Akiokota Kitu Cha Thamani Njiani Je Ni Miliki Yake?

SWALI:

 

Assalam aleykum wa rahmatullah wa barakatuh,

 

Suala langu ni hili lifuatalo:-

 

Ikiwa mtu kaokota kitu njiani, madukani, ikiwa pesa, dhahabu, camera au kitu chochote kile, jee inaweza achukue au aulize kwanza?

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kiokotwa. Katika istilahi ya kisheria inaitwa Luqtwah (Kuokota). Hii ina maana ya kukuta kitu kilichoachwa katika sehemu isiyokuwa na mmiliki na hali hiyo ni kama kukuta mtu Muislamu kwenye njia yoyote pesa au nguo na akaogopea kupotea kitu hicho itabidi akiokote.

 

Sheria ya Kiislamu inaruhusu kuokota kilichoachwa kama alivyoulizwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye akajibu:

 

"Taja mfuko wake na kifuniko chake halafu ukitangaze mwaka mzima, akija mwenyewe atakichukuwa na kama hakutokea kitakuwa ni chako" (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Na aliulizwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ikiwa kitu kilichookotwa ni mbuzi/ kondoo, akasema:

 

"Mchukue kwani huyo ni wako au ni wa nduguyo au ni wa mbwa mwitu" (al-Bukhaariy, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

 

Zipo kanuni Fulani za suala hili, nazo ni kama zifuatazo:

  1. Kikiwa kitu kinachookotwa ni kitu duni ambacho hakina umuhimu wowote kwa watu kama vile tumba moja la tende, zabibu au kitambaa au bakora itakuwa si vibaya kukiokota na muokotaji atafaidika nacho wakati ule ule anapokiokota wala halazimiki kukitangaza na kukihifadhi. Na hilo ni kwa kauli ya Jaabir (Radhiya Allaahu 'anhuma): "Alituruhusu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika fimbo, bakora na kamba na mfano wa vitu hivyo mtu akiviokota afaidike navyo" (Abu Daawuud).

  2. Kikiwa kitu kilichookotwa ni chenye thamani katika jamii itampasa aliyeokota akitangaze mwaka mzima. Akitangaze kwenye milango ya Msikiti, sehemu za mkusanyiko wa watu au kupitia kwenye magazeti na Radio au vyombo vingine vya habari. Akija mwenyewe akakitaja kwa sifa zake, itabidi apewe na kama hakuja baada ya mwaka kamili atakitumia au atakitoa sadaka akitaka.

  3. Kiokotwa cha Makkah hakifai kuokotwa ila kitakapohofiwa kupotea. Na mwenye kukiokota itampasa akitangaze muda wa kuwa bado yuko Makkah na akitoka Makkah atakipeleka alichokiokota kwa kiongozi na wala si haki yake kukimiliki. Kwa kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mji wa Makkah ni haramu (mtukufu) hakiokotwi kitu.

  4. Kiokotwa aina ya mnyama kinaitwa mnyama aliyepotea akiwa porini inafaa kumuokota na kunufaika naye kuanzia wakati huo kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyo hapo juu. Na mfano wa ngamia aliyepotea, punda, nyumbu na farasi waliopotea huitwa 'wapuuzwa' kwani hairuhusiwi kuwaokota.

Tumejibu kwa kina kidogo ili ikusanye mambo mengi kuhusu kiokotwa. Ama kuhusu swali lako jawabu lake lipo wazi katika kipengele cha pili hapo juu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share