Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) - 3
Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) - 3
Kuhama Iraq:
وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ ﴿٧١﴾
Na Tukamuokoa na Luutw kuelekea ardhi ambayo Tumeibariki humo kwa walimwengu. [Al-Anbiyaa:71]
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliondoka Iraq pamoja na Luutw (‘alayhis-salaam) na wakaelekea kwanza katika mji unaoitwa 'Aur, kisha Haraan, kisha tena Falastina (Palestine).
Alivyompata Haajar (Mama wa Nabiy Ismaa’iyl (‘alayhis-salaam):
Akaelekea Misri na wakati wote alipokuwa safarini ilikuwa hima yake ni kuwaita watu katika Tawhiyd, kuwaongoza katika haki na katika mambo mema. Alipokuwa anaelekea Misri alipita mji wa dhalimu mmoja, akapiga kambi hapo. Matukio yote hapo yameelezwa katika Hadiyth ifuatayo:
عن أبي هريرة رضي الله عنه؛ أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((إن إبراهيم، عليه السلام، لم يكذب غير ثلاث: ثنتين في ذات الله ، قوله: ( بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَذَا ) وقوله (إِنِّي سَقِيمٌ ) قال: "وبينا هو يسير في أرض جبار من الجبابرة ومعه سارة، إذ نـزل منـزلا فأتى الجبار رجل، فقال: إنه قد نـزل بأرضك رجل معه امرأة أحسن الناس، فأرسل إليه فجاء، فقال: ما هذه المرأة منك؟ قال: هي أختي. قال: فاذهب فأرسل بها إليّ، فانطلق إلى سارة فقال: إن هذا الجبار سألني عنك فأخبرته أنك أختي فلا تكذبيني عنده، فإنك أختي في كتاب الله، وأنه ليس في الأرض مسلم غيري وغيرك، فانطلق بها إبراهيم ثم قام يصلي. فلما أن دخلت عليه فرآها أهوى إليها، فتناولها، فأخذ أخذًا شديدًا، فقال: ادعي الله لي ولا أضرك، فدعت له فأرسل، فأهوى إليها، فتناولها فأخذ بمثلها أو أشد. ففعل ذلك الثالثة فأخذ، [فذكر] مثل المرتين الأوليين فقال ادعي الله فلا أضرك. فدعت، له فأرسل، ثم دعا أدنى حجابه، فقال: إنك لم تأتني بإنسان، وإنما أتيتني بشيطان، أخرجها وأعطها هاجر، فأخرجت وأعطيت هاجر، فأقبلت، فلما أحس إبراهيم بمجيئها انفتل من صلاته، قال: مَهْيَم؟ قالت: كفى الله كيد الكافر الفاجر، وأخدمني هاجر)
قال محمد بن سيرين وكان: أبو هريرة إذا حدث بهذا الحديث قال: فتلك أمكم يا بني ماء السماء
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya-Allaahu ‘anhu): Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “ Ibraahiym (‘alayhis-salaam) hakuongopa ila mara tatu tu; mara mbili kwa ajili ya Allaah aliposema:
( بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَذَا )
((Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao))
na aliposema:
(إِنِّي سَقِيمٌ )
((Hakika mimi ni mgonjwa!)). Na alipokuwa akisafiri katika mji wa dhalimu mmoja na (mkewe) Sarah alikuwa naye. Alipopiga kambi, mtu mmoja alikwenda kwa dhalimu na kumwambia, "Kuna mtu amepiga kambi katika ardhi yako na anaye mwanamke mzuri kupita wote". Dhalimu akamuita Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kwake, na akamuuliza, "Nini uhusiano wa mwanamke huyu na wewe?". Akasema, "Yeye ni dada yangu". Dhalimu akasema, "Nenda kamlete kwangu". Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akaenda kwa Sarah na akasema, "Dhalimu huyu ameniuliza kuhusu wewe, na nimemwambia kwamba wewe ni dada yangu, kwa hiyo usimfanye akajua kwamba nimeongopa, kwani hakika ni dada yangu kufuatana na kitabu cha Allaah, na hakuna Waislamu katika ardhi hii ila mimi na wewe". Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akampeleka (Sarah) kwake, kisha akasimama na kuswali. Alipoingia kwa dhalimu na (dhalimu) alipomuona (Sarah), akataka kumshika kwa matamanio, lakini akagandishiwa (mkono) Akasema, "Niombee kwa Allaah na sitokudhuru". Sarah akamuombea, na akaachiliwa. Kisha akamfikia kwa matamanio, lakini akapatwa tena (kuganda mkono) kama mwanzo au zaidi. Ikaendelea hivyo mara tatu, na kila mara alisema kama alivyosema mara ya mwanzo. Kisha akamwita mlinzi wake wa karibu naye kabisa na akasema, "Hukuniletea binaadamu bali umenilitea shaytwaan! Muondoshe na mpe Haajar". Akaondoshwa (Sarah) na kupewa Haajar, akarudi. Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alipotambua kuwa (Sarah) amerudi, alimaliza kuswali na kugeuka akasema, "Imekuwaje?". Akasema, "Allaah Ametosheleza njama za kafiri dhalimu, na amenipa Haajar kama mtumwa")) [Al-Bukhaariy na Muslim].
Muhammad bin Siriyn amesema, "Abu Huraryah amesimulia Hadiyth hii akasema: "Huyu ni mama yenu enyi wana wa maji ya mbinguni" (yaani Waarabu kizazi cha Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam), mwana wa Haajar ambaye ndiye aliyesababisha maji ya Zamzam). [Fat-h Al-Baariy 6:447, Muslim 4:1840]
Mke wa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) Sarah, alikuwa tasa. Na Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alikuwa anazeeka na nywele zake zikatawaliwa na mvi baada ya kuita watu miaka mingi katika dini ya Allaah. Sarah akafikiria kwamba yeye na Ibraahiym (‘alayhis-salaam) wako katika upweke kwa vile hawakupata mtoto. Kwa hiyo akampa mumewe mtumwa wake Haajar amuoe. Haajar akamzaa Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) ambaye ndiye mtoto wa mwanzo wa Ibraahiym (‘alayhis-salaam).
Siku zikapita na Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akawa na furaha ya kupata mtoto, lakini Sarah akawa na wivu sasa na Haajar, ingawa yeye mwenyewe ndiye aliyempa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) Haajar amuoe. Wivu huo ukamfanya Haajar awe anajificha ili Sarah asimuone anapokwenda kwa mumewe. Akawa ni mwanamke wa kwanza kufunga mkanda kuficha alama zake kama ilivyotajwa katika Hadiyth ndefu kutoka kwa Al-Bukhaariy iliyopokelewa na Ibn 'Abbaas kwamba "Haajar ni mwanamke wa mwanzo kutumia mkanda".
Makusudio hapo ni mkanda kiunoni kuzuia nguo yake ndefu inayoburuza ardhini isiache alama apitapo (ikaja ikajulikana na Sarah kuwa kapita). Inasemekana kuwa wakati huo wanawake walikuwa wakivaa nguo ndefu zinazoburuza. Na hii inaonyesha jinsi stara ilivyokuwa kwa wanawake tangu wakati huo.
Pia katika masimulizi kwenye Al-Bukhaariy anasema, ''Wakati Nabii Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alipomuoa Haajar na akamzalia Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam), mkewe wa mwanzo, Sarah, akapata wivu na akaapa kuwa atamkata mwili wake vipande vitatu, hivyo Haajar akajifunga mkanda kiunoni mwake na kukimbia huku akiburuza vazi lake nyuma yake ili kufuta alama za nyayo zake ili Sarah asiweze kujua alipoelekea. [Al Bukhaariy - Kitabu cha Visa Vya Manabiim, Hadiyth namba 3364]
Na Allaah Anajua zaidi.
Safari ya Makkah:
Siku moja Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliamka na kumwambia mke wake Haajar ajitayarishe kwa safari ndefu. Baada ya siku chache, Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akaanza safari yake pamoja na mkewe na mwanawe Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) ambaye alikuwa bado ananyonya.
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akatembea na kupitia ardhi zilizolimwa, majangwa na milima hadi akafika katika jangwa la kisiwa cha Uarabu (Arabian Peninsula) na akafika katika bonde lisilolimwa ambalo halikuwa na miti wala matunda wala chakula wala maji. Bonde hilo halikuwa na athari yoyote ya maisha. Baada ya kumsaidia mkewe kuteremka kipando cha safari, akawaacha hapo wakiwa na chakula na maji kidogo tu ya kuwatosheleza kama siku mbili tu.
Aligeuka nyuma na kuondoka. Nyuma yake mkewe akamkimbilia na kumuuliza: "Unakwenda wapi ee Ibraahiym na kutuacha sisi katika bonde hili tupu?" Ibraahiym (‘alayhis-salaam) hakumjibu kitu bali aliendelea kuondoka. Haajar alirudia kumuuliza tena, lakini alinyamaza kimya bila ya kumjibu. Mwishowe alifahamu kuwa hafanyi hivyo kwa matamanio au amri yake, na akatambua kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemuamrisha kufanya hivyo. Akamuuliza: "Je, Allaah Amekuamrisha ufanye hivyo?". Akamjibu: "Naam". Haajar akasema: "Basi hatutapotea kwani Allaah Aliyekuamrisha Atakuwa nasi". Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akaondoka na alipokuwa mbali kiasi ya kutowaona akaomba:
رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿٣٧﴾
Rabb wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuria wangu katika bonde lisilokuwa na mmea wowote, kwenye Nyumba Yako Tukufu. Rabb wetu, ili wasimamishe Swalaah na Ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao na Uwaruzuku mazao ili wapate kushukuru. [Ibraahiym :37]
Kupatikana Maji Ya Zamzam:
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akamuacha mkewe na mwanawe katika jangwa na akarudi alikotoka kuendelea kufanya daawah ya kuwalingania watu katika katika Tawhiyd. Haajar akabakia kumlea mwanawe hapo alipoachwa. Chakula kiliwaishia, maziwa yakamkauka, jua lilikua kali mno, maji waliyokuwa nayo yalikwisha na kiu kikawashika, hali ikawa mbaya ya njaa ya kiu kikubwa.
Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) akaanza kulia kwa kiu. Mama yake akamuacha kwenda kutafuta maji. Akatembea kwa haraka hadi akafikia kilima cha Swafaa. Akapanda kilima na kuangaza kama ataona kisima au aone kama kuna msafara au chochote ili apate maji, lakini hakuona lolote. Akateremka kilima na akawa anahangaika kwenda baina ya kilima cha Swafaa na kilima cha Marwah, akipanda vilima vyote kila anapofikia kuangaza kama ataona lolote, lakini hakufanikiwa, na huku mwanawe anagaragara na kulia kwa kiu. Akawa anatembea na huku akikimbia mara nyingine baina ya Swafaa na Marwah kwa mara saba. Na ndio maana wenye kutekeleza ‘Umrah au Hajj, huwa wanatembea baina ya vilima viwili hivyo kama ni taratibu mojawapo ya ‘Umrah na Hajj.
Hakika hii taadhima kubwa aliyojaaliwa nayo Haajar, na ni fakhari kwa wanawake wote wa Kiislamu kuwa taratibu hiyo ya kutembelea baina ya vilima vya Swafaa na Marwah, imekuwa ni ibaada tukufu na inatekelezwa na milioni ya watu tokea zama za Hajj na itaendelea hadi siku ya Qiyaamah.
Alipofika Marwah kwa mara ya saba, alisikia sauti, mara akamuona Malaika anachimba ardhini kwa mbawa zake na mara maji yakamwagika kwa nguvu kabisa, akawa anayateka na kuyazuia yasimwagike zaidi.
عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((يرحم الله أم إسماعيل لو تركت زمزم)) أو قال: ((لو لم تغرف من الماء لكانت زمزم عينًا معينًا )) البخاري
Imetoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “(Allaah Amrehemu mama yake Ismaa'iyl angeliacha (maji ya Zamzam)) (yamwagike bila ya kuyazuia) au kasema ((asingelichota kutoka katika maji hayo, Zamzam ingelikuwa chemchemu inayoendelea kumwagika katika ardhi))” [Al-Bukhaariy]
Akanywa maji na kumnywesha mwanawe. Kulikuwa na misafara ya watu kutoka Yemen na walipoona kuna ndege wanazunguka wakatambua kuwa ni sehemu yenye maji. Walikuwa watu wa kabila la Jurhum kutoka Yemen wakaja kuishi hapo. Wakamuuliza Haajar: "Je, unaturuhusu tuishi hapa?" Akajibu: "Naam, lakini hamtakua na haki kumiliki maji haya ya Zamzam". Wakakubali na Haajar akaridhika na akafurahi kupata watu kuishi nao. Wakaleta familia zao na wakazidi kuwa wengi hapo.
Mtihani Mkubwa Aliopewa Nabiy Ibraahiym (‘alayhis-salaam) Wa Ndoto Ya Kumchinja Mwanawe Ismaa’iyl:
Miaka ikapita na Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akawa anamtembelea mkewe Haajar na mwanawe mara kwa mara. Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamtahini kuhusu mapenzi ya mwanawe Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam). Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema hayo katika Aayah zifuatazo:
وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَىٰ رَبِّي سَيَهْدِينِ ﴿٩٩﴾رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٠٠﴾فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلَامٍ حَلِيمٍ ﴿١٠١﴾فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَىٰ فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَىٰ ۚ قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ ۖ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّابِرِينَ ﴿١٠٢﴾فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ ﴿١٠٣﴾وَنَادَيْنَاهُ أَن يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿١٠٤﴾قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا ۚإِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ﴿١٠٥﴾إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْبَلَاءُ الْمُبِينُ ﴿١٠٦﴾وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ ﴿١٠٧﴾وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ ﴿١٠٨﴾سَلَامٌ عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ ﴿١٠٩﴾كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿١١٠﴾إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ ﴿١١١﴾
99. Akasema: Hakika mimi ni mwenye kwenda kwa Rabb wangu Ataniongoza. 100. Rabb wangu! Nitunukie miongoni mwa Swalihina. 101. Basi Tukambashiria ghulamu mvumilivu. 102. Alipofikia makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye; akasema: Ee mwanangu! Hakika mimi nimeona ndoto usingizini kwamba mimi nakunchinja, basi tazama unaonaje? (Ismaa’iyl) Akasema: Ee baba yangu! Fanya yale uliyoamrishwa, utanikuta In Shaa Allaah miongoni mwa wanaosubiri. 103. Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza kifudifudi juu ya kipaji. 104. Na tukamwita: Ee Ibraahiym. 105. Kwa yakini umesadikisha ndoto. Hakika Sisi hivyo ndivyo Tunavyolipa wafanyao ihsaan. 106. Hakika hili bila shaka ni jaribio bayana. 107. Na Tukamtolea fidia kwa dhabihu adhimu. 108. Na Tukamuachia (sifa nzuri) kwa karne za baadaye. 109. Salaamun! Amani iwe juu ya Ibraahiym. 110. Hakika hivyo ndivyo Tunavyolipa wafanyao ihsaan. 111. Hakika yeye ni miongoni mwa waja Wetu Waumini. [As-Swaaffaat: 99-111]
Hakika huu ulikuwa ni mtihani mkubwa kwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) wa kuoteshwa amchinje mwanawe kwa kuwa ni mwana mmoja tu aliyejaaliwa na ambaye aliyempenda sana, na aliyeruzukiwa baada ya kufika uzee.
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) anatupa fundisho ya adabu baina ya mzazi na mtoto, pindi alipomtajia Nabiy Ismaa’iyl kuwa ameoteshwa amchinje. Alimuuliza anaonaje? Basi Nabiy Ibraahiym (‘alayhis-saalaam) ameonyesha upole na huruma kwa mwanawe na adabu njema, kwa sababu, angelimchinja bila ya kumtaka ushauri wake maadamu ni amri ya kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na hivyo kwa kuwa ndoto za Manabii ni Wahyi kutoka kwa Allaah:
.. يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَىٰ فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَىٰ ۚ.. ﴿١٠٢﴾
Ee mwanangu! Hakika mimi nimeona ndoto usingizini kwamba mimi nakunchinja, basi tazama unaonaje? [As-Swaafaat: 102]
Na mtoto naye anatupa mafunzo kwa kuheshimu wito wa baba yake ambao anajua haukuja kwa matamanio yake bali ni kutimiza amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), amri ambayo baba yake alijua ni muhimu kuliko mapenzi ya mwanawe. Naye Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) alimjibu:
.. ۚ قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ ۖ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّابِرِينَ ﴿١٠٢﴾
Ee baba yangu! Fanya yale uliyoamrishwa, utanikuta In Shaa Allaah miongoni mwa wanaosubiri. [As-Swaaffaat:102]
Basi Nabiy Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alitambua mapenzi na utiifu wa mwanawe kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwani hakujali kuchinjwa bali aliona kutekeleza amri ya Mola wake ni muhimu kuliko maisha yake.
Nabiy Ibraahiym (alayhis-salaam) alimlaza Ismaa’iyl kifudifudi ili asimuone wakati anapomchinja, bila shaka kutokana na huruma. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ ﴿١٠٣﴾
Basi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza kifudifudi juu ya kipaji. [As-Swaaffaat:103]
Yaani: Wote wawili walitamka Shahaada na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwani alikuwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) anakaribia kumchinja Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam), hivyo ingelikuwa ni mauti yake. Au 'walipojisalimisha' ina maana kwamba walipofuata amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alimtii Mola wake na Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) pia alimtii baba yake. Hii ni rai ya Mujaahid, Ikrimah, Qataadah, As-Sudi na Ibn Is-haaq na wengineo. [At-Twabariy 21:77]
Maana ya:
.. وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ ﴿١٠٣﴾
na akamlaza kifudifudi juu ya kipaji.
ni kwamba, alimuelekeza uso wake kifudifudi ili amchinje kutoka kwa nyuma ili iwe wepesi kwake kufanya hivyo (asipate kuuona uso wake akashikwa na huruma na kushindwa kutekeleza amri ya Mola wake). Ibn 'Abbaas, Mujaahid, Sa'iyd bin Jubayr, Adhw-Dhwahaak na Qataadah wamesema ina maana kwamba, "Alimgeuza kifudifudi". [At-Twabariy 21:77, 78]
Shaytwaan Anamshawishi Ibraahiym Asimchinje Mwanawe Ismaa’iyl:
Imaam Ahmad amerekodi kwamba Ibn 'Abbaas amesema: "Wakati alipokuwa anataka kutekeleza Ibraahiym (‘alayhis-salaam) amri ya kumchinja 'Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam), shaytwaan alimjia katika Mas'aa na akakimbia naye, lakini Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alifika mwanzo. Kisha Jibriyl (‘alayhis-salaam) akamchukua katika Jamratul-'Aqabah na shaytwaan akamjia tena huko, kwa hiyo akamtupia vijiwe saba mpaka akatokomea. Kisha akamjia tena katika Jamratul-Wustwaa, akamtupia vijiwe saba. Kisha akamlaza kifudifudi. Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) alikuwa amevaa shati jeupe akasema: "Ee baba yangu, sina nguo yoyote ambayo nitakafiniwa, kwa hiyo nivue ili iwe nikafiniwe nayo.” Alianza kuivua ndipo alipoitwa nyuma:
وَنَادَيْنَاهُ أَن يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿١٠٤﴾قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا ۚإِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ﴿١٠٥﴾
104. Na tukamwita: Ee Ibraahiym. 105. Kwa yakini umesadikisha ndoto. Hakika Sisi hivyo ndivyo Tunavyolipa wafanyao ihsaan. [As-Swaaffaat:104-105]
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aligeuka, tahamaki akamuona kondoo mweupe mzuri mwenye pembe.
Ibn 'Abbaas kasema: "Tulikuwa tukitafuta aina kama ya huyo kondoo" (yaani wakati wa kuchinja katika 'Iydul-Adhwhaa) [Ahmad: 1:297]
As-Suddiy na wengineo wamesema kwamba alikipitisha kisu shingoni mwa Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) lakini hakikumkata kwa sababu aliwekewa bamba la shaba.
Na ndipo Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alipoitwa:
قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا ۚ…﴿١٠٥﴾
Kwa yakini umesadikisha ndoto [As-Swaaffaat:105]
[At-Twabariy 21:74]
Ibn 'Abbaas amesema kuwa: "Kondoo huyo alikuzwa Peponi kwa muda wa miaka arubaini". [At-Twabariy 21:90]
Kitendo hiki cha kuchinja ndicho kinachofanyika katika taratibu za Hajj, kufuata Sunnah ya baba yetu Ibraahiym (‘alayhis-salaam), ya kurusha vijiwe katika milingoti mitatu.
Uthibitisho Kwama Aliyetaka Kuchinjwa Ni Ismaa’iyl Na Sio Is-haaq Kama Wanavyodai Watu Wa Kitabu:
Imaam Ahmad amerekodi kwamba Swafiyyah bin Shaybah alisema: "Mwanamke kutoka Bani Sulaym ambaye alikuwa mkunga wa wengi katika jamii yetu, kaniambia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtuma 'Uthmaan bin Twalhah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akazifunike pembe katika Ka'bah ili zisiwashawishi watu wanaposwali: Akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
))إني كنتُ رأيت قرني الكبش، حين دخلت البيت، فنسيت أن آمرك أن تخمرهما، فَخَمَّرْهما، فإنه لا ينبغي أن يكون في البيت شيء يشغل المصلي". قال سفيان: لم يزل قرنا الكبش معلقين في البيت حتى احترق البيت، فاحترقا)) أحمد.
“Niliziona pembe za kondoo nilipoingia katika Nyumba (yaani Ka’bah) nikasahau kukuambia uzifunike, zifunike kwani kusiweko na kitu katika nyumba (Ka'bah) cha kuwashawishi watu wanaofanya ibada”. [Ahmad 4:68]
Wasimulizi waliosimulia kuhusu pembe hizo za kondoo:
-Sufyan kasema: "Pembe za kondoo zilibakia zikining'inia katika Nyumba (Ka'bah) hadi zilipoungua wakati Nyumba ilipoungua".
-Sa'iyd bin Jubayr, 'Aamir Ash-Sha'abiy, Yuusuf bin Mihraan, Mujaahid, 'Atwaa' na wengineo wameripoti kutoka Ibn 'Abbaas kwamba alikuwa ni 'Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam).
-Ibn Jariyr amesimulia kwamba Ibn 'Abbaas amesema: "Aliyefidiwa alikuwa ni Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam). Mayahudi wamedai kuwa ni Is-haaq, lakini Mayahudi wameongopa". [At-Twabariy 21:83]
-Ibn Is-haaq amesema, "Nimemsikia Muhammad bin Ka'ab Al-Quraazi anasema, "Ambaye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameamuamrisha Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kumchinja miongoni mwa wanawe wawili alikuwa ni Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam).
Tunapata dalili hii kutoka kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anapomalizia kisa cha mmoja wa wana wawili wa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ambaye alitakiwa kuchinjwa Anasema:
وَبَشَّرْنَاهُ بِإِسْحَاقَ نَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿١١٢﴾
Na Tukambashiria Is-haaq; Nabiy miongoni mwa Swalihina. [As-Swaaffaat:112]
Vile vile,
وَامْرَأَتُهُ قَائِمَةٌ فَضَحِكَتْ فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَاقَ وَمِن وَرَاءِ إِسْحَاقَ يَعْقُوبَ﴿٧١﴾
Na mkewe amesimama wima, akacheka; Tukambashiria Is-haaq na baada ya Is-haaq ni Ya’quwb. [Huud:71]
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemtaja mtoto na mwanawe (Ya’quwb), lakini Asingelimuamrisha kumchinja Is-haaq wakati Aliahidi kuwa mwanawe (Is-haaq) atazaa mtoto. Kwa hiyo ni dhahiri kuwa yule aliyeamrishwa amchinje ni Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam). [At-Twabariy 21:84].
Hadiyth nyingi zimenukuliwa kuhusu mas-ala haya [Tafsiyr Ibn Kathiyr 8:277-279]
Ziara Ya Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) Kwa Wake Zake Ismaa’iyl:
Maelezo haya yamenukuliwa kutoka Hadiyth ndefu ya Ibn 'Abbaas iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy:
Baada ya kufa mama yake Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam), Ibraahiym alikuja kumtembelea Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) nyumbani kwake (ambaye alikuwa amekwishaoa). Alipofika hakumkuta Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) bali alimkuta mkewe peke yake. Akamuuliza: "Yuko wapi Ismaa'iyl?" Akajibu: "Amekwenda kutafuta rizki". Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akamuuliza kuhusu hali ya maisha yao, akajibu: "Tunaishi katika shida, dhiki na karaha". Akamwambia: "Atakaporudi mumeo mpe salam zangu na mwambie abadilishe kizingiti chake".
Aliporudi Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) alihisi hali sio ya kawaida yaani kama kumetokea kitu, akamuuliza mkewe: "Je, amekuja mtu yeyote kukutembelea?" Akajibu: "Naam! Ni Bwana mmoja mtu mzima mwenye sifa kadha na kadha amekuja na ameniuliza kuhusu wewe nikamjulisha, kisha akaniuliza kuhusu hali ya maisha, nikamuambia kuwa tunaishi katika shida, dhiki na umasikini". Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) hapo akamuuliza: "Je, amekupa maagizo yangu yoyote?". Akajibu: "Naam! Amenipa salaam zako, kisha amesema nikuambie kuwa ubadilishe kizingiti chako". Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) akasema: "Huyo ni baba yangu, na ameniamrisha nikutaliki, hivyo basi rudi kwenu". Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) akampa talaka, kisha akaoa mwanamke mwingine miongoni mwao (yaani kutoka kabila la Jurhumu).
Mara ya pili alipokuja Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kumtembelea Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) alimkuta mke wake Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) wa pili, alipoumuuliza kuhusu Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) alisema: "Amekwenda kutafuta rizki". Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akamuuliza kuhusu maisha yao, akajibu: "Tuko katika neema na tumebahatika (yaani tuna kila kitu cha kututosheleza)". Akamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akamuuliza: "Aina gani ya chakula mnakula?" Akasema: "Nyama". Akasema: "Mnakunywa nini?", Akasema: "Maji". Akasema: "Ya Allaah Wabarikie nyama yao na maji yao". (Mke huyo wa Ismaa’iyl amesema hivyo ingawa hali yao ilikuwa ni ya shida).
Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akamwambia mke wa Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam): "Atakaporudi mumeo mpe salaam zangu na mwambie ashikilie kizingiti chake". Aliporudi Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) alimuuliza mkewe: "Je, amekuja mtu yeyote?". Akajibu: "Naam! Amekuja bwana mmoja mtu mzima mwenye sura nzuri". Akamsifia kisha akaendelea: "Ameniuliza kuhusu wewe nikamjulisha, kisha akauliza kuhusu hali ya maisha yetu, nikamuambia kuwa tunaishi katika hali nzuri". Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) akamuuliza: "Je, alikupa nasiha yoyote?" Akajibu: "Naam! Amekupa salaam zake kisha anakuamrisha ushikilie kizingiti chako".
Kwa maneno haya, Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) akasema: "Huyo alikuwa ni baba yangu na wewe ndio kizingiti, na ameniamrisha nibakie na wewe".