Mke Afanyeje Ikiwa Mumewe Hana Uzazi

 

SWALI:

 

Assalam Aleykum,

 

Mimi ni mpenzi wa website hii.  Huwa najifunza mambo mengi humu.

 

Nimesoma kuhusu matatizo ambayo yanamfanya mwanaume aruhusiwe kuoa mke wa pili n.k. kwa kuwa ndio solution inayoonekana bora zaidi. Napenda kuuliza je kama inakuwa kwa upande wa pili inakuwaje?  Mfano; mume ndo ana tatizo ndani ya nyumba mke anatakiwa kufanyaje?   Yani kama tu hayo matatizo atakayokayo kuwa nayo mwanamke pia wanaume wanayo. Je mume akiwa hazai na mimi nahitaji watoto natakiwa kufanyaje?

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu mume kutokuwa na uzazi, mke afanyeje?

 

Hakika ni kuwa kama vile mwanamke anavyokuwa hawezi kuzaa mume naye pia anaweza kuwa na tatizo hilo. Hilo ni tatizo linalomkumba mwanamke na mwanamme sawasawa.

 

Tatizo hilo ni mitihani Anayoitoa Allaah kumjaribu nayo mja Wake.

 

Hata hivyo, si vibaya kutafuta tiba kwani kuna waliokuwa na tatizo hilo wakapatiwa tiba hususan wale wenye matatizo kwenye sehemu zao za uzazi.

 

Hakika ni kuwa Uislamu, umetoa suluhisho kwa kila tatizo. Bila shaka, mke akiwa na tatizo hilo mume anatakiwa amvumilie mkewe kwa makidhio hayo ya Allaah kwao, na ikishindikana basi anaweza kuoa lakini akabaki na mke wake wa kwanza asiyeweza kuzaa. Hata hivyo, anaweza kuoa na akakutana na tatizo kama hilo kwa mke mwengine, kwa huko kuoa mke mwengine si dhamana ya kupata mtoto ingawa sheria haimkatazi kuoa mke mwengine.

 

Ikiwa tatizo hilo analo mwanamme, mwanamke atamvumilia kwa muda huku mume anatafuta ufumbuzi na matibabu. Ikiwa muda umepita mwingi hadi mke kukosa utulivu anaweza kuzungumza na mumewe ili amuache au ikiwa hataki basi anaweza kwenda kwa Qaadhi na shitaka hilo. Na ndoa hiyo inaweza kuvunjwa. Ama ikiwa mke anaona anaweza kuishi na mume huyo asiyezaa itakuwa ni uamuzi wake na bora kwake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share