Mke Wake Ana Ukimwi Je Aendelee Kuishi Naye?
Mke Wake Ana Ukimwi Je Aendelee Kuishi Naye?
SWALI:
Nimewahi kuuliza lakini sikupata jibu niswali ligumu na ninapendelea kupata jibu, ni mtu anaishi na mkee wake alafu mkee wake kapata ujauzito alafu mkee kapimwa kakutana ana umwa ukimwi na mee ana sasa itakuwa vipi kuusu kuu ishi pamoja napendelea kupata jibu juu madocta wanasema kama munaweza kuishi pamoja na ukaendelea kumuingilia
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Katika Uislaam mwanamume anaruhusiwa kutoa talaka ikiwa mkewe ana maradhi hatari. Pia mke anaruhusiwa kuomba talaka ikiwa mumewe ana maradhi ya hatari kwa sababu Shariy’ah yetu ya Kiislaam haipendelei kusababishiana madhara kama ilivyothibiti katika Hadiyth:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ سَعْدِ بْنِ مَالِكِ بْنِ سِنَانٍ الْخُدْرِيّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه و سلم قَالَ: " لَا ضَرَرَ وَلَا ضِرَارَ"
Kutoka kwa Abu Sa’iyd bin Sa’d bin Maalik bin Sinaan Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Haifai kudhuru wala kulipana madhara” [Hadiyth Hasan iliyopokewa na Ibn Maajah, Maalik na ad-Daaraqutwniy]
Maradhi ambayo mwanamke anaruhusiwa kuomba talaka ni matano:
1-Uwendawazimu usiopona kabisa
2-Ukoma
3-Mbalanga
4-Mwanamume ambaye hawezi kufanya kabisa tendo la ndoa
5-Mwanamume mwenye ugonjwa wa pongwa (kukatika kipande sehemu ya uume wake)
Ikiwa mwanaume hana uwezo wa tendo la ndoa atapewa muda wa mwaka mmoja wa kujitibia ikishindikana mke anapewa khiyari ya kuchagua kati ya kubakia katika maisha ya ndoa yale au kuachana na maisha ya ndoa na mume yule.
Ama maradhi haya ya ukimwi pia mke au mume kila mmoja ana khiyari kati ya mambo mawili tuliyoyataja.
Kadhalika mume atakuwa na khiyari ya kutoa talaka ikiwa mkewe atakuwa na moja ya maradhi yafuatayo:
1-Uwenda wazimu usiopona
2-Ukoma
3-Mbalanga
4-Kuota nyama sehemu ya siri
5-Kuota kifupa sehemu ya siri ambayo humuondolea raha ya maisha ya tendo la ndoa pia humsababishia maumivu makali.
Hivyo chukulia kwa mfano huo kila ugonjwa ambao ni hatari katika maisha ya mwana-Aadam.
Na Allaah Anajua zaidi