Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) - 2

 

Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) – 2

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Da'wah Kwa Baba Yake: 

 

 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alikuwa akiumia kupita kiasi kumuona baba yake (Au ‘ammi yake aliyemlea kama walivyonukuu baadhi ya Mufassiriyn) kuwa anaabudu masanamu. Bali akiumia zaidi kwani yeye huyo baba yake ndiye aliyekuwa akichonga hayo masanamu. Hii ni tabia ya mwenye kufanya da'wah anapoona jamaa zake wenyewe wako katika upotofu na khaswa inapokuwa jamaa aliye karibu zaidi kama baba, mama, ndugu, watoto na kadhalika. Kwa hiyo, lilikuwa tamanio lake kubwa kumtoa baba yake kutoka katika upotofu na kumuingiza katika Tawhiyd. Akamuita kwa maneno ya upole kabisa na kumpa kila hoja ili atambue upotofu huo:  

 

 

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا ﴿٤٢﴾ يَا أَبَتِ إِنِّي قَدْ جَاءَنِي مِنَ الْعِلْمِ مَا لَمْ يَأْتِكَ فَاتَّبِعْنِي أَهْدِكَ صِرَاطًا سَوِيًّا ﴿٤٣﴾ يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ عَصِيًّا ﴿٤٤﴾ يَا أَبَتِ إِنِّي أَخَافُ أَن يَمَسَّكَ عَذَابٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ فَتَكُونَ لِلشَّيْطَانِ وَلِيًّا ﴿٤٥﴾

42. Pindi alipomwambia baba yake: Ee baba yangu! Kwa nini unaabudu vile visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa kitu chochote? 43. Ee baba yangu! Hakika mimi imekwishanijia elimu isiyokufikia wewe; basi nifuate nikuongoze njia iliyonyooka.  44. Ee baba yangu! Usimwabudu shaytwaan. Hakika shaytwaan daima ni mwenye kumuasi Ar-Rahmaan. 45. Ee baba yangu! Hakika mimi nakhofu isikushike adhabu kutoka kwa Ar-Rahmaan, ukaja kuwa rafiki kwa shaytwaan. [Maryam: 42-45]

 

Lakini baba yake Ibraahiym (‘alayhis- salaam) hakutaka kuacha ibada yake na hakupendezewa na wito wa mwanawe, na ingawa Ibraahiym (‘alayhis- salaam) alimuita kila mara kwa upole na adabu kabisa kama aya hizo za juu "Ee baba yangu", baba yake hakumjibu kwa upole wala hakuonyesha adabu baina ya baba na mtoto, bali alimtisha kuwa akiendelea kumwita katika ibada yake atamfukuza na kumpiga mawe kama ilivyotajwa katika Kauli Zake Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

قَالَ أَرَاغِبٌ أَنتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْرَاهِيمُ ۖ لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ ۖ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا ﴿٤٦﴾

(Baba yake) Akasema: Unachukia waabudiwa wangu ee Ibraahiym? Usipokoma, bila shaka nitakupiga mawe; na niondokelee mbali kwa muda mrefu! [Maryam:46]

 

Hata hivyo Ibraahiym (‘alayhis-salaam) anatupa mafunzo makubwa hapa kuwa juu ya kwamba alimuita baba yake kwa upole na adabu kisha baba yake akamjibu kwa kumkemea, majibu ya Ibraahiym (‘alayhis-salaam) yalikuwa ni ya uzuri zaidi kwa kumtakia amani iwe juu yake na kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amghufurie. 

 

قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَىٰ أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاءِ رَبِّي شَقِيًّا ﴿٤٨﴾

 47. (Ibraahiym) Akasema: Salaamun ‘Alayka. (Amani iwe juu yako). Nitakuombea maghfirah kwa Rabb wangu. Hakika Yeye daima ni Mwenye kunihurumia sana.  48.  Na natengana nanyi na mnavyoviomba badala ya Allaah; na namuomba Rabb wangu asaa nisijekuwa mwenye kunyimwa du’aa yangu kwa kumwomba Rabb wangu. [Maryam:47- 48]

 

 

Baba Yake Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Atageuzwa Kuwa Fisi Siku Ya Qiyaamah Na Kutupwa Motoni:

 

 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alijiombea Du'aa mwenyewe na kumuombea baba yake:  

 

رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿٨٣﴾وَاجْعَل لِّي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الْآخِرِينَ ﴿٨٤﴾وَاجْعَلْنِي مِن وَرَثَةِ جَنَّةِ النَّعِيمِ ﴿٨٥﴾وَاغْفِرْ لِأَبِي إِنَّهُ كَانَ مِنَ الضَّالِّينَ ﴿٨٦﴾وَلَا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ ﴿٨٧﴾يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

83. Rabb wangu! Nitunukie hikmah; elimu ya Dini na Unikutanishe na Swalihina.  84. Na Nijaalie kusifika kwa heshima kwa vizazi watakaokuja baadaye.   85. Na Nijaalie miongoni mwa warithi wa Jannah ya neema.  86. Na Mghufurie baba yangu, hakika yeye amekuwa miongoni mwa waliopotea.  87. Na wala Usinihizi Siku watakayofufuliwa.  88. Siku hayatofaa mali wa watoto. 89. Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu'araa: 83-89]

 

Tunaona kwamba katika Du'aa hizo Ibraahiym (‘alayhis-salaam) amemuombea baba yake maghfira kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ ۚ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ ﴿١١٤﴾

Na haikuwa Ibraahiym kumuombea maghfirah baba yake isipokuwa kwa sababu ya ahadi aliyoahidiana naye. Lakini ilipombainikia kwamba yeye ni adui wa Allaah, alijiepusha naye. Hakika Ibraahiym ni mwenye huruma mno na mvumilivu. [At-Tawbah:114]

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: "Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliendelea kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amghufurie baba yake mpaka alipokufa. Baada ya hapo alipotambua kwamba baba yake amekufa akiwa ni adui ya Allaah, akajitenga naye".   [At-Twabariy 14.519]

 

 

Katika kauli ya

وَلَا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ ﴿٨٧﴾

Na wala Usinihizi Siku watakayofufuliwa. [Ash-Shu'araa 87]

 

Imaam Al-Bukhaariy amesimulia Hadiyth ifuatayo:

 

عن أبي هريرة، رضي الله عنه، عن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((إن إبراهيم رأى أباه يوم القيامة عليه الغَبَرَةُ والقَتَرَةُ))  البخاري 4768

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasul wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “ Ibraahiym atamuona baba yake siku ya Qiyaamah akiwa amefunikwa na vumbi na kiza” [Al-Bukhaariy 4768].

 

Usimulizi mwingine kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

يلقى إبراهيم أباه، فيقول: يا رب، إنك وعدتني أنك لا تخزيني يوم يبعثون. فيقول الله: إني حرمت الجنة على الكافرين

Ibraahiym atakutana na baba yake na atasema: "Ee Rabb, Umeniahidi kwamba Hutonihizi siku watakaofufuliwa viumbe vyote". Allaah Atasema: "Nimeiharamisha Jannah (Pepo) kwa makafiri" [Fat-h Al-Baariy 8:357]

 

Usimulizi mwingine vile vile:

 

((يلقى إبراهيم أباه آزر يوم القيامة، وعلى وجه آزر قَتَرَةٌ وغَبَرة، فيقول له إبراهيم: ألم أقل لك: لا تعصني فيقول أبوه: فاليوم لا أعصيك. فيقول إبراهيم: يا رب، إنك وعدتني ألا تخزيني يوم يبعثون، فأي خزي أخزى من أبي الأبعد؟ فيقول الله تعالى: إني حرمت الجنة على الكافرين. ثم يُقال: يا إبراهيم، ما تحت رجليك؟ فينظر فإذا هو بذبح متلطخ، فيؤخذ بقوائمه فيلقى في النار)) البخاري

Ibraahiym atakutana na baba yake Aazar siku ya Qiyaamah na kutakuweko na vumbi na kiza usoni mwa Aazar. Ibraahiym atamuambia: "Sikukuambia kwamba usiniasi?". Baba yake atasema: "Leo sikuasi". Ibraahiym atasema: "Ee Rabb, Umeniahidi kwamba hutonihizi siku watakaofufuliwa, lakini hizaa gani itakuwa kubwa zaidi ya kumuona baba yangu katika hali hii?". Allaah Atamuambia: "Nimeharamisha Jannah (Pepo) kwa makafiri". Kisha itasemwa: "Ee Ibraahiym! Tazama chini ya miguu yako". Atatazama na ataona (kwamba baba yake amebadilishwa kuwa) fisi amefunikwa katika samadi/kinyesi, atachukuliwa kwa miguu yake na kutupwa motoni. [Al-Bukhaariy 3350 katika kunukuliwa na Fat-h Al-Baariy 6:445]

 

Kugeuzwa baba yake Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kuwa fisi ni Rahma kutoka kwa Allaah ili Ibraahiym (‘alayhis-salaam) asimuone baba yake katika sura yake akiwa anatupwa motoni. 

 

 

Kuvunja Masanamu:

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuambia kuhusu Khaliyl Wake Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na vipi Alivyomjaalia uongofu tokea zamani yaani tokea udogoni mwake. Alimpa moyo kwa kumuonyesha haki na dalili dhidi ya watu wake kwa yale waliokuwa wakiabudu kama Anavyosema:

 

وَتِلْكَ حُجَّتُنَا آتَيْنَاهَا إِبْرَاهِيمَ عَلَىٰ قَوْمِهِ ۚ .. ﴿٨٣﴾

Na hiyo ndio hoja Yetu Tuliyompa Ibraahiym juu ya watu wake... [Al-An'aam:83]

 

Na kumpa uongofu tokea alipokuwa mdogo Anasema Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa 

وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِهِ عَالِمِينَ ﴿٥١﴾

Na kwa yakini Tulimpa Ibraahiym uongofu wake kabla, na Tulikuwa Wenye kumjua vizuri. [A-Anbiyaa:51]

 

Na ndio maana alipokuwa mdogo alikuwa anashangazwa na ibada yao ya masanamu, akiyaendea masanamu hayo kuyatazama na kuona jinsi walivyokuwa wapumbavu watu wake kuabudu mawe yaliyochongwa ambayo akiona kuwa hayawezi kuwafaa kitu wala kuwadhuru kitu.

 

Akaapa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kuwa atayavunja haya masanamu, na alipoapa kiapo hicho mmoja wa watu wake alimsikia. Walikuwa wana sikukuu ambayo walikuwa wakienda wote kusherehekea. Yeye akabakia, na walipomuuliza sababu ya kutokwenda aliwajibu kuwa anaumwa. 

فَنَظَرَ نَظْرَةً فِي النُّجُومِ ﴿٨٨﴾فَقَالَ إِنِّي سَقِيمٌ ﴿٨٩﴾ 

Akatazama mtazamo katika nyota. 89. Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa. [As-Swaaffaat: 88-89]

 

Ilikuwa siku moja baada ya kuapa kuwa atayavunja masanamu.  Watu wake wakatoka kwenda kwenye sherehe zao, huku nyuma Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akayavunja masanamu yote isipokuwa sanamu kubwa kabisa, akachukua shoka alilotumia kuwavunjia na kuliweka katika mikono ya hilo sanamu kubwa ili watu wafikiri kuwa hilo sanamu ndilo lililovunja masanamu mingine. Akaanza kwa kuapa kuwa atayafanyia hila masanamu yao:

وَتَاللَّـهِ لَأَكِيدَنَّ أَصْنَامَكُم بَعْدَ أَن تُوَلُّوا مُدْبِرِينَ ﴿٥٧﴾فَجَعَلَهُمْ جُذَاذًا إِلَّا كَبِيرًا لَّهُمْ لَعَلَّهُمْ إِلَيْهِ يَرْجِعُونَ ﴿٥٨﴾ 

57. Na naapa kwa Allaah, bila shaka nitafanyia hila masanamu yenu baada ya mkishageuka kwenda zenu. 58. Basi akayavunja vipande vipande isipokuwa kubwa lao ili wapate kulirejea. [Al-Anbiyaa: 57-58]

 

Walikuwa wanawaekea chakula masanamu yao na alipokwenda kuyavunja masanamu Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliyasemesha na kuyauliza masanamu kwa kejeli:

 

فَتَوَلَّوْا عَنْهُ مُدْبِرِينَ ﴿٩٠﴾ فَرَاغَ إِلَىٰ آلِهَتِهِمْ فَقَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ ﴿٩١﴾مَا لَكُمْ لَا تَنطِقُونَ ﴿٩٢﴾ فَرَاغَ عَلَيْهِمْ ضَرْبًا بِالْيَمِينِ ﴿٩٣﴾

90. Wakaachana naye wakimgeukilia mbali kwenda zao.   91. Akaenda kwa siri kwa waabudiwa wao; akasema: Mbona hamli?  92. Mna nini! Mbona hamsemi?
93. Akayakabili (masanamu) kwa siri akawapiga kwa mkono wa kulia. [As-Swaaffaat: 90-93]

 

Waliporudi wakapatwa na mshangao mkubwa kuona masanamu yao wanayoyaabudu yamevunjwa! 

 

 قَالُوا مَن فَعَلَ هَـٰذَا بِآلِهَتِنَا إِنَّهُ لَمِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٩﴾ قَالُوا سَمِعْنَا فَتًى يَذْكُرُهُمْ يُقَالُ لَهُ إِبْرَاهِيمُ ﴿٦٠﴾قَالُوا فَأْتُوا بِهِ عَلَىٰ أَعْيُنِ النَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَشْهَدُونَ ﴿٦١﴾قَالُوا أَأَنتَ فَعَلْتَ هَـٰذَا بِآلِهَتِنَا يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿٦٢﴾قَالَ بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَـٰذَا فَاسْأَلُوهُمْ إِن كَانُوا يَنطِقُونَ ﴿٦٣﴾
 

59. Wakasema: Nani amefanya hivi kwa waabudiwa wetu? Hakika yeye ni miongoni mwa madhalimu.  60. Wakasema: Tulimsikia kijana akiwataja anaitwa Ibraahiym.  61. Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu ili wapate kushuhudia.  62. Wakasema: Je, ni wewe uliyefanya hivi kwa waabudiwa wetu, ee Ibraahiym?   63. Akasema: Hapana, bali amefanya hayo hili kubwa lao. Hivyo waulizeni wakiwa wanaweza kunena! [Al-Anbiyaa:59-63]

 

Wakajirudi kidogo kuwaza kwamba kweli walikuwa wanaabudu miungu isioweza hata kujikinga na madhara, lakini kuwaza kwao kulikuwa kwa muda mdogo, kisha wakarudi katika upotofu ule ule:

 

 فَرَجَعُوا إِلَىٰ أَنفُسِهِمْ فَقَالُوا إِنَّكُمْ أَنتُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٦٤﴾ثُمَّ نُكِسُوا عَلَىٰ رُءُوسِهِمْ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا هَـٰؤُلَاءِ يَنطِقُونَ ﴿٦٥﴾قَالَ أَفَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكُمْ شَيْئًا وَلَا يَضُرُّكُمْ ﴿٦٦﴾أُفٍّ لَّكُمْ وَلِمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٦٧﴾

64.  Basi wakajirudia nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi ndio madhalimu.   65. Kisha wakarudia hali yao ya mwanzo ya upotofu: (Wakasema): Umekwishajua kwamba hawa hawasemi.   66. (Ibraahiym) Akasema: Je, basi mnaabudu badala ya Allaah isiyokunufaisheni kitu chochote na wala kukudhuruni?   67. Aibu yenu nyinyi na vile mnavyoviabudu badala ya Allaah. Je, hamtii akilini?  [Al-Anbiyaa: 64-67]

 

Hii ndio ilikuwa sababu khaswa ya Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ya kuyavunja hayo masanamu ili wajiulize na watambue ujinga wao wa kuabudu vitu visivyosema na wala visivyoweza kujihifadhi na madhara.   

 

Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Anaingizwa Katika Moto:

 

Hapo tena ndipo walipotaka kumchoma moto:

 

قَالُوا حَرِّقُوهُ وَانصُرُوا آلِهَتَكُمْ إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ ﴿٦٨﴾

Wakasema: Muunguzeni na mnusuru waabudiwa wenu, mkiwa ni wafanyao (kunusuru). [Al-Anbiyaa:68]

 

Wakakusanya kuni nyingi kabisa za kuandaa moto mkubwa.  Wakachimba shimo na ukawashwa moto uliowaka kwa cheche kubwa, moto ambao haujapata kuwashwa moto kama huo kabla wakamtia Ibraahiym (‘alayhis- salaam). 

 

Yafuatayao ni maelezo mbali mbali kuhusu tukio hilo:

 

-Bwana mmoja Mkurdi aliyekuwa ni mhamajihamaji, ambaye ametokea Persia, alitoa rai kuwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) atiwe katika manati kubwa (chombo cha kurushia mawe) [Al-Qurtwubiy 11:303] 

 

-Shu'ayb Al-Jabaa'i kasema: (Bwana huyo) "Jina lake alikuwa ni Hayzan na kwa sababu ya rai yake hiyo aliyotoa, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kamjaalia kumezwa na ardhi na ataendelea kudidimia hadi siku ya Qiyaamah.

 

-Alipotumbukizwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) katika moto alisema:

حَسْبُنا اللَّه وَ نِعْم الْوَكِيل

Ananitosheleza Allaah na Yeye Ndiye Mbora wa kupanga mambo yangu [At-Twabariy 18:465]

 

-Inavyosemekana kuwa zilikusanywa kuni kwa muda wa mwezi na alipotupwa kwenye moto huo alikuja Jibriyl (‘alayhis-salaam) akasema: Ee Ibraahiym, una haja yoyote? Akajibu: Ama kwako la!

 

حَسْبِيَ اللَّه وَنِعْمَ الْوَكِيِل

Hasbiya-Allaah Wa Ni'mal-Wakiyl [Aysarut-Tafaasiyr – Abu-Bakkar Al-Jazaairiy 3:426]

 

-Kutokana na wingi wa kuni zilizokusanywa ilifika hadi watu kuweka nadhiri, ya kupeleka kuni. 

 

-As-Sudi kasema: "Mwanamke alipokuwa akiumwa akiweka nadhiri kuwa akipona ataleta kuni za kumuunguza Ibraahiym (‘alayhis-salaam). [Al-Qurtubiy 11:303]

 

-Kutokana na Hadiyth ifuatayo, baadhi ya Mufassiriyn wamesema kwamba fadhila hii ya kuwa Ibraahiym (‘alayhi-salaam) atakuwa ni mtu wa kwanza kuvishwa nguo, ni kwa sababu yakutiwa motoni bila ya sababu yoyote ya haki bali kwa kushikilia Tawhiyd na kukanusha shirk:   

 

عن ‏ ‏ابن عباس ‏ ‏رضي الله عنهما ‏ عن النبي ‏ ‏صلى   الله عليه وسلم ‏قال: ((إنكم محشورون  حفاة عراة غرلا ثم قرأ ((كما بدأنا أول خلق نعيده)) وأول من يكسى يوم القيامة  إبراهيم)) البخاري ومسلم

Imetoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

amesema: “Mtafufuliwa bila ya viatu, uchi nabila ya kutahiriwa (khitaan) kisha akasoma”: ((Kama Tulivyoanza umbo la awali tutalirudisha tena)) na wa kwanza kuvalishwa nguo siku ya Qiyaamah ni Ibraahiym)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

-Sa'iyd bin Jubayr karipoti kwamba Ibn 'Abbaas kasema:  "Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alipotupwa katika moto, Malaika wa mvua alisema: Lini nitaruhusiwa kuteremsha mvua?  Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alijibu haraka kama aya inavyosema:

 

قُلْنَا يَا نَارُ كُونِي بَرْدًا وَسَلَامًا عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ ﴿٦٩﴾

Tukasema: Ee moto! Kuwa baridi, na salama juu ya Ibraahiym! [Al-Anbiyaa: 69]

 

-Na kwa maneno hayo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hakuna moto uliokuwa ukiwaka duniani wakati huo ila ulizimwa [At-Twabariy 18:466]

 

-Ibn 'Abbaas na Abu Al-Aliyah kasema: "Ingelikuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hakusema (Hakuuambia moto): 

.. وَسَلَامًا ﴿٦٩﴾

Na salama

 

Basi Ibraahiym (‘alayhis-salaam) angelidhurika kwa ubaridi wake [At-Twabariy 18:466, 465]

 

-Qataadah amesema: "Siku hiyo hakikuweko kiumbe kisichojaribu kuuzima moto wa Ibraahiym (‘alayhi wa sallam) ila mjusi" [At-Twabariy 18:467].

 

-Az-Zuhriy kasema: "Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamrisha kuwa (mjusi) auliwe na akaitwa 'mnyama mharibifu' [At-Twabariy 18:467 na pia imesimuliwa katika Muslim Namba 2238]

 

Mbinu zao za kutaka kumuunguza Ibraahiym (‘alayhis-salaam) katika moto hazikufaulu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

وَأَرَادُوا بِهِ كَيْدًا فَجَعَلْنَاهُمُ الْأَخْسَرِينَ ﴿٧٠﴾

Na wakamkusudia njama; lakini Tukawajaalia wao ndio wenye kukhasirika.  [Al-Anbiyaa:70]

 

Moto ukamalizika kuwaka, watu wakiwa wanasubiri kwa hamu kubwa waone majivu tu, lakini dhana yao iliwashtua, na walitahayarika walipomuona Ibraahiym (‘alayhis-salaam) anatoka salama mbele ya macho yao akitembea mzima bila ya kudhurika popote.  Ni muujiza mkubwa hakika!

 

Lakini kama kawaida ya hali ya watu wa zamani walivyokuwa na ukaidi wao hawakumuamini Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na wito wake wa ibada ya Tawhiyd kwamba kuna Ilaah Apasaye kuabudiwa Pekee, Ambaye Alifanya maajabu haya ya Moto kutokumuunguza Ibraahiym (‘alayhis- salaam).

 

 

Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Anahama Iraq Kuelekea Shaam:

 

Hakuamini mtu isipokuwa Luutw (‘alayhis-salaam) ambaye alikuwa ni binamu (cousin) wake, na mke wake Saarah.  

 

فَآمَنَ لَهُ لُوطٌ ۘ وَقَالَ إِنِّي مُهَاجِرٌ إِلَىٰ رَبِّي ۖ إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٦﴾

 Basi Luutw akamwamini; na (Ibraahiym) akasema: Hakika mimi nahajiri kwa Rabb wangu; hakika Yeye Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al'Ankabuut: 26]

 

Vile vile akasema Ibraahiym (‘alayhis-salaam):

 

وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَىٰ رَبِّي سَيَهْدِينِ ﴿٩٩﴾رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٠٠﴾

99. Akasema: Hakika mimi ni mwenye kwenda kwa Rabb wangu Ataniongoza. 100. Rabb wangu!  Nitunukie miongoni mwa Swalihina. [As-Swaaffaat: 99-100]

Hapo tena Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamhamisha na kumpeleka Shaam nchi ambayo ndio iliyokusudiwa kuwa 'nchi Tulioibariki'.

 

وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ ﴿٧١﴾

Na Tukamuokoa na Luutw kuelekea ardhi ambayo Tumeibariki humo kwa walimwengu. [Al-Anbiyaa:71]

 

Na kutokana na Du'aa yake hiyo ya:

رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٠٠﴾

Rabb wangu!  Nitunukie miongoni mwa Swalihin. [As-Swaaffaat:100]

 

Allaah (Subhaanahu Allaahu wa Ta’aalaa) Akamjaaliya kupata watoto kama aya zifuatazo zinavyotuelezea:

فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلَامٍ حَلِيمٍ ﴿١٠١﴾

Basi Tukambashiria ghulamu mvumilivu. [As-Swaaffaat:101] 

 

Aayah hii imekusudiwa ni Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam)

 

Na katika Aayah nyingine Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ نَافِلَةً ۖ وَكُلًّا جَعَلْنَا صَالِحِينَ ﴿٧٢﴾

Na Tukamtunukia Is-haaq na (mjukuu) Ya’quwb kuwa ni ziada. Na wote Tumewajaalia kuwa Swalihina. [Al-Anbiyaa:72]

 

'Atwaa' na Mujaahid wamesema:  "Naafilatan (Na ziada) ina maana kwamba zawadi" [At-Twabariy 18:471]

 

Ibn 'Abbaas na Qataadah wamesema: "Zawadi ya mtoto mwenye mtoto, maana kwamba Ya'quwb alikuwa mtoto wa Is-haaq kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)

.. فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَاقَ وَمِن وَرَاءِ إِسْحَاقَ يَعْقُوبَ﴿٧١﴾

..Tukambashiria Is-haaq na baada ya Is-haaq ni Ya’quwb. [Huwd:71]

 

 

.../3

 

 

Share