Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Kusherehekea Siku Ya Mama ('Iydul-Ummi - Mother's Day)

 

Hukmu Ya Kusherehekea Siku Inayoitwa Sikukuu Ya Mama (Mother's Day)

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn  (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Nini hukmu ya kusherehekea inayoitwa Sikukuu ya mama?

 

 

JIBU:

 

Ikiwa ni ‘Iyd zinazokwenda kinyume na ‘Iyd za Shariy’ah, basi zote ni bid’ah mpya ambazo hazikuwa zikijulikana katika zama za Salafus-Swaalih Na huenda zikawa zimeanzishwa na wasio Waislamu pia, basi hio ni bid’ah za kuwaiga maadui wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Na ‘Iyd za ki-shariy’ah zinajulikana kwa Waislamu nazo ni ‘Iydul-Fitwr na ‘Iydul-Adhw-haa na ‘Iyd ya wiki nayo ni Ijumaa. Na hakuna katika Uislamu ‘Iyd nyinginezo isipokuwa ‘Iyd hizi tatu tu. Na kila ‘Iyd zinazozushwa zisizokuwa hizo ni za kurejeshewa na kutokubaliwa kwa mzushi wake, na ni batili katika Shariy’ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هَذَا مَا لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدٌّ

((Atakayezusha katika jambo letu hili (Dini yetu) basi litarudishwa.)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 

Yaani: Zinakanushwa na hazikubaliwi mbele ya Allaah. Na katika tamshi jengine:

مَنْ عَمِلَ عَمَلاً ليسَ عليه أمرُنا هذا فهو رَدٌ

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa katika jambo letu hili (Dini yetu) basi kitarudishwa.)) [Al-Bukhaariy] 

 

Na inapobainika hayo basi haijuzu kusherehekea 'Iyd iliyotajwa katika Swali,  inayoitwa "Sikukuu ya Mama (Siku ya Mama" au "Mother's day")". Haijuzu katika siku hiyo kuzusha chochote katika nembo za 'Iyd, kama vile, kudhihirisha furaha na kupeana zawadi na mfano wa hayo.

 

Na ni wajibu kwa Muislamu kujitukuza kwa Dini yake na kujifakharisha nayo na kutosheka na yale Aliyoyawekea mipaka Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Dini hii iliyonyooka ambayo Ameiridhia Allaah Aliyetukuka kwa waja Wake. Basi asizidishe ndani yake na wala asipunguze chochote (kilichokuja katika Dini).

 

Na yanayompasa Muislamu vilevile ni kuwa asiwe  mwenye kufuata kwa kuiga akifuata kila mwenye kupiga kelele, bali inampasa hali yake ya kiutu ni yenye kwenda na shariy'ah ya Allaah Aliyetukuka, hadi awe ni mwenye kufuatwa na si mwenye kufuata, na hadi awe ni kigezo na asiwe ni muigaji, kwani hakika shariy'ah ya Allaah -AlhamduliLLaah- ni kamili katika pande zote kama Alivyosema Allaah Aliyetukuka:

 

 

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ فَمَنِ اضْطُرَّ فِي مَخْمَصَةٍ غَيْرَ مُتَجَانِفٍ لِّإِثْمٍ ۙ فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣﴾

"Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislaam uwe Dini yenu. Basi atakayelazimika katika njaa kali bila kuinamia kwenye dhambi (akala vilivyoharamishwa) basi hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu." [Al-Maaidah: 03]

 

Na mama ana haki zaidi kuliko kusherehekewa kwa siku moja tu katika mwaka, bali mama ana haki kwa wanawe ambao wanapaswa kumlea, amwangalie, na asimamishe utiifu kwa yote isipokuwa yale ya kumuasi Allaah ('Azza wa Jalla) katika kila nyakati na kila mahali.

 

 

[Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-'Uthaymiyn, Mj. 16, Mlango wa Swalaah ya 'Iyd].

              

 

Share