Mume Yuko Masomoni Mke Anamhudumia Pamoja Na Watoto, Mume Anataka Azae Na Mke Hataki Kwa kukhofia Gharama

SWALI:

 

Asalam Alaykum wa baady, Naomba kuchukua nafasi huu kumshkuru Allah Karim kwa kuniwezesha afya njema alhamdulilah.

Naomba kuuliza swali langu kama ifuatavyo, mimi ni msichana wa miaka 26 nimeolewa na alhamdulilah Allah ametujaalia binti wa miaka 4. Mume wangu kwa sasa ni mwanafunzi wa chuo, Kwa ujumla maisha ya familia yangu nayaendesha mimi mwenyewe kwa chakula, mavazi, kodi ya nyumba na wakati mwingine kumpatia pesa za matumizi na expense zote za maisha na hii ni kutokana na mume wangu hana kazi kwa sasa, Mume wangu anataka nizae tena sasa hivi, nimejaribu kumuelewesha japo amalize masomo yake kwani familia ninayohudumia mimi binafsi siimudu kisawasawa ila anakuwa mgumu sana kuelewa kiukweli maisha kwa kupande wangu ni magumu sana. Je kwa kumuomba mume wangu asubiri amalize ili anisaidie gharama za maisha ninapata dhambi?

na namuudhi Allah Karim  Naomba munijibu kwani tunamgogoro mkubwa kati yetu. Na Inshaalah Allah atawalipa kheri Amiyn

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kumsubirisha mumeo ili mupate muhula kabla ya kuzaa mtoto mwengine.

Hili ni jambo la kukaa pamoja na kulizungumzia kwa hali ya utulivu na umakini. Hakuna ubaya wowote kwa kupumzika kidogo kabla ya kupata mtoto mwengine japokuwa isiwe kufanya hivyo ni kwa khofu ya kukosa chakula kwani Allaah Aliyetukuka ndiye mwenye kuwaruzuku waja Wake.

 

Shauri lililo bora ni kuweza kumuelewesha kwa njia nzuri zaidi kwa unayoyaona wewe naye akakosa kuyazingatia au kuyaona.

Na Uislamu umeruhusu ‘azl (kumwaga nje) kama Hadiyth kadhaa zilizvyokuja kuhusiana na hilo. Jaribu kumuelewesha na huku unamuomba Allaah Aliyetukuka kwa dhati ili apate kulifahamu hilo na kulikubali.

 

Hata hivyo, haifai kwa hali yako kufunga uzazi kabisa maishani mwako, kwani kufanya hivyo ni dhambi.

 

Kadhalika msisitize na muhimize mume atafute kazi kwa bidii kwani haifai na haipendezi mume kulishwa na kuvishwa na kuhudumiwa watoto wake na mkewe. Jukumu hilo ni la mume na si la mke.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share