu na wingi wa kazi hizi ambazo ni wachache sana wanaozifanyia kazi. Tunatumai kuwa mpaka hivi sasa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atakuwa Amekutatulia matatizo yako na zifuatazo ni nasaha na majibu yetu.
Swala lako ni lakuhuzunisha. Ushauri wetu ni ufanye haraka kuhamia nyumba yako wewe na familia yako, hili litapunguza uhasama baina yako na babako na mamako wa kambo na ndugu zako kwa baba.
Pili uliyoyataja kumhusu babako ikiwa ndivyo, chukuwa huu kama mtihani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amekujaalia utwahirike na kupata daraja mbele Yake. Bila shaka nimajaribio makubwa lakini nadharia yako iwe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anakutihini na mzee wako (ili akutihini nani mbora kati yenu) Subira imegawanyika sampuli tatu na mojawapo ni "kusubiri katika mitihani" Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Asema (Watalipwa ujira bila ya hesabu wenye kusubiri bila ya hisabu) [Az-Zumar:10]
Majibu ya maswali yako kama ulivyoyapanga:
1. Nini hukmu ya mzazi asiye hukumu sawa kati ya watoto wake na wake zake?
Jibu:
Uadilifu ni katika dini, kuhukumu tofauti baina ya watoto ni kinyume na Sunnah.
Katika hadithi ya Nu'maan bin Bashiyr asema: "Baba yangu alinichukuwa kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akumueleza nimemzawadia mwanangu huyu mtumwa, akamuuliza Mtume "Umewapa wanao wote watumwa kama huyu" akajibu la! Mtume akamwambia mchukue mtumwa wako.[Al-Bukhaariy].
2. Je nini hukmu ya baba yangu kama ananidai matumizi ya wakati yeye anauwezo kimali huku akiuficha na akiutumia tu bila ya kuundeleza.
Jibu:
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema katika hadithi iliyopokelewa na Jabir, Umar ibnul-Khatwaab na bibi 'Aishah na wengineo: Wewe na mali yako ni (milki) ya baba yako" Na bila shaka yatikakana achukue au umpe kiasi anachohitajia kujikimu kimaisha. Lakini hukmu hii ni wakati anahitaji la sikufanya dhulma kwako au kuchukuwa mali ili kujistarehesha. Ni juu yako kumpa kwa maaruf (kulingana na haja zake asasi na uwezo wako kifedha)
3. Nini hukmu juu yangu kama nitakata matumizi (nafaka) ninayokuwa nampa ili kumaliza nyumba yangu na kisha kuendelea kumpa nikimaliza nyumba
Jibu:
Kwanza ni lazima kumuangalia kwa nafaka mzazi, wazazi wako na khasa ikiwa hawana uwezo. Hii nikatika Aliyoamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) (Wabil waalidayni ihsaana) Ukipunguza adhurike itakuwa makosa lakini akipata vya msingi (kwa maaruf) hakuna ubaya InshaAllaah. Kipimo kinaangaliwa na daraja yake ya maisha na uweza wako.
4. Je, nini hukmu ya uadui anaoufanya baba yangu na wadogo zangu juu yangu na familia yangu?
Jibu:
Bila shaka hili nijambo haramu Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akusubirishe na Awasamehe na kuwaongoza.
Lau kama hawatatubia watapata adhabu ya Allaah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuhifadhi sote.
5. Je, sina haki ya kujaribu kuendeleza maisha yangu na watoto wangu na hata kuwatengea pesa ya masomo kwa mustaqbal wa watoto wangu kimasomo ukijali ni mimi tu wanaonitegemea na sitegemei jema au msaada toka kwa wadogo zangu hawa kesho kwani dalili ya mvua ni mawingu
Jibu:
Una haqi lakini si kwa hisabu ya nafaqa au usaidizi wa baba yako kama tulivotanguliza hapo awali.
6. Nini hukmu mama wa kambo na watoto zake(wadogo zangu) wanapomtumia mzee kwa maksudi kama ngao na wao wakiwa ni sababu ya matatizo yote kwa kumshiniza baba yaani wao wakicheza mbali kama sio wahusika mbele za watu lakini kwangu hawajifichi kwa hilo.
Tafadhali nilikuwa naomba nitumie jibu haraka kwani nipo katika msongamano huu bado, kupata jibu haraka kutanisaidia mimi kujua mkondo upi ni bora kuufuata kama kuna mabadiliko katika ninayotaka kufuata ili kuhitimisha kesi hii
Jibu:
Hili ni jambo haraam, Mtume asema "dhulma ni giza siku ya Qiyaamah" Allaah atuongoze sote kwani huo ni ujaahil ambao unapelekea watu kumuasi Allaah.
Allaah Akujaze imani, subira na busara.
Na Allaah Anajua zaidi