Tahadhari Na Istihzai, Masikhara, Ambayo Ni Kukufuru!: Kufanya Vichekesho Suwrah Za Qur-aan
Tahadhari Na Istihzai, Masikhara, Ambayo Ni Kukufuru!
Kufanya Vichekesho Suwrah Za Qur-aan
Mfano: Suwrah Ya Al-Baqarah (Ng’ombe) Na Ya Al-Fiyl (Tembo)
Kuhadithia kisa cha kutunga, kwamba mtu alikwenda kuswali Msikiti mmoja ambao Imaam alikuwa anaswalisha Suwrah ya Al-Baqarah (Ng'ombe). Huyo mtu akachoka kusimama akaondoka zake. Kisha alipotaka kuswali Msikiti mwengine na alipojua kuwa Imaam anaswalisha kwa Suwrah ya Al-Fiyl (Tembo), akakimbia huku akisema: “Ikiwa Suwrah ya Al-Baqarah (Ng’ombe) ilikuwa ndefu mno, sasa hii ya Al-Fiyl (Tembo) itakuwaje?” Ikikusudiwa kuwa Suwrah ya Al-Fiyl (Tembo) itakuwa ni ndefu zaidi kuliko ya Al-Baqarah (Ng’ombe)!
Basi hii ni kufru na hatari, inaweza kumtoa mtu nje ya Uislamu kwa sababu kufanya istihzai (masikhara) katika yanayohusiana na Dini ya Allaah ni kukufuru!
Na dalili ni Aayah Alizoteremsha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwahusu watu waliofanya istihzai (masikhara) katika Dini wakadai kuwa walikuwa wanaporoja tu na kufanya mzaha. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ﴿٦٥﴾
Na ukiwauliza, bila shaka watasema: Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza. Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli Wake?
لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ
Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.
[Suwrah At-Tawbah (9:65-66)]