Hajj Ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

 

Hajj Ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

(Kama Ilivyohadithiwa Na Jaabir Bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

 

Imetafsiriwa Na: Muhammad Faraj Saalim As-Sa’ay (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Anasema Imaam Muslim:

 

“Nimehadithiwa na Abu Bakr bin Abi Shaybah na Is-haaq bin Ibraahiym, wote pamoja. Na kutoka kwa Haatim amesema kuwa Abu Bakr amesema:

 

'Nimehadithiwa na Haatim bin Ismaa’iyl Al-Madaniy, kutoka kwa Ja’afar bin Muhammad, kutoka kwa baba yake (Radhiya Allaahu ‘anhum) kuwa alisema:

 

“Tulimwendea Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu), akaanza kutuuliza majina yetu mmoja mmoja mpaka akaishia kwangu. Nikamwambia:

 

'Mimi ni Muhammad bin Aliy bin Husayn”. Akakivamia kichwa changu, kisha akanifungua kifungo changu cha juu kisha cha chini yake, kisha akauweka mkono wake kifuani pangu, na wakati huo nilikuwa bado kijana. Akaniambia;

“Marhaban (karibu) ewe mwana wa ndugu yangu. Uliza unalotaka kuuliza”.

 

Nikamuuliza, na wakati ule alikuwa kipofu, na wakati wa Swalah ulipowadia aliinuka huku akiikusanyakusanya nguo yake, kila akijifunika nayo upande mmoja wa bega lake, upande wa pili inaanguka kwa sababu ya udogo wake.

Akatuswalisha, kisha nikamwambia:

 

“Tuhadithie juu ya Hajj ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)”

 

Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

“Watu walipoarifiwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) atahiji mwaka huu, walianza kumiminika mjini Madiynah kwa wingi sana, kila mmoja akitamani aongozwe na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na afanye kama atakavyofanya.

 

(Ilipowadia siku ya safari) Tukaondoka naye mpaka tulipowasili Dhul Hulayfah (Abaar ‘Aliy - mikati ya watu wa Madiynah), Asmaa bint Umays akamzaa Muhammad bin Abi Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu), akamtuma mtu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kumuuliza nini afanye. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:

 

“Oga, kisha weka kitambaa na utie nia ya Ihram (niyyah ya kuhiji)”.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaswali Msikitini kisha akampanda ngamia wake anayejulikana kwa jina la Al-Qaswaa, na alipokuwa katikati ya jangwa nikainua kichwa changu kutizama waliokuwa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), nikaona watu wengi sana, upeo wa macho yangu wakiwemo waliopanda wanyama na wanaokwenda kwa miguu, kisha nikatazama kuliani kwake, nikaona hivyo hivyo, kisha upande wake wa kushoto nikaona hivyo hivyo, na nyuma yake hivyo hivyo, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa pamoja nasi huku wahyi ukimteremkia, huku akituhadithia, na kila anachokifanya, sisi tulikuwa tukimfuata.

Kisha akaanza kusema:

 

“Labbayka Allahumma labbayka, labbayka laa shariyka laka labbayka. Innal hamda wa n’imata laka wal mulk, laa shariyka laka”.

 

Na watu wakawa wanasema kama anavyosema”.

 

Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaendelea kusema:

 

“Hatukuwa tukitia niyyah nyingine isipokuwa nia ya Hajj, (hatukuwa tukijua aina nyingine za Hajj), hatukuwa tukijua juu ya ‘‘Umrah. Tukaendelea na Safari mpaka tulipoifikia Al-Ka’abah tukiwa pamoja naye, akaligusa jiwe jeusi kisha akaanza kutufu. Katika mizunguko mitatu ya mwanzo alikuwa akenda kwa kukazana, na katika minne iliyobaki akenda mwendo wa kawaida. Alipomaliza akaenda penye Maqaamu Ibraahiym ('Alayhis Salaam), akasoma:

 

وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى ۖ 

Na chukueni kutoka mahali pa kusimama Ibraahiym kuwa ni pahala pa kuswalia.”

[Al-Baqarah: 125]

 

Akaelekea Qiblah na kuswali rakaa mbili mahali hapo, akasoma katika rakaa ya mwanzo (Alhamdu pamoja na) Qul yaa ayyuhal kaafiruun na katika rakaa ya pili akasoma (Alhamdu pamoja na) Qul Huwa Allaahu Ahad, kisha akarudi penye jiwe jeusi, akaligusa kisha akatokea mlangoni kuelekea Swafaa.

 

Alipokaribia Swafaa akasoma:

 

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ 

 

“Hakika Swafaa na Marwah (Majabali mawili yanayofanyiwa ibada ya Saa'yi huko Makkah) ni katika alama za kuadhimisha Dini ya Allaah

 

Abdau bimaa bada-a Allaahu bihi”

 

  Naanzia pale alipoanzia Allaah.

 

Akaanzia Swafaa, akaupanda mlima huo mpaka alipoweza kuiona Al-Ka'bah akaelekea Qiblah akasema:

 

“Laa ilaha illa Allaah - Allahu Akbar”

,

Kisha akasema:

 

“La Ilaaha Illa Allaah, Wahdahu La shariyka Lahu, Lahul Mulku wa Lahul Hamdu, wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr. La Ilaaha Illa Allaah, Wahdahu, Anjaza wa’adahu, wa Naswara ‘abdahu, wa Hazamal ahzaaba Wahdah”.

 

Kisha akaomba du’aa, kisha akarudia kusema hivyo mara tatu, kisha akashuka kuelekea Marwah, alipofika katikati ya bonde akawa anakwenda mwendo wa kukazana, na alipolifikia jabali la Marwah akalipanda kwa mwendo wa kawaida, na alipolifika juu yake akasoma na kufanya kama alivyofanya alipokuwa juu ya Swafaa.

 

Akaendelea hivyo mpaka twawafu yake ilipomalizikia Marwah akasema:

“Lau kama amri niliyopewa (hivi sasa) ningelipewa kabla, nisingechukuwa pamoja nami mnyama na ningeijaalia (twawafu yangu na sa’ayi yangu) kuwa ‘Umrah, na kama yupo kati yenu asiyekuwa na mnyama basi avue nguo za Ihraam na aijaalie iwe ‘Umrah”.

 

Akainuka Suraaka bin Maalik bin Ja’athum (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:

“Ee Mtume wa Allaah, (hukmu hii) ni kwa ajili ya mwaka huu tu au milele?”

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaviingiza vidole vyake vya mkono wa kulia ndani ya vidole vya mkono wa kushoto na kusema:

 

“Umrah na Hajj zishaingiliana” akasema hivyo mara mbili, kisha akasema; “Laa, bali milele”.

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawasili kutoka nchi ya Yemen akiwa na ngamia wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), akamkuta Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) amekwishavuwa nguo za Ihraam na kuvaa nguo za kawaida za rangi rangi na ametia wanja. Akamkataza, kwa ajili hiyo, lakini Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) akamwambia:

 

“Baba yangu ameniamrisha kufanya hivi”.

 

Akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kumshtaki Faatwimah kwa vile alivyofanya (kuvua nguo za Ihraam na kupaka wanja) na kwa kule kusema kwake kuwa Baba yake ndiye aliyemuambia, akamjulisha kuwa yeye alimkataza kwa kufanya kwake vile.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamjibu:

 

“Ni kweli, (na) wewe umetia niyyah gani ya kuhiji ulipokuwa unakuja?”

Akasema:

 

“Nilisema; 'Allahumma mimi natia niyyah ile ile aliotia Mtume wako”.

Akamwambia:

 

“Basi mimi ninaye mnyama, kwa hivyo tusivuwe (nguo za Ihraam)”.

 

Idadi ya wanyama aliokuja nao ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutoka Yemen ikichanganywa na idadi ya wanyama aliokuja nao Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ikafikia ngamia mia moja.

 

 

Watu wote wakavua Ihraam zao na kukata nywele isipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na wachache waliokuja na wanyama wao.

 

Ilipofika siku ya Tarwiyah - siku ya tarehe 8 Dhul Hajj, watu wakaondoka kuelekea Minaa wakitia niyyah ya Hajj, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akampanda mnyama wake na kuelekea huko pamoja nao. (Walipowasili Minaa), wakaswali Adhuhuri, Al-'aswr, Maghrib, ‘Ishaa na Al-Fajir (Qaswran, kila Swalah katika wakati wake).

 

(Baada ya kuswali Al-fajir) Akasubiri kidogo mpaka jua lilipochomoza akaamrisha lisimamishwe hema mahali paitwapo Namirah, - karibu na ‘Arafah -. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaondoka kuelekea Namirah na akapitiliza Muzdalifah bila ya kusimama penye Mash’arul Haraam, juu ya kuwa Ma-Quraysh walidhania atasimama hapo kama walivyokuwa wakifanya wakati wa Ujahilia.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakusimama mpaka alipowasili Arafat, akaliona hema lishasimamishwa pale Namirah kama alivyoamrisha, akashuka na kupumzika hapo mpaka ulipoingia wakati wa Adhuhuri, akaamrisha aletwe ngamia wake Al-Qaswaa, akampanda na kwenda moja kwa moja mpaka alipofika katikati ya bonde la ‘Arafah akasimama na kuwahutubia watu akasema:

 

“Hakika ya damu zenu na mali zenu (ni tukufu sana kwa hivyo) ni haramu baina yenu (kumwaga damu zenu na kudhulumiana baina yenu) kama ulivyokuwa utukufu wa siku yenu hii, katika mwezi wenu huu, katika mji wenu huu, visasi vyenu vyote vya wakati wa ujahilia viko chini ya mguu wangu - nishavibatilisha - na kisasi cha mwanzo cha kumwaga damu yetu ninachokibatilisha ni kisasi cha (kumwaga) damu ya Ibn Rabi’ah bin Al-Haarith - alikuwa na mtoto anayenyonyeshwa katika kabila la Bani Sa’ad,akauliwa na watu wa kabila la Hudhayl - Na ribaa iliyokuwa ikichukuliwa wakati wa Ujahilia ishabatilika, na ribaa ya mwanzo ninayoibatilisha ni ribaa yetu, ribaa ya ‘Abbaas bin ‘Abdil Muttwalib, ishabatilika yote, na muogopeni Allaah katika wake zenu, kwani nyinyi mumewachukuwa kwa dhamana ya Allaah, na mkahalalishiwa tupu zao kwa neno la Allaah, na nyinyi mna haki zenu juu yao. Wasiwaingize nyumbani kwenu yeyote msiyempenda (awe mwanamume au mwanamke), na wakifanya hivyo, mnayo haki ya kuwapiga kipigo kisichoumiza. Na haki yao juu yenu ni kuwalisha na kuwavisha kwa wema. Na nimekuwachieni ambayo hamtopotea baada yake ikiwa mtashikamana nayo, Kitabu cha Allaah. Mkiulizwa juu yangu mtasema nini?”

 

Wakasema:

 

“Tutashuhudia kuwa umefikisha na umekamilisha na umenasihi.”

Akanyanyua kidole cha shahada akawa mara anakielekeza mbinguni mara anakielekeza kwa watu, akasema:

 

“Mola wangu shuhudia - (mara tatu)”.

 

Kisha akaadhini, akakimu na kuswali Swalah ya Adhuhuri, kisha akaqimu tena na kuswali Swalah ya Alasiri bila kuswali Sunnah baina yao. Kisha akampanda ngamia wake na kuelekea naye moja kwa moja mpaka mahali pa kusimama (katika uwanja wa Arafah), akamuelekeza ngamia wake Al-Qaswaa penye majabali na yeye akaelekea Qiblah.

 

Akasimama mahali hapo mpaka wakati wa Maghribi ulipoingia na umanjano wa jua kutoweka na juwa kuzama kabisa, ndipo alipoondoka akiwa amempakia Usaamah nyuma yake.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akampanda ngamia wake Al-Qaswaa na kuianza safari ya kwenda Muzdalifah. Akawa anazikaza kamba za hatamu za ngamia wake na kumbana nazo ili asiweze kwenda mbio kwa ajili ya zahma ya watu. Akawa anaashiria watu kwa mkono wake wa kulia huku akiwaambia:

“Enyi watu! (nendeni kwa) utulivu (nendeni kwa) utulivu.”

 

Na kila anapolifikia jabali akawa anailegeza kamba ili mnyama wake aweze kupanda kwa wepesi. Akawa anafanya hivyo mpaka alipowasili Muzdalifah, akaswali hapo Swalah ya Maghribi na ‘Ishaa kwa Adhana moja na Iqaamah mbili, bila ya kusabbih baina ya Swalah hizo.

 

Kisha Mtume wa Allaah akapumzika mahala hapo mpaka Alfajiri ilipoingia, akaswali Alfajiri pale ilipombainikia kuwa wakati wa Swalah ya Alfajiri ushaingia, kwa Adhaana na Iqaamah.

 

Kisha akampanda Al-Qaswaa mpaka alipowasili Masha’arul Haraam - (jabali lililopo hapo hapo Muzdalifah), akaelekea Qiblah na kuomba du’aa huku akikabbir na kumtukuza na kumpwekesha Allaah. Akawa katika hali hiyo mpaka kulipopambazuka.

 

Kisha akaondoka na kuianza safari ya kuelekea Minaa kabla ya jua kupanda akiwa amempakia Al-Fadhwl bin ‘Abbaas aliyekuwa kijana mwenye nywele nzuri, mweupe, na mwenye sura nzuri. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa akiondoka naye, akapita mbele yao ngamia aliyebeba wanawake wawili, na Al-Fadhwl akawa anawaangalia wanawake hao. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akauweka mkono wake usoni pa Al-Fadhwl ili asiweze kuwatazama, lakini Al-Fadhwl aliugeuza uso wake upande wa pili na kuendelea kuwatazama, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaukamata uso wa Al-Fadhl na kuugeuza upande mwingine. Akaendelea na safari yake mpaka alipolifikia bonde la Muhsir akaongeza mwendo kidogo, kisha akapita njia ya kati inayopeleka moja kwa moja mpaka penye Jamaraat kubwa (nguzo watu wanaporusha vijiwe vidogo), na alipolifikia Jamarah (hilo) lililokuwa karibu na mti akalipiga kwa vijiwe saba huku akikabbir kila anaporusha jiwe.

 

Kisha akaondoka kuelekea mahali pa kuchinja, akachinja (ngamia) sitini na tatu kwa mkono wake, kisha akampa ‘Aliy achinje waliobaki, kisha akaamrisha nyama ikatwe katwe, ikatiwa ndani ya vyungu vya kupikia, ikapikwa, wakala katika nyama ile na kunywa supu yake.

 

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akampanda ngamia wake na kuelekea penye Al-Ka’abah, akaswali Adhuhuri alipowasili Makkah.

 

Baada ya kuswali akawaendea watu wa kabila la Bani ‘Abd-l Muttwalib waliokuwa na jukumu la kuwahudumia watu katika kunywa maji ya Zamzam, akawaambia:

 

“Wanywesheni maji enyi watu wa kabila la Bani ‘Abdil Muttwalib, ingekuwa sikuogopeeni watu kukuchukulieni kazi hii ya kunywesha maji, basi ningelikusaidieni.”

 

Wakampa maji (ya Zamzam), akanywa.

 

 

 

Share