Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) - 4
Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (‘Alayhi-Salaam) – 4
Kujenga Al-Ka’bah:
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamuamrisha Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ajenge Al-Ka'bah. Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) wakapandisha msingi wa nyumba (yaani Ka'bah). Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) akawa analeta mawe huku Ibraahiym (‘alayhis-salaam) anajenga. Kuta za nyumba ziliponyanyuka juu, Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) alileta jiwe na kumpa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ili asimamie kuendelea kujenga huku Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) anamletea mawe.
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alikuwa akisimama juu ya jiwe hilo, na kila alipomaliza kujenga upande mmoja, alisogea upande mwingine kumalizia kujenga Ka’bah.
Jiwe hilo liliweka alama ya miguu yake Ibraahiym (‘alayhis-salaam). Alipomaliza kujenga, aliliweka jiwe karibu na ukuta wa Ka’bah na hapo ndipo mahali lilipokuwa miaka yote hiyo hadi ilipofika zama za ukhalifa wa 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye alilisogeza kutoka kuta za Ka’bah. 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni mmoja wa wawili ambao Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salaam) amesema:
اقتدوا باللَّذَين من بعدي أبي بكر وعمر
“Wafuateni watakaokuwa baada yangu, Abu Bakar na 'Umar” [Tuhfat Al-Ahwadhiy: 569]
Na hapo ndipo mahali panapoitwa Maqaam Ibraahiym (Kisimamo cha Ibraahiym) ambako mwenye kufanya Hajj au 'Umrah, anapaswa kuswali Raka'ah mbili baada ya kufanya twawaaf.
Na amri ya kuswali Raka'ah mbili ilikuwa ni kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ أَنَسٍ، قَالَ قَالَ عُمَرُ: وَافَقْتُ رَبِّي فِي ثَلاَثٍ، فَقُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ لَوِ اتَّخَذْنَا مِنْ مَقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى فَنَزَلَتْ: ((وَاتَّخِذُوا مِنْ مَقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى)) وَآيَةُ الْحِجَابِ، قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ، لَوْ أَمَرْتَ نِسَاءَكَ أَنْ يَحْتَجِبْنَ، فَإِنَّهُ يُكَلِّمُهُنَّ الْبَرُّ وَالْفَاجِرُ. فَنَزَلَتْ آيَةُ الْحِجَابِ، وَاجْتَمَعَ نِسَاءُ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فِي الْغَيْرَةِ عَلَيْهِ فَقُلْتُ لَهُنَّ عَسَى رَبُّهُ إِنْ طَلَّقَكُنَّ أَنْ يُبَدِّلَهُ أَزْوَاجًا خَيْرًا مِنْكُنَّ. فَنَزَلَتْ هَذِهِ الآيَةُ
Kutoka kwa ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Rabb Wangu Ameniwafikia mambo matatu: Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Lau tungefanya sehemu aliyosimamia Ibraahiym kuwa sehemu ya kuswali. Ikateremka:
.. وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى ۖ ...﴿١٢٥﴾
“na fanyeni mahali pa kusimama Ibraahiym kuwa ni pahala pa kuswalia.” (2: 125) Na Aayah ya hijaab nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Ungewaamrisha wake zako kujiwekea hijaab (kizuizi) kutokana na wanaume kwa sababu watu wema na waovu wanaongea nao. Basi ikateremka Aayah ya hijaab kwa wanawake. Na wakeze Nabiy walijiunga dhidi ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na wivu wao baina yao. Nikawaambia: Huenda akutalikini kisha Rabb wake Ambadilishie wake walio bora zaidi kuliko nyinyi” ikateremka Aayah (At-Tahriym 5) [Al-Bukhaariy]
Utukufu Wa Ka’bah:
a-Mahali Pa Salama Na Amani:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuhusu utukufu wa Ka’bah:
وَإِذْ جَعَلْنَا الْبَيْتَ مَثَابَةً لِّلنَّاسِ وَأَمْنًا وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى ۖ وَعَهِدْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ ﴿١٢٥﴾
Na Tulipoifanya Nyumba (Al-Ka’bah) kuwa ni mahali pa kurejewa na watu na pa amani, na fanyeni mahali pa kusimama Ibraahiym kuwa ni pahala pa kuswalia. Na Tulichukua ahadi kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl kwamba: Itakaseni Nyumba Yangu kwa wanaotufu na wanaokaa i’tikaaf, na wanaorukuu na kusujudu. [Al-Baqarah:125].
Mahali pa amani: Yaani: amani kutokana na maadui. Na ikaendelea Ka’bah kuwa mahali patukufu na amani tokea zama hizo na itaendelea mpaka Siku ya Qiyaamah. Hata zama za ujaahiliyyah watu mara nyingi walikuwa ni waathirika wa uvamizi na watekwa nyara, ila waliokuwa katika eneo la Ka’bah (Al-Masjidul-Haraam) ndio walikuwa katika usalama wa kutekwa nyara. [At-Twabariy 3:29]
Vile vile Mujaahid, 'Atwaa' As-Suddiy, Qataadah na Ar-Rabi' bin Anas wameripotiwa wakisema kwamba: Aayah hiyo ina maana: "Yeyote atakayeingia humo atakuwa salama". [Ibn-Abi Haatim 1:370].
Aayah hii ina inaonyesha kwamba, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameitukuza nyumba hii tukufu ambayo Ameifanya iwe kimbilio na bandari ya salama. Kwa hiyo nafsi za watu huwa zina hamu kubwa ya kuweko hapo, na hawachoshwi kutembelea kila mara au kila mwaka. Hii ni kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliikubali Duaa ya Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alipomuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Ajaaliye nyoyo za watu zipende kuelekea huko, wakati alipomuacha mkewe Haajar na mwanawe Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) mwanzo kabisa pindi alipofika hapo. [Al-Bukhaariy 3364]
Aliomba:
رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿٣٧﴾
Rabb wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuria wangu katika bonde lisilokuwa na mmea wowote, kwenye Nyumba Yako Tukufu. Rabb wetu, ili wasimamishe Swalaah na Ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao na Uwaruzuku mazao ili wapate kushukuru. [Ibraahiym :37]
b-Mahali Patukufu Pa Kuswaliwa:
Heshima ya mwanzo inamfikia Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kwa kufanywa sehemu aliyosimama kujenga Ka’bah kuwa mahali patukufu pa kuswaliwa.
.. وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى ۖ ...﴿١٢٥﴾
Na fanyeni mahali pa kusimama Ibraahiym kuwa ni pahala pa kuswalia. [Al-Baqarah:125]
c-Nyumba Iliyotakaswa:
Vile vile ilikuwa ni amri kwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na mwanawe Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) kwamba waitakase Ka’bah.
ۖ وَعَهِدْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ ﴿١٢٥﴾
Na Tulichukua ahadi kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl kwamba: Itakaseni Nyumba Yangu kwa wanaotufu na wanaokaa i’tikaaf, na wanaorukuu na kusujudu [Al-Baqarah:125]
Hali kadhalika ilikuwa ni amri ya kuitakasa na shirki:
وَإِذْ بَوَّأْنَا لِإِبْرَاهِيمَ مَكَانَ الْبَيْتِ أَن لَّا تُشْرِكْ بِي شَيْئًا وَطَهِّرْ بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْقَائِمِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ ﴿٢٦﴾
Na (taja) Tulipomwonyesha Ibraahiym mahali pa Nyumba; Al-Ka’bah, (Tukamwambia): Usinishirikishe na chochote; na twaharisha Nyumba Yangu kwa wafanyao Twawaaf, na wanaosimama kuswali na wanaorukuu na kusujudu. [Al-Hajj:26]
Maana: Ifanye iwe safi kwa wale wanaomuabudu Allaah Pekee bila ya kumshikirikisha na mtu au msaidizi.
d-Nyumba Ya Pekee Inayozungukwa Kama Ibaada:
Ni nyumba pekee katika ulimwengu wa Waislamu inayozungukwa, kuwa ni ibaada. Twawaaf na Swalaah zimetajwa pamoja katika Aayah hiyo, kwa sababu hakuna mahali popote kwengine kulikofaradhishwa ibaada hizi mbili kwa pamoja, isipokuwa hapa katika Ka’bah.
e-Ni Msikiti Wa Mwanzo Ulimwenguni Na Ni Msikiti Wenye Baraka Na Mwongozo:
Nayo ni nyumba ya mwanzo kabisa duniani iliyofanywa kuwa ya ibaada, yenye baraka, uongofu kwa watu wote, na ndipo Waislamu huenda kutekeleza Hajj:
إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ ﴿٩٦﴾
Hakika nyumba ya awali iliyowekwa kwa ajili ya watu (kufanya ibaada) ni ile ambayo iko Bakkah (Makkah), yenye barakah na mwongozo kwa walimwengu. [Aal-‘Imraan:96]
عن أبي ذَر، رضي الله عنه، قال قلتُ: يا رسولَ الله، أيُّ مَسجِد وُضِع في الأرض أوَّلُ؟ قال: الْمسْجِدُ الْحَرَام .قلت: ثم أَيُّ؟ قال: الْمسجِدُ الأقْصَى. قلت: كم بينهما؟ قال: أرْبَعُونَ سَنَةً .قلتُ: ثم أَيُّ؟ قال: ثُم حَيْثُ أدْرَكْت الصَلاةَ فَصَلِّ، فَكُلُّهَا مَسْجِدٌ. أخرجه البخاري، ومسلم، وأحمد
Imetoka kwa Abu Dharr amesema: "Nilisema Ee Rasuli wa Allaah! Ni Msikiti gani ulikuwa wa mwanzo kabisa kujengwa duniani?" Akasema: ((Al-Masjidul-Haraam)) (Ulioko Makkah). Nikasema: Kisha upi? Akasema: ((Al-Masjidul-Aqswaa)) (Palestina). Nikasema: Ilikuwa muda gani kujengwa baina yao? Akasema: ((Miaka arubaini)) Akaongeza: ((Popote (mtakapokuwa) na Swalaah ikawakuta, Swalini humo, kwani ardhi yote imefanywa kuwa ni mahali pa kusujudu)) [Al-Bukhaariy, Muslim na Imaam Ahmad]
Usemi mwingine kutoka kwa wataalamu wanaofasiri, wamesema kuwa kwa vile Adam (‘alayhis-salaam) ni kiumbe cha mwanzo katika ardhi, alipewa heshima kujenga nyumba ya mwanzo ya ibaada. Aliijenga kisha akaizunguka kama Malaika wanvyozunguka juu katika Baytul-Ma'amuur huko juu katika 'Arshi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) iliyoko katika mbingu ya saba. Na inasemekana alijenga hema akawa anafanya ibaada yake hapo, lakini baada ya kufariki na karne nyingi kupia, ikapotea alama ya sehemu hiyo.
f-Nguzo Ya Tano Ya Kiislamu Inatimizwa Hapo:
فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ ۖ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا ۗ وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٩٧﴾
Ndani yake kuna Aayaat (Ishara, Dalili) zilizo wazi; mahali pa kisimamo cha Ibraahiym. Na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu. [Al-'Imraan: 97]
Du’aa Za Ibraahiym ‘Alayhis -Salaam Baada Ya Kujenga Ka’bah:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿١٢٧﴾
Na aliponyanyua Ibraahiym na Ismaa’iyl msingi wa Nyumba (Al-Ka’bah): Rabb wetu, Tutakabalie, hakika Wewe ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah:127]
Hapa tunapata fundisho kubwa kutoka kwa baba yetu Nabiy Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kwamba ingawa yeye na Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) wamejenga Ka’bah, ambayo inayozungukwa na Waislamu kama ni ibaada tukufu, lakini hawakutegemea kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atawapokelea amali hii moja kwa moja, bali walimuomba Allaah Awatakabalie. Hivi ni katika sifa za Waumini kuwa baina ya khofu na matumaini wanapotekeleza amali njema. Na sisi tunatakiwa tuwe tunaiomba Duaa hii kila mara tunapomaliza matendo mema, kwani nasi hatujui kama matendo yetu yatakubaliwa na Allaah.
Akaendelea Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kuomba pamoja na mwanawe Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam)
رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿١٢٨﴾
Rabb wetu, Tujaalie tuwe wenye kujisalimisha Kwako pamoja na kizazi chetu wawe ummah wenye kujisalimisha Kwako na Tuonyeshe taratibu za ibaada zetu na Pokea tawbah zetu, hakika Wewe ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al-Baqarah: 128]
.. وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا .. ﴿١٢٨﴾
na Tuonyeshe taratibu za ibaada zetu
Ina maana ni Taratibu za Hajj na 'Umrah ambazo Waislamu wanazifuata kutekelea nguzo hii ya Kiislamu.
رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١٢٩﴾
Rabb wetu, wapelekee Rasuli miongoni mwao atakayewasomea Aayaat Zako na atakayewafunza Kitabu na Hikmah na atakayewatakasa. Hakika Wewe ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Baqarah:129]
Duaa hii: ((Waletee Rasuli anayetokana na wao)), ndio sababu ya kutoka Nabiy wa mwisho kutoka kizazi cha Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam), ambaye ni Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salaam).
Vile vile maana ya ((awasomee Aayah Zako, na awafundishe Kitabu na hikma)), ni Kitabu cha mwisho kuteremshwa kutoka mbinguni; Qur-aan aliyoteremshiwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa salaam) kwa ajili ya walimwengu wote.
Duaa nyingine alizoomba Ibraahiym (‘alayhis-salaam):
وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَـٰذَا الْبَلَدَ آمِنًا وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ ﴿٣٥﴾ رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ ۖ فَمَن تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي ۖ وَمَنْ عَصَانِي فَإِنَّكَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣٦﴾ رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿٣٧﴾ رَبَّنَا إِنَّكَ تَعْلَمُ مَا نُخْفِي وَمَا نُعْلِنُ ۗ وَمَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِن شَيْءٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ ﴿٣٨﴾الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي وَهَبَ لِي عَلَى الْكِبَرِ إِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ ۚ إِنَّ رَبِّي لَسَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٩﴾رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلَاةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي ۚ رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاءِ﴿٤٠﴾رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿٤١﴾
35. Na pindi Ibraahiym aliposema: Ee Rabb wangu! Ujaalie mji huu (Makkah) uwe wa amani; na Uniepushe na wanangu kuabudu masanamu. Rabb wangu! Hakika hao (masanamu) wamepoteza wengi kati ya watu. Basi atakayenifuata, huyo ni katika mimi, na atakayeniasi, basi hakika Wewe ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. Rabb wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuria wangu katika bonde lisilokuwa na mmea wowote, kwenye Nyumba Yako Tukufu. Rabb wetu, ili wasimamishe Swalaah na Ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao na Uwaruzuku mazao ili wapate kushukuru. Rabb wetu! Hakika Wewe Unajua tunayoyaficha na tunayoyadhihirisha. Na hakifichiki kitu chochote kwa Allaah katika ardhi wala katika mbingu. AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Amenitunukia juu ya umri mkubwa wangu Ismaa’iyl na Is-haaq. Hakika Rabb wangu bila shaka ni Mwenye kusikia duaa yangu. Rabb wangu! Nijaalie niwe mwenye kusimamisha Swalaah na dhuria wangu. Rabb wetu! Nitakabalie duaa yangu. Rabb wetu! Nighufurie na wazazi wangu wawili na Waumini Siku itakayosimama hesabu. [Ibraahiym: 35-41]
Kuwaadhinia Watu Waitikie Kwenda Hajj:
Alipomaliza Nabiy Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kujenga Ka’bah, Allaah Alimtaka awatangazie watu wafike Makkah kuhiji:
وَأَذِّن فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالًا وَعَلَىٰ كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِن كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ ﴿٢٧﴾
Na tangaza kwa watu Hajj; watakufikia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, watakuja kutoka katika kila njia pana za milima zilioko mbali kabisa. [Al-Hajj:27]
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alisema: "Rabb wangu, vipi niwatangazie watu hivyo na hali sauti yangu haitawafikia?" Akaambiwa: "Waite (waadhinie) na Sisi Tutawafikishia". Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akasimama na kusema: "Enyi watu! Rabb wenu Ameanzisha Nyumba ili mje kuhiji".
Imesemekana kuwa milima ilijiinamisha ili sauti ifikie pande zote za dunia, na ikawafikia watu wote mpaka waliokuwa matumboni mwa mama zao na migongo ya baba zao (yaani waliokuwa bado hawakuzaliwa).
Majibu yakawa ni:
"لبيك اللهم لبيك"
"Labbayka Allaahumma Labbayk"
Nimekuitika Ee Allaah nimekuitika,
Na hao ni ambao wamejaaliwa kutekeleza Hajj. Na kauli hiyo anaitamka mwenye kufanya Hajj au Umrah anapoingia katika Ihraam.
Kuondoka Makkah Baada Ya Kujenga Ka’bah:
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akaondoka na mkewa Sarah kurudi Palestina. Lakini alumuacha Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) pamoja na familia yake Makkah.
Siku moja, Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alikuwa amekaa katika kambi yake akimfikiria mwanawe Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) kuhusu ndoto ya kumchinja na fidia Aliyomteremshia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Moyo wake ukazidi kujaa mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa neema Zake zisizohesabika. Chozi kubwa likamdondoka alivyokuwa akimfikiria Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) na umbali alioko, jinsi alivyokuwa akimkosa na hamu ya kuwa naye.
Mara Malaika watatu wakateremka; Jibriyl, Israafiyl na Miykaaiyl. Walimjia kwa maumbo ya binaadamu wenye sura nzuri kabisa. Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliinuka na kuwakaribisha. Aliwaita ndani ya kambi huku akiwaza kuwa ni wageni asiowajua. Akawakaribisha vizuri na kuhakikisha kuwa wamestarehe, kisha akaomba idhini kwao ili aende kwa ahli yake. (kuagiza waletewe chakula).
Sarah wakati huo ameshakuwa mzee, mvi zimemjaa kichwani. Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akamuambia: "Tumepata wageni watatu".
Akamuuliza: "Ni nani hao?" Akamjibu: "Simjui hata mmoja wao". Akauliza Ibraahiym (‘alayhis-salaam): "Tuna chakula gani?". Akajibu Sarah: "Tuna nusu kondoo". Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akasema: "Nusu kondoo? Wachinjie nusu ndama, kwani wao ni wageni tusiowajua na hatujui pengine wana njaa".
Watumishi wakachinja nusu ndama na kumchoma vizuri. Kikaletwa chakula mbele ya hao wageni, Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akawakaribisha wasogee kula. Akaona hawasogei kula, basi akaanza kula yeye ili awatie moyo nao watake kula lakini aliona kuwa hakuna hata mmoja wao aliyegusa chakula. Akawauliza: "Kwa nini hamli?". Akaendelea yeye kula, lakini wao walibakia vile vile bila ya kukaribisha mikono yao katika chakula. Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akaanza kuogopa.
Khofu ya Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ikazidi na Malaika wakawa wanamsoma mawazo yake, kisha mmoja wao akasema: "Usikhofu". Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akasema: "Hakika nina khofu, kwani nimekukaribisheni mle lakini naona hamjanyoosha mikono yenu kutaka kula. Je, mmekusudia uovu?"
Malaika mmoja akatabasamu na kusema: "Sisi hatuli, kwani sisi ni Malaika wa Allaah". Mmoja wao akageuka kwa mkewe Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na kumbashiria bishara njema ya mwana Is-haaq.
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na Sarah walishtuka kubashiriwa mtoto katika umri huo walionao. Lakini juu ya mshtuko huo, Sarah aliingiwa na furaha kubwa kuwa atapata mtoto ambaye alimtamani miaka mingi sana! Na furaha ilizidi alipoambiwa kuwa mtoto huyo atakuwa ni mtoto mwenye ujuzi.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuelezea matukio haya kwa kirefu katika Aayah zifuatazo:
وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ﴿٥١﴾إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا قَالَ إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ﴿٥٢﴾قَالُوا لَا تَوْجَلْ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ﴿٥٣﴾ قَالَ أَبَشَّرْتُمُونِي عَلَىٰ أَن مَّسَّنِيَ الْكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ﴿٥٤﴾قَالُوا بَشَّرْنَاكَ بِالْحَقِّ فَلَا تَكُن مِّنَ الْقَانِطِينَ﴿٥٥﴾قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ﴿٥٦﴾قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ﴿٥٧﴾قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ﴿٥٨﴾إِلَّا آلَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٥٩﴾إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَا ۙ إِنَّهَا لَمِنَ الْغَابِرِينَ﴿٦٠﴾
Na wajulishe kuhusu wageni wa Ibraahiym. Pale walipoingia kwake, wakasema: Salaama! (Ibraahiym) Akasema: Hakika sisi tunakuogopeni. (Malaika) Wakasema: Usiogope! Hakika sisi tunakubashiria ghulamu mjuzi. (Ibraahiym) Akasema: Je, mnanibashiria (mwana) na hali uzee umeshanishika, basi kwa njia gani mnanibashiria? Wakasema: Tunakubashiria kwa haki, basi usiwe miongoni mwa wakatao tamaa. Akasema: Na nani anayekata tamaa na rahmah ya Rabb wake isipokuwa wapotofu. Akasema: Basi nini jambo lenu muhimu enyi Wajumbe. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakhalifu. Isipokuwa familia ya Luutw, hakika Sisi Tutawaokoa wote. Isipokuwa mkewe Tumehukumu kwamba yeye bila shaka ni miongoni mwa watakaobakia nyuma (kuangamizwa). [Al-Hijr: 51-60]
Waliposema kuwa wanakwenda kuangamiza mji wa Luutw (‘alayhis-salaam) Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alikhofu kuwa vipi wataangamiza mji huo na hali yumo Luutw (‘alayhis-salaam)? Majibu yao Malaika yamo katika aayah zifuatazo:
وَلَمَّا جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَىٰ قَالُوا إِنَّا مُهْلِكُو أَهْلِ هَـٰذِهِ الْقَرْيَةِ ۖ إِنَّ أَهْلَهَا كَانُوا ظَالِمِينَ ﴿٣١﴾ قَالَ إِنَّ فِيهَا لُوطًا ۚ قَالُوا نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَن فِيهَا ۖ لَنُنَجِّيَنَّهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٣٢﴾
Na Wajumbe Wetu walipomjia Ibraahiym kwa bishara walisema: Hakika sisi tutawahiliki watu wa mji huu. Hakika watu wake wamekuwa madhalimu. (Ibraahiym) Akasema: Hakika humo yumo Luutw. (Malaika) Wakasema: Sisi tunajua zaidi waliokuwemo humo; tutamuokoa na ahli zake isipokuwa mke wake amekuwa miongoni mwa watakaobakia nyuma. [Al-'Ankabuwt: 31-32]
هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ﴿٢٤﴾إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا ۖ قَالَ سَلَامٌ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ﴿٢٥﴾فَرَاغَ إِلَىٰ أَهْلِهِ فَجَاءَ بِعِجْلٍ سَمِينٍ﴿٢٦﴾فَقَرَّبَهُ إِلَيْهِمْ قَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ﴿٢٧﴾فَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً ۖ قَالُوا لَا تَخَفْ ۖ وَبَشَّرُوهُ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ﴿٢٨﴾فَأَقْبَلَتِ امْرَأَتُهُ فِي صَرَّةٍ فَصَكَّتْ وَجْهَهَا وَقَالَتْ عَجُوزٌ عَقِيمٌ﴿٢٩﴾قَالُوا كَذَٰلِكِ قَالَ رَبُّكِ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ﴿٣٠﴾قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿٣١﴾قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿٣٢﴾لِنُرْسِلَ عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن طِينٍ ﴿٣٣﴾مُّسَوَّمَةً عِندَ رَبِّكَ لِلْمُسْرِفِينَ ﴿٣٤﴾
Je, imekufikia hadithi ya wageni wahishimiwao wa Ibraahiym? Walipoingia kwake wakasema: Salaam! Akasema: Salaam watu wasiotambulikana. Akaondoka bila kuhisiwa kuelekea kwa ahli yake akaleta ndama aliyenona. Akawakurubishia; akasema: Mbona hamli? Akawaogopa ndani ya nafsi yake. Wakasema: Usikhofu! na wakambashiria ghulamu mjuzi. Mkewe akawakabili kwa hoihoi na vifujo (kushtuka), akijipiga usoni na akasema: Kikongwe, tasa! Wakasema: Hivyo ndivyo Alivyosema Rabb wako, hakika Yeye Ndiye Mwenye hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. (Ibraahiym) Akasema: Basi nini shughuli yenu mloikusudia enyi Wajumbe? Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wahalifu. Ili Tuwapelekee mawe ya udongo. Yaliyotiwa alama kutoka kwa Rabb wako kwa wapindukao mipaka. [Adh-Dhaariyaat: 24-34]
Malaika hao walikuwa wanakwenda katika mji wa Nabiy Luutw (‘alayhis-salaam) kuwaangamiza watu wake ambao walikuwa katika maasi.
Baada ya hapo, na kutokana na kubashiriwa mtoto, Sarah akashika mimba na akamzaa Is-haaq (‘alayhis-salaam).
Naye Is-haaq (‘alayhis-salaam) akamzaa Ya'aquwb (‘alayhis-salaam) ambaye amemzaa Yuwsuf (‘alayhis-salaam) pamoja na ndugu zake wengine kumi na mojo. Mmoja wa ndugu yake Yuwsuf (‘alayhis-salaam) akiitwa Binyaamiyn ndiye aliyekuwa ni ndugu yake khalisa (ndugu kwa baba na mama).
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) amefariki katika umri wa miaka mia na sabini na tano. [Qwisasul-Anbiyaa- Ibn Kathiyr] na amezikwa Falastina katika mji ulioitwa Khaliyl.
Na Allaah Anajua zaidi.
Mwisho wa Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam)
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatujulisha kuhusu visa vya Manabii kwamba:
قَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَىٰ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿١١١﴾
Kwa yakini katika visa vyao kuna mazingatio (na mafunzo) kwa wenye akili. Haikuwa (Qur-aan) hadithi zinazotungwa, lakini ni sadikisho la (Vitabu) vya kabla yake na tafsili ya waziwazi ya kila kitu, na ni mwongozo na rehma kwa watu wanaoamini. [Yuwsuf (12:111)]