Aingie Wapi Katika Ihraam Akiwa Anasafiri Kutoka Uingereza?

 

Aingie Wapi Katika Ihraam Akiwa Anasafiri Kutoka Uingereza?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

In shaa Allaah Salaama. Nilikuwa na sualla kuhusu kituo cha ihram kutoka England. Wapi tutasimama kuvaa ihram kabla ya kwenda hajj? ama inaruhusiwa kuvaa ihram ndani ya ndege? Shukran, Jazakallahu kheir. Wasalam Alaikum Warahmatulah Wabarakatuh.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mwanzo ni muhimu tufahamu kuwa kwa sababu ya kutofautiana katika usafiri ni bora mtu avae Ihraam yake kutoka nyumbani kwake ikiwa anakwenda kupanda ndege. Huwa watu wengi wanapata shida kubwa sana kuanza kutoa Ihraam zao wakiwa katika ndege na kuanza kuvaa katika hali ya dhiki. Kuvaa nyumbani ni bora kwani litakalobakia ni kutia nia tu wakati unafika katika Miqati (Miyqaat).

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuekea Miqati tano kwa watu wanaotoka sehemu tofauti nje ya Makkah. Katika hizo ni ule usemi wake  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa:

 

"Miqati kwa watu wa Madiynah ni Dhul Hulayfah, watu wa Shaam ni al-Juhfah, watu wa Najd ni Qarn al-Manaazil na kwa watu wa Yemen ni Yalamlam" [al-Bukhaariy na Muslim].

Na pia: "Dhaat 'Irq kwa watu wa Iraq" [Muslim].

 

Dhul Hulayfah, nayo kwa sasa inaitwa Aabar 'Aliy ipo kaskazini mwa Makkah, takriban kilomita 450, ama Juhfah, ambayo iko karibu na Raaghib ipo Kaskazini Magharibi mwa Makkah takriban kilomita 187. Juhfah pia ni Miqati kwa walio Misri na Morocco. Qarn al-Manaazil, kwa sasa inajulikana kama Waadiy as-Sayl, sehemu ambayo ipo mashariki mwa Makkah ambayo ina umbali wa kilomita 94 kutoka Makkah. Na Dhaat 'Irq ipo Kaskazini mashariki ya Makkah.

 

Ikiwa nchi unayotoka haipo katika orodha (qaima) iliyopo hapo juu utakuwa ni mwenye kuulizia kabla ya kuondoka nchini mwako kuhusu mapitio ya ndege katika safari hiyo. Ikiwa ndege inapitia katika Miqati yoyote iliyotajwa au karibu na hapo pindi itakapofika utatia nia yako ya ‘Umrah au Hajj. Kwa siku hizi mambo yamekuwa rahisi kwani marubani na wahudumu wa ndege hasa ikiwa ni za kuwapeleka watu Hajj au umekwenda na kundi utakuwa ni mwenye kufahamishwa nawe utakuwa unaona vile ndege inavyokwenda kwa ramani inayonyeshwa ndani ya ndege.

 

Kulingana na Miqati tulizotaja na walio na Miqati hizo inaonyesha Miqati ya watu kutoka Uingereza ni Juhfah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share