Tunawakumbusha Kutamka Maneno Bora Kabisa Siku Ya ‘Arafah, Kuomba Maghfirah Na Kuepushwa Na Moto!

 

Tunawakumbusha Kutamka Maneno Bora Kabisa Siku Ya ‘Arafah

Pamoja Na Kumdhukuru Allaah Kwa Wingi, Na Kuomba Du'aa,

Kuomba Maghfirah Na Kumuomba Allaah Akuache Huru Kutokana Na Moto!

 

 Alhidaaya.com

 

Kwanza: Inapoingia Alfajiri ya Siku ya ‘Arafah, inapasa kutamka kwa wingi maneno yafuatayo ambayo ni maneno bora kabisa aliyoyatamka Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Manabii kabla yake kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((خَيْرُ الدُّعَاءِ دُعَاءُ يَوْمِ عَرَفَةَ، وخَيْرُ مَا قُلْتُ أنَا وَالنَّبيُّونَ مِنْ قَبْـلِي: لَا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيْكَ لَهُ، لَهُ الـمُلْكُ، ولَهُ الـحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَدِير)) روى الترمذي

“Du’aa bora kabisa ni du’aa katika siku ya 'Arafah, na (maneno) yaliyo bora kabisa niliyosema mimi na Manabii kabla yangu ni:

لَا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيْكَ لَهُ، لَهُ الـمُلْكُ، ولَهُ الـحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَدِير

Laa Ilaaha illa Allaah Wahdahu laa shariyka Lahu, Lahul-Mulku Walahul-Hamdu wa Huwa 'alaa kulli shay-in Qadiyr. 

 

Hapana mwabudiwa wa haki  ila Allaah, Pekee, Hana mshirika, Ufalme ni Wake, na Himdi zote ni Zake Naye juu ya kila kitu ni Muweza.  [At-Tirmidhiy]

 

Pili: Siku ya ‘Arafah ni Siku ambayo Allaah ('Azza wa Jalla) Huteremka duniani kwa uteremko unaolingana na Utukufu Wake na kuwaacha huru kwa wingi waja Wake kutokana na Moto kwa dalili:

 

 عنْ عَائِشَةَ أنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: "‏مَا مِنْ يَوْمٍ أَكْثَرَ مِنْ أَنْ يُعْتِقَ اللَّهُ فِيهِ عَبْدًا مِنَ النَّارِ مِنْ يَوْمِ عَرَفَةَ وَإِنَّهُ لَيَدْنُو ثُمَّ يُبَاهِي بِهِمُ الْمَلاَئِكَةَ فَيَقُولُ مَا أَرَادَ هَؤُلاَءِ"‏‏.‏

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna siku ambayo Allaah Anayoacha kwa wingi huru waja kutokana na Moto kama siku ya ‘Arafah.  Na huwa karibu kisha Anajigamba kwao kwa Malaika na Husema: Wametaka nini hawa? [Muslim]

Na katika Riwaayah nyingine:

اشْهَدُوا مَلاَئِكَتِي أَنِّي قَدْ غَفَرْتُ لَهُمْ. صحيح الترغيب

((“Shuhudieni Malaika wangu kwamba hakika Mimi Nimewaghufuria”)) [Swahiyh At-Targhiyb (1154)]

 

Tatu: Bakia katika 'ibaadah baada ya Swalaah ya Adhuhuri na khasa usikose baada ya Alasiri mpaka iingie Magharibi, kwa Haaj aliyejaaliwa kusimama ‘Arafah na kwa asiyejaaliwa kwenda Hajj. Lisikushughulishe jambo lolote jengine ila umdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) khasa kwa maneno hayo ya:

 

لَا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيْكَ لَهُ، لَهُ الـمُلْكُ، ولَهُ الـحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَدِير

na kumuomba maghfirah kwa wingi, kuomba du’aa na kuomba Allaah ('Azza wa Jalla) Akuache huru kutokana na Moto pamoja na wazazi wako na ahli zako, vizazi vyako, jamaa zako, nduguzo katika Iymaan na Akutaqabalie haja zako. Wakati huo ni muhimu kabisa katika Siku hiyo tukufu ya ‘Arafah kutokana na Hadiyth ifuatayo:

      

عن عبدالله بن عمرو إنَّ اللهَ عزَ وجلَّ يباهي ملائكتَهُ عشيةَ عرفةَ بأهلِ عرفةَ فيقولُ : انظروا إلى عبادي أتوني شُعثا غُبرا

((Hakika Allaah (‘Azza wa Jalla) Huwafakharisha watu ‘Arafah kwa Malaika Wake kuanzia mchana mpaka jioni ya ‘Arafah na Husema: “Watazameni waja Wangu wamenijia wakiwa timtimu wamejaa vumbi.”)) [Musnad Ahmad (12/42) na ameisahihisha Imaam Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb (1153), Swahiyh Al-Jaami’ (1868), Taz pia As-Silsilah Asw-Swahiyhah (1503)

 

Bonyeza hapa upate Takbira:

 

 

 

Share