Wapi Ilipo Jannah (Pepo) Na Wapi Ilipo Jahannam (Moto)?

 

 

Wapi Ilipo  Jannah (Pepo) Na Wapi Ilipo Jahannam (Moto)?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Kuna ufafanuzi ulio wazi zaidi juu ya uwepo wa jahannam chini ya ardhi ya saba?

Baaraka Allaahu fiyk

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Wanachuoni wameeleza kuwa Jannah iko juu ya mbingu ya saba na Moto wa Jahannam ni chini kabisa ya ardhi.

 

Kuna riwaaya lakini si sahihi kutoka kwa Al-Bayhaqiy isemayo kuwa Jannah iko juu katika mbingu ya saba na Moto wa Jahannam ni katika ardhi ya saba chini.

 

Lakini kuna riwaaya ya Al-Haakim ambayo yeye kaisema ni sahihi na baadhi ya Maimaam wameiona ni sahihi inasema Jannah iko mbinguni na Moto wa Jahannam uko chini ya ardhi.

 

Hakuna shaka katika riwaaya za kuhusu Jannah kuwa ipo juu. Kama ilivyo hapa chini.

 

Jannah ipo juu ya mbingu saba chini ya 'Arsh. Kama Hadiyth inayozungumzia Jannah ya Al-Firdaws iliyopo kwenye Al-Bukhaariy ambapo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Mnapomuomba Allaah Jannah (Pepo) Muombeni (Jannah) ya Al-Firdaws kwani (Jannah hiyo) ni ya kati na kati na ndani yake inatiririka mito, juu yake kuna Arshi ya Ar-Rahmaan."

[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Vilevile Abuu Hurayrah amesimuliwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Kuna daraja mia moja za Jannah ambazo Amezitayarisha Allaah kwa ajili ya Mujaahidiyn wanaopigana kwa ajili Yake. Baina ya sehemu moja na sehemu nyingine, ni masafa sawa ya baina ya ardhi na mbingu. Unapomuomba Allaah, 'Azza Wa Jalla, muombe Al-Firdaws, kwa sababu ipo katikati ya Jannah na ni sehemu ya Juu kabisa ambamo mito ya Jannah inapita, na juu yake kuna ‘Arsh ya Mola Mtukufu".  [Imaam Al-Bukhaariy, Ahmad na wengineo]

 

 

Kuhusu Jahannam, amesema Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) kuwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kasema:

 

"Jannah iko juu ya mbingu saba na Jahannam iko chini ya ardhi saba.

 

Pia kuna riwaaya nyingine iliyosimuliwa na Ibn Mandah  (Rahimahu Allaah) kuwa Mujaahid  (Rahimahu Allaah) kasema:

 

"Nilimuuliza Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu): "Wapi ilipo Jannah?" Akajibu: "Juu ya mbingu saba." Nikamuuliza: "Wapi ilipo Jahannam?" Akajibu: "Chini ya bahari saba, moja juu ya nyingine."

 

Na kadhaalika Ibn Abiy Dunyaa (Rahimahu Allaah) amesimulia kwa mapokezi kuwa Qataadah (Rahimahu Allaah) alikuwa akisema kuwa walikuwa wanasema (wanaelewa) kuwa Jannah iko juu ya mbingu saba na Moto  uko chini ya ardhi saba.

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aliulizwa wapi ilipo Jannah na Jahannam?

 

Akajibu:

 

"Jannah iko juu ya 'Illiyyiyn na Moto wa Jahannam uko katika Sijjiyn, na As-Sijjiyn ni chini kabisa ya ardhi. Kama isemavyo Hadiyth:

 

"Anapokufa mtu, Allaah Ta'aalaa, Anasema: "Kirekodi kitabu cha mja Wangu katika Sijjiyn chini kabisa ya ardhi."

 

Ama Jannah iko juu, juu kabisa ya 'Illiyyiyn.

 

Na imethibiti kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

 

"'Arsh ya Rabb, Aliyetukuka Aliye juu, ni sakafu ya Jannah ya Al-Firdaws."

 

[Fataawa Nuwr ‘Alaa Ad-Darb (4/2)]

 

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn Ibn (Rahimahu Allaah) amesema katika fatwa nyingine kuwa Hadiyth zilizosimuliwa kuhusu ilipo Jahannam ni dhaifu kwa hiyo haziwezi kutumika kama ushahidi lakini ameeleza kuwa kutokana na Aayah na wafasiri na wema waliotangulia kama kina Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) na wengine, inaonesha kuwa Jahannam iko ardhini.

 

Anaendelea kusema kuwa, sehemu iliyopo Jahannam ni ardhini, lakini baadhi ya Wanachuoni wamesema kuwa ipo kwenye bahari na wengine wamesema iko katikati ya ardhi. Lakini kinachodhihirika ni kuwa (Jahannam) iko ardhini, lakini hatujui wapi haswa ilipo katika ardhi.

 

Akasema, ushahidi wa Aayah kwamba Jahannam ipo ardhini ni kauli ya Allaah Ta'aalaa:

 

"كَلَّا إِنَّ كِتَابَ الْفُجَّارِ لَفِي سِجِّينٍ ﴿٧﴾

 

"Laa hasha! Hakika kitabu cha watendaji dhambi bila shaka kimo katika Sijjiyn."

[Al-Mutwaffifiyn: 7]

 

Sijjiyn ni chini kabisa ya ardhi, na Jahannam (ndipo ilipo) chini ya ardhi.

 

Mwisho wa kumnukuu Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah).

 

[Ash-Sharh Al-Mumti', mj. 3, uk. 174-175]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share