Fadhila Na Sifa Za Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام)
Fadhila Na Sifa Za Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام)
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِّلَّـهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ﴿١٢٠﴾
Hakika Ibraahiym alikuwa mwenye akhlaaq na maadili yote mema, mtiifu kwa Allaah, aliyeelemea haki, na hakuwa miongoni mwa washirikina.
شَاكِرًا لِّأَنْعُمِهِ ۚ اجْتَبَاهُ وَهَدَاهُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴿١٢١﴾
Mwenye kushukuru Neema Zake, (Naye Allaah) Akamteua na Akamuongoza kuelekea njia iliyonyooka.
وَآتَيْنَاهُ فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً ۖ وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ﴿١٢٢﴾
Na Tukampa duniani mazuri. Na hakika yeye Aakhirah bila shaka ni miongoni mwa Swalihina.
ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ﴿١٢٣﴾
Kisha Tukakufunulia Wahy (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba fuata mila ya Ibraahiym aliyeelemea haki na hakuwa miongoni mwa washirikina.
[An-Nahl: 16:120-123]
Katika Aayah (120-123) za Suwrah hii An-Nahl, Allaah (سبحانه وتعالى) Amemsifia Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) kwa sifa zifuatazo: Mwenye akhlaaq na maadili yote mema, mtiifu, Haniyfah (ameelemea katika haki), hakuwa katika washirikina, mwenye kushukuru Neema za Allaah (سبحانه وتعالى), mwongofu na miongoni mwa Swalihina.
Na katika Suwrah nyenginezo, Allaah (سبحانه وتعالى) Amemsifia pia kwa sifa nyenginezo mbalimbali na Akamjaalia kuwa na fadhila tele.
Miongoni Mwa Fadhila Za Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام):
-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemteua yeye Nabiy Ibraahiym na mwanawe Nabiy Ismaa’iyl (عليهما السّلام) waijenge Al-Ka’bah. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akamteua Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) awatangazie watu kwenda kutekeleza Hajj. Hivyo basi, akawa yeye (عليه السّلام) na ahli wake ni mwongozo kwa watu katika utekelezaji wa manaasik (ibaada na taratibu) za Hajj na ‘Umrah. Rejea Al-Hajj (22:26-37). Na miongoni mwa manaasik hizo, ni kuswali katika Maqaam Ibraahiym baada ya kutufu Al-Ka’bah. Rejea Al-Baqarah (2:125). Pia, kusai baina ya Swafaa na Marwah, rejea Al-Baqarah (2:158) kama ni kigezo cha mkewe Haajar alipokuwa akihangaika kumtafutia maji mwanawe Ismaa’iyl (عليه السّلام). Na huko ndiko palipotokea mbubujiko wa maji ya Zamzam ambayo watu wanakunywa kwa niya tofauti kama alivyogusia hilo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Pia kuchinja mnyama baada ya yeye kupewa mtihani au majaribio makubwa, pindi alipoona njozini kuwa anamchinja mwanawe, naye kutokana na utiifu wake, akataka kutekeleza njozi hiyo akiamini kuwa ni Amri ya Allaah (سبحانه وتعالى). Lakini kumbe ilikuwa ni mtihani na jaribio, hivyo akafaulu katika hili, na hapo Allaah (سبحانه وتعالى) Akambadilishia kwa kumteremshia kondoo kutoka mbinguni ili amchinje badala ya mwanawe. Rejea Asw-Swaaffaat (37:101-107). Pia kutupia vijiwe Jamaraat ambayo ni katika waajibaat za Hajji na Sunnah zake nyenginezo.
-Ni kipenzi cha Allaah. Rejea An-Nisaa (4:125).
-Ameitwa Baba wa Manabii: Kama ilivyokuwa hali ya Nabiy Nuwh (عليه السّلام): Al-‘Ankabuwt (29:27). Na katika Al-Hadiyd (57:26), ametajwa yeye Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) pekee kuwa amejaaliwa kuwa na Unabii na kupewa Kitabu.
Imaam Ibn Kathiyr amesema kuhusu Aayah ya Suwrah Al-‘Ankabuwt: “Hii ni fadhila na baraka kubwa sana. Sio tu kwamba Allaah Alimfanya (Nabiy Ibraahiym) kuwa ni kipenzi Chake na kumfanya Imaam wa watu, bali pia Alijaalia Unabii na Kitabu kuwa katika dhuriya zake. Baada ya zama za Ibraahiym, hapakuwa na Nabii ambaye hakutokana na kizazi chake. Manabii wote wa Wana wa Israaiyl (Ya’quwb) walikuwa katika kizazi chake, kuanzia Ya’quwb bin Is-haaq bin Ibraahiym hadi wa mwisho wao, `Iysa bin Maryam, ambaye alisimama kuwatangazia kaumu yake, bishara ya kuja kwa Nabii Mwarabu, Al-Qurashiy, Al-Haashimiy, Nabii wa mwisho wa Manabii wote, bwana wa wana wa Aadam katika dunia hii na Aakhirah, ambaye Allaah Alimteua kutoka kwa Waarabu safi wa asili kutoka kwa kizazi cha Ismaa’iyl bin Ibraahiym (عليهما السلام). Hakuna Nabii yeyote katika ukoo wa Ismaa’iyl isipokuwa yeye Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). [Tafsiyr Ibn Kathiyr]
-Ameomba duaa kizazi chake kitoe Nabii wa mwisho; Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) baada ya kujenga Al-Ka’bah. Rejea (2:129).
-Ibraahiym (عليه السّلام) ni Imaam wa Tawhiyd:
Allaah (سبحانه وتعالى) Amemfanya kuwa ni Imaam wa watu wa kufuatwa katika Tawhiyd. Rejea Al-Baqarah (2:124). Na pia Ummah umeusiwa kufuata mila yake. Rejea Al-Baqarah (2:135), Aal-‘Imraan (3:95), An-Nisaa (4:125), Al-An’aam (6:161), na An-Nahl (16:123). Na pia, Amewausia wanawe na kizazi chake Uislamu. Rejea Al-Baqarah (2:130-132). Na pia Amefanya neno la Tawhiyd (laa ilaaha illa-Allaah) lenye kubakia katika kizazi chake. Rejea Az-Zukhruf (43:28). Ingawa Rusuli wengineo wote wamekuja pia katika kulingania Tawhiyd, ila Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) amekuwa ni makhsusi kwa Tawhiyd. Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله) amesema alipoulizwa:
Kwa nini Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) amehusishwa zaidi na Tawhiyd, ilhali Manabii wote wengineo wamelingania Tawhiyd?
Akajibu: Manabii wote wamekuja na (kulingania) Tawhiyd. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ ﴿٢٥﴾
“Na Hatukutuma kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Rasuli yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: Hakika hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi, basi Niabuduni.” [Al-Anbiyaa (21:25)]
Lakini Ibraahiym ni baba wa Waarabu, na baba wa Waisrael, naye amelingania Tawhiyd khalisi, na Mayahudi na Manaswara wamedai kuwa ni wafuasi wake, na Waislamu ndio wafuasi wake. Kwa hiyo yeye (عليه السّلام) akahusishwa kuwa ni baba wa Manabii, na kwamba yeye ndiye mwenye Haniyfiyyah (sifa ya kuelemea haki na kujiweka kando na shirki). Na sisi tumeamrishwa kumfuata, kwa sababu sisi ndio tulio karibu zaidi Ibraahiym kama Anavyosema Allaah (عزّ وجلّ):
إِنَّ أَوْلَى النَّاسِ بِإِبْرَاهِيمَ لَلَّذِينَ اتَّبَعُوهُ وَهَـٰذَا النَّبِيُّ وَالَّذِينَ آمَنُوا ۗ وَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٦٨﴾
“Hakika watu walio karibu zaidi kwa Ibraahiym ni wale waliomfuata na huyu Nabiy (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na wale walioamini. Na Allaah Ni Mlinzi wa Waumini.” [Aal-‘Imraan (3:68)]
Na Akasema kuwaradi Mayahudi na Manaswaara:
مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلَا نَصْرَانِيًّا وَلَـٰكِن كَانَ حَنِيفًا مُّسْلِمًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٦٧﴾
“Ibraahiym hakuwa Yahudi wala Naswara, lakini alikuwa mwenye kujiengua na upotofu akaelemea Dini ya haki, Muislamu na hakuwa miongoni mwa washirikina.” [Aal-‘Imraan (3:67)]
[Liqaa-a Al-Baab Al-Maftuwh Swali namba (7/189).
-Anatajwa katika kila Swalaah, kwenye Tashahhud, kwa Swalaah inayojulikana kama Swalaatul-Ibraahiymiyyah.
Na fadhila hii tukufu ni kutokana na sababu zilizotangulia kutajwa juu na Imaam Ibn ‘Uthaymiyn. Pia kutokana na sababu zifuatazo kama walivyosema ‘Ulamaa: Kwamba (عليه السّلام) Ibraahiym ni babu (kizazi kilichoanzia kwa Ismaaiyl) wa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم)
Na ‘Allaamah Badr Ad-Diyn Al-Hanafiy (رحمه الله) ana maelezo mengineyo katika kubainisha sababu ya hili. Amesema: “Ikiwa mtu atauliza: Kwa nini Ibraahiym (عليه السّلام) ameteuliwa yeye pekee kutajwa katika Swalaah badala ya Manabii wengine (عليهم السّلام)?
Nitajibu: Kwa sababu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwaona katika usiku wa Mi’iraaj, Manabii na Rusuli wote, na akamtolea Salaam kila Nabii, na hakuna hata mmoja wao aliyesalimia ummah wake isipokuwa Ibraahiym (عليه السّلام) . Hivyo basi, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametuamrisha tumswalie kila mwisho wa Swalaah mpaka Siku ya Qiyaamah, kama malipo ya wema wake. Na imesemwa: Ibraahiym (عليه السّلام) alipomaliza kuijenga Al-Ka’bah, aliuombea Ummah wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: Ee Allaah! Atakayehiji Nyumba hii miongoni mwa Ummah wa Muhammad, basi Mpe amani kutoka kwangu. Pia akawaombea ahli zake na watoto wake kwa duaa hii. Hivyo basi tukaamrishwa tuwakumbuke katika Swalaah kama malipo ya wema wao.” Mwisho. Ufafanuzi wa Sunan Abi Daawuwd cha Al-‘Ayniy (4/260). Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
-Kizazi chake kimepewa ufalme mkubwa: An-Nisaa (4:54).
-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimkuta mbingu ya saba akielemea Bayt Al-Ma’muwr inayozungukwa na Malaika elfu sabiini. (Haya yapo katika Hadiyth ndefu iliyopokelewa na Imaam Muslim katika Kitaab Al-Iymaan, na wengineo).
-Alijaaliwa Ar-Rushd (Uongofu) na Allaah (سبحانه وتعالى) Alimjua vyema: Al-Anbiyaa (21:51).
-Ni Nabii ambaye amemshabihi Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم): Hadiyth ya Abu Hurayrah (رضي الله عنه) [Al-Bukhaariy, Muslim]
-Ni miongoni mwa Rusuli watano wa Ulul-‘Azmi: Al-Ahzaab (33:7).
-Amewaombea Waislamu wawe wenye kuelekeza nyoyo zao kuipenda Makkah na Al-Ka’bah. Ibraahiym (14:37).
-Amewaombea duaa kizazi chake wasimamishe Swalaah, na Amewaombea Waumini maghfirah Siku ya Hesabu. Ibraahiym (14:40-41).
-Atakuwa wa kwanza kuvalishwa nguo baada ya kufufuliwa kutokana na vile washirikina katika kaumu yake walivyomuingiza motoni akiwa uchi baada ya kuvunja masanamu yao. Yapo haya kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما):
Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Enyi watu, hakika mtafufuliwa na Allaah hali ya kuwa hamna viatu, mpo uchi na bila kutahiriwa (na magovi). ”Kisha akasoma:
كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ
Kama Tulivyoanza umbo la awali Tutalirudisha tena. [Al-Anbiyaa (21:104)]
Tanabahini! Hakika mtu wa kwanza atakayevishwa nguo ni Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na ‘Ulamaa wameeleza pia kuwa sababu ya kutangulizwa Ibraahiym kuvishwa nguo Siku ya Qiyaamah kabla ya wengine ni kuwa hapakuweko miongoni mwa watu wa mwanzo na wa baadae, waliomkhofu zaidi Allaah kuliko yeye. Hivyo basi, nguo zitamharakia ili kumhifadhi, na moyo wake upate kutulia.
Na sababu nyingine -kama ilivyoeleza Hadiyth- ni kuwa, inawezekana kwamba yeye alikuwa ni wa kwanza kuvaa suruali wakati anaposwali ili kupata sitara ya ziada isiyo na shaka na kulinda tupu yake isigusane na sehemu yake ya kuswalia, naye akafanya kama alivyoamrishwa, na akalipwa hilo kuwa wa kwanza kusitiriwa Siku ya Qiyaamah.
Kadhalika, inawezekana kuwa wale waliomtupa motoni, walimwacha uchi na wakamvua nguo zote mbele ya watu kama anavyofanywa mtu anayetekelezewa adhabu ya kifo. Hivyo atalipwa nguo zake Siku ya Qiyaamah, na atakuwa mtu wa kwanza kuvaa mbele ya halaiki, na haya ni malipo mazuri zaidi. [Al-Qurtwubiy katika At-Tadhkirah]
-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema kwamba yeye ni kiumbe bora kabisa: Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه): Alikuja mtu mmoja kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia: “Ee kiumbe bora kabisa!” Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamjibu: “Huyo ni Ibraahiym (عليه السّلام). [Muslim]
Sifa Za Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام):
-Hakuwa mshirikina kabisa. Ametajwa kwa sifa hii katika Suwrah kadhaa kwenye Qur-aan ikiwemo Suwrah hii An-Nahl (16:120). Pia, kisa chake katika Al-An’aam (6:74-81) cha kutokuabudu nyota wala mwezi wala jua kinathibitisha sifa hii. Kadhalika, alimuomba Allaah Amuepusha yeye na wanawe wasiwe washirikina: Ibraahiym (14:35). Isitoshe, alimnasihi baba yake pia asiwe mshirikina lakini hakumsikiliza bali alimfukuzilia mbali: Maryam (19:41-48) na Ash-Shu’araa (26:69-89).
-Alikuwa ni mtimizaji ahadi: An-Najm (53:37).
-Ni mwenye huruma mno na mvumilivu: At-Tawbah (9:114).
-Ni mvumilivu sana, mnyenyekevu mno kwa Allaah, na mwingi wa kurejea Kwake. Huwd (11:75).
-Mkarimu mno: Huwd (11:69), na Adh-Dhaariyaat (51:24-26).
-Mwenye utukufu: Rejea Tanbihi namba 1 ya Aayah namba (4) katika Suwrah Yuwsuf.
-Mnyeyekevu, kwani aliomba duaa baada ya kujenga Al-Ka’bah: Al-Baqarah (2:128). Al-Ka’bah ni Nyumba Tukufu kabisa katika Vitukufu vya Allaah katika Mji Mtukufu kabisa. Lakini juu ya utukufu huu, alikuwa na wasiwasi juu ya kutaqabaliwa kitendo hiki, kwa maana hakuwa na kibri kuwa madamu amejenga kitu kitukufu kabisa cha Allaah, basi awe amesifika au ni mtu bora kabisa.
-Ana kisa muhimu cha uthibitisho wa Tawhiyd iliyojikita moyoni mwake wakati alipoingizwa motoni na watu wake kwa sababu aliyavunja masanamu waliyokuwa wakiyaabudu: Al-Anbiyaa (21:51-70), na Asw-Swaaffaat (37:83-99).
-Mwenye moyo uliosalimika: Asw-Swaaffaat (37:84).
-Swiddiyq (mkweli wa kidhati): Maryam (19:41).
-Mwenye akhlaaq na mfano wa maadili mema: Al-Mumtahinah (60:4).
-Amekhitariwa duniani, na Aakhirah ni miongoni mwa Swalihina: Al-Baqarah (2:130).
-Mwenye nguvu na busara: Swaad (38:45). Na katika busara zake, alimwambia mwanawe Ismaa’iyl abadilishe kizingiti chake badala ya kumwambia moja kwa moja “mwache mkeo.” Hii ni kutokana na malalamiko ya mke huyo kuhusu maisha yao na shida zao. Kisha akamtaka athibitishe kizingiti chake, akimaanisha aendeleze ndoa yake na mkewe mwengine (asimtaliki), mke wa pili ambaye hakulalamika shida zao za kimaisha. Maelezo ya hili yapo katika Hadiyth ndefu ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) iliyopokelewa na Al-Bukhaariy, Kitaab Ahaadiyth Al-Anbiyaa.
Pia katika busara zake ni kumtaka mfalme Namruwd aliyejifanya kuwa yeye ni Mola na mwabudiwa, alichomoze jua kutoka Magharibi badala ya Mashariki, lakini mfalme huyo akabakia kinywa wazi ameduwaa. Rejea Al-Baqarah (2:258) kwenye maelezo bayana katika faida ya Aayah hiyo.
Pia katika busara yake nyengineyo ni vile alivyovunja masanamu kisha akatundika shoka ya sanamu lilokuwa kubwa lao. Kaumu yake walipomuuliza nani aliyevunja masanamu yetu, alijibu: “Waulizeni wakiwa wanaweza kunena!” Akikusudia pia kama kweli wanastahiki kuabudiwa ikiwa hawawezi kujihami wenyewe kusingiziwa uvunjaji wa masanamu yao. Rejea Al-Anbiyaa (21:57-63), na Asw-Swaafaat (37:88-96)
-Alikhofia familia yake wasije kuabudu masanamu. Naye mwenyewe tokea utotoni alichukia ibaada ya shirki na masanamu. Na alikhiari Dini kuliko dunia, napo ni pale alipowaacha familia yake katika bonde la Makkah ambako hapakuwa na chochote, na alitaja sababu yake kuwa ili wasimamishe Swalaah: Ibraahiym (14:35-37).
Hizo ni baadhi ya fadhila na sifa za Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) , na bila shaka zinapatikana nyenginezo katika Kitabu na Sunnah.