Kisa Cha Nabiy Swaalih (عليه السلام) - 1
Kisa Cha Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam)
Sehemu Ya 1
Da’wah (Kulingania) Kaumu Ya Thamuwd:
Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) alikuwa ni Rasuli katika kabila maarufu linatokana na jina la Babu yao Thamuwd ambaye ni katika ukoo wa Nabiy Nuwh ('alayhis-salaam). Hivyo jina lake ni Swaalih ibn 'Ubayd ibn Maasiyh ibn 'Ubayd ibn Haajir ibn Thamuwd, ibn 'Aabir ibn Iram, ibn Saam, ibn Nuwh.
Naye Swaalih na watu wake wa Thamuwd ni Waarabu waliokuwa wakiishi Hijr ambayo iko baina ya Hijaaz na Tabuwk (Kaskazini Magharibi ya Madiynah) ambako siku moja Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipita wakati wanaelekea kwenda kwenya vita vya Tabuwk. (maelezo haya yatatajwa mwishoni mwa kisa hiki).
Watu wa Thamuwd walikuwa ni baada ya Nabiy Nuwh ('alayhis-salaam) waliokuwa wakiabudu masanamu na ambao waliangamizwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya kumkanusha Nabiy Nuwh ('alayhis-salaam) na da’wah yake ya kuwalingania katika Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Baada ya miaka, watu wa Thamuwd wakaibuka na kuwa na nguvu na ufakhari. Nao pia walimshirikisha Allaah ('Azza wa Jalla) kwa kuabudu masanamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akawatumia Rasuli miongoni mwao ambaye ni Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam). Na kawaida ya risala ya Rasuli ni kuwalingania washirikiana katika Tawhiyd; kumpwekesha Allaah ('Azza wa Jalla) kwa kumuabudu Yeye Pekee bila ya kumshirikisha na yeyote au chochote. Juu ya hivyo, kuwanasihi waombe maghfirah na watubie kwa Allaah ('Azza wa Jalla). Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuhusu hayo kama ifuatavyo:
وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۚ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ هُوَ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُّجِيبٌ﴿٦١﴾
61. Na kwa Thamuwd (Tulimpeleka) ndugu yao Swaalih. Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Yeye Ndiye Aliyekuanzisheni katika ardhi, na Akakufanyieni makazi humo; basi mwombeni maghfirah, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu Yuko Karibu, Mwenye kuitikia. [Huwd: 61]
Kwa maana: Amekujaalieni kuwa makhalifa baada ya watu wengine (kina 'Aad na wa nyuma yao) ili mfikiri na mtambue uovu wao waliotenda, na nyinyi msiwe kama wao, na Akakujaalieni katika hii ardhi na kukuneemesheni neema mbali mbali kama za mashamba na matunda na majumba ya fakhari mkastarehe, basi Yeye Allaah ('Azza wa Jalla) Ndiye Pekee Anayestahiki kuabudiwa bila ya kumshirikisha. Vile vile mkabilini Rabb wenu kwa kumshukuru na kufanya amali njema wala msjije kumkhalifu amri Zake mkaja kutoka nje ya mipaka kwa kutokumtii, basi rudini kwake kwa kutubia na Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Yuko tayari kupokea tawbah zenu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ قَدْ جَاءَتْكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ ۖ هَـٰذِهِ نَاقَةُ اللَّـهِ لَكُمْ آيَةً ۖ فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّـهِ ۖ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٣﴾
73. Na kwa Thamuwd (Tuliwapelekea) kaka yao Swaalih. Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Kwa yakini imekujieni hoja bayana kutoka kwa Rabb wenu. Huyu ngamia jike wa Allaah ni Aayah (ishara, dalili) kwenu. Basi muacheni ale katika ardhi ya Allaah, na wala msimguse kwa uovu isije ikakuchukueni adhabu iumizayo.
وَاذْكُرُوا إِذْ جَعَلَكُمْ خُلَفَاءَ مِن بَعْدِ عَادٍ وَبَوَّأَكُمْ فِي الْأَرْضِ تَتَّخِذُونَ مِن سُهُولِهَا قُصُورًا وَتَنْحِتُونَ الْجِبَالَ بُيُوتًا ۖ فَاذْكُرُوا آلَاءَ اللَّـهِ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿٧٤﴾
74. Na kumbukeni Alipokujaalieni warithi baada ya ‘Aad, Akakufanyieni makazi katika ardhi mnachukua katika nyanda zake tambarare majumba ya fakhari na mnachonga majumba kutokana na majabali. Basi kumbukeni neema nyingi za Allaah na wala msifanye vitendo vya hujuma katika ardhi mkifisidi. [Al-A’raaf: 73 - 74]
Lakini kama ilivyokuwa kawaida za umati za kale, kila walipotumiwa Rasuli kutoka kwa Rabb wao, wengi wao wao walikmanusha Rasuli na risala yake. Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ فَإِذَا هُمْ فَرِيقَانِ يَخْتَصِمُونَ ﴿٤٥﴾
45. Na kwa yakini Tuliwapelekea kina Thamuwd ndugu yao Swaalih kwamba: Mwabuduni Allaah. Tahamaki wakawa makundi mawili yanayokhasimiana. [An-Naml: 45]
Waliomkanusha walimtuhumu kuwa anawaletea shari, na kwamba labda akili yake haiko sawa kwani hawakumtegemea mtu kama wao ambaye ni Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) na ambaye alikuwa kwao ni mtu mwema kabisa, aje kuwakataza kuacha waliyokuja nayo mababu zao na kutaka wamfuate hayo anayotaka yeye. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
قَالُوا يَا صَالِحُ قَدْ كُنتَ فِينَا مَرْجُوًّا قَبْلَ هَـٰذَا ۖ أَتَنْهَانَا أَن نَّعْبُدَ مَا يَعْبُدُ آبَاؤُنَا وَإِنَّنَا لَفِي شَكٍّ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ مُرِيبٍ﴿٦٢﴾
62. Wakasema: Ee Swaalih! Kwa yakini ulikuwa kwetu mwenye kutarajiwa (khayr) kabla ya haya. Je, unatukataza kuabudu wale wanaowaabudu baba zetu; na hakika sisi tumo katika shaka na wasiwasi katika unayotuitia. [Huwd: 62]
Walikuwa na shaka kubwa juu ya risala aliyowalingania nayo Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) na kuona kuwa jambo geni mno. Lakini Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) akawajibu na akawanaisihi na kuwapa dalili ya muujiza waliomtaka Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) awaletee mbele ya macho yao; nao ni ngamia jike mwenye mimba na ambaye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliwatimizia ombi lao hilo:
قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِن كُنتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَآتَانِي مِنْهُ رَحْمَةً فَمَن يَنصُرُنِي مِنَ اللَّـهِ إِنْ عَصَيْتُهُ ۖ فَمَا تَزِيدُونَنِي غَيْرَ تَخْسِيرٍ﴿٦٣﴾
63. (Swaalih) Akasema: Enyi kaumu yangu! Je, mnaonaje ikiwa niko katika hoja bayana kutoka kwa Rabb wangu, na Amenipa rahmah (Unabiy na risala) kutoka Kwake basi nani atakayeninusuru nikimuasi? Basi hamnizidishii ila khasara.
وَيَا قَوْمِ هَـٰذِهِ نَاقَةُ اللَّـهِ لَكُمْ آيَةً فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّـهِ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ قَرِيبٌ﴿٦٤﴾
64. Enyi kaumu yangu! Huyu ni ngamia jike wa Allaah, ni Aayah (miujiza, ishara) kwenu, basi mwacheni ale katika ardhi ya Allaah, na wala msimguse kwa uovu ikakupateni adhabu iliyo karibu.
Lakini hawakuwa wenye kutakwa kuongoka. Bali walizidi kumtuhumu Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) wakimwambia kuwa amerogwa!
قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ ﴿١٥٣﴾
153. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa. [Ashu’araa: 153]
Mujaahid kasema; Wamemaanisha kuwa kaathirika na uchawi.
Baadhi ya wafasiri wa Qur-aan wamesema wamekusudia kuwa Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) hakuwa anajua anachokisema kuwalingania katika ‘ibaada ya Mwabudiwa Mmoja (Laa ilaaha illa-Allaah) na badala yake kuacha waabudiwa wao waliokuwa wakiabudiwa na mababu zao.
Ilikuwa ni kawaida ya watu wa umati za nyuma kuwatilia shaka na kuwatuhumu Manabii kuwa ni wachawi au wamerogwa au waongo,. Hata Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituhumiwa na makafiri wa ki-Quraysh. Na pia waliwatilia shaka kwa kuwa wao ni wana Aadam kama wao; walitegemea watumiwe Malaika badala yake. Basi Kauli ya Thamuwd nao wakamwambia Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam):
مَا أَنتَ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا فَأْتِ بِآيَةٍ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿١٥٤﴾
154. Wewe si chochote isipokuwa mtu kama sisi; basi lete Aayah (dalili, muujiza) ukiwa wewe ni miongoni mwa wakweli. [Ash-Shu’araa: 154]
Na pia Kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
كَذَّبَتْ ثَمُودُ بِالنُّذُرِ ﴿٢٣﴾
23. Kina Thamuwd waliwakadhibisha Waonyaji.
فَقَالُوا أَبَشَرًا مِّنَّا وَاحِدًا نَّتَّبِعُهُ إِنَّا إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ ﴿٢٤﴾
24. Wakasema: Ah! Tumfuate binaadamu miongoni mwetu? Hakika hapo sisi tutakuwa katika upotofu na wazimu.
أَأُلْقِيَ الذِّكْرُ عَلَيْهِ مِن بَيْنِنَا بَلْ هُوَ كَذَّابٌ أَشِرٌ ﴿٢٥﴾
25. Ah! Ameteremshiwa ukumbusho baina yetu? Bali yeye ni muongo mkubwa mfidhuli mwenye kutakabari mno.
سَيَعْلَمُونَ غَدًا مَّنِ الْكَذَّابُ الْأَشِرُ ﴿٢٦﴾
26. Watakuja kujua kesho nani muongo mkubwa mfidhuli mwenye kutakabari mno. [Al-Qamar: 23- 26]
Wakadai muujiza uwatokezee mbele ya macho yao, na hata walipotimiziwa ombi lao hawakumwamini Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam). Basi Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) akajitenga nao kwa kuwa alikata tamaa nao kuwa wataitikia risala ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَةَ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُحِبُّونَ النَّاصِحِينَ ﴿٧٩﴾
79. (Swaalih) akajitenga nao na akasema: Enyi kaumu yangu! Kwa yakini nilishakubalighishieni risala ya Rabb wangu na nilikunasihini, lakini nyinyi hamuwapendi wenye kunasihi. [Al-A’raaf: 79]
…./2