Mke/Mume Kutoa Siri Za Ndoa

 

SWALI:

NINI HUKUMU YA MWANAMKE ALIYE KATIKA UNYUMBA WAKE WA NDOA, AKACHUKUWA UAMUZI WA KUFUNGA MIZIGO YAKE NA KUMTOROKA MUMEWE BILA MAGOMVI WALA NINI?


 2. NI MAASI GANI YAFANYAYO DUA YA MUME DHIDI YA MKEWE ITAKABALIWE? AU YA MKE DHIDI YA MUMEWE ITAKABALIWE VILE VILE?


 3. NINI HUKUMU YA MUME AU YA MKE KUTOA SIRI ZA NDANI?
   
 NAOMBA NIPATE UFAFANUZI ZAIDI. JAZAKALLAAHU KHAIRAN

 



Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

1.    Kuhusu swali lako la kwanza tungependa kuwausia wanawake na pia wanaume kuwa matatizo ya unyumba yasiwe ni yenye kuchukuliwa kwa njia ya hasira na mmoja kufunga virago vyake au mwengine kumtoa mwenziwe. Hili ni tatizo ambalo limezagaa katika jamii yetu. Baadhi ya wanaume kuwafurusha wake zao kutoka katika majumba yao hata ikiwa ni usiku na baadhi ya wanawake kwa kosa dogo kufunga virago na kwenda zao sehemu wanayoiita ya kwao.

((لاَ تُخْرِجُوهُنَّ مِن بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ إِلَّا أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّهِ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ لَا تَدْرِي لَعَلَّ اللَّهَ يُحْدِثُ بَعْدَ ذَلِكَ أَمْرًا))

((Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Allaah, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Allaah, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Allaah Ataleta jambo jengine baada ya haya)) (65: 1).

Aya hii inatueleza jinsi gani mume hafai hata wakati ametoa talaka kumtoa mtalaka wake nyumbani wala mke yeye mwenyewe kutoka. Na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) hapa Ameziita hizo nyumba kuwa ni za mke japokuwa mume ndiye anayelipa ijara au nyumba yenyewe ni miliki ya mume. Mke anaweza kufukuzwa nyumbani tu ikiwa atafanya uchafu ulio wazi kabisa. Hivyo, ni makosa hasa kwa mke kutoroka nyumbani kwake bila magomvi yoyote. Kwani mke mwema ni yule ambaye anamtii mumewe na utiifu huu ni mkubwa na ni ‘Ibaadah na ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Lau ingekuwa ni mwenye kumuamuru yeyote kumsujudia mwengine basi ningemuamuru mwanamke kumsujudia mumewe” (At-Tirmidhiy).

Mwanamke kama huyo atakuwa katika uasi na madhambi mpaka atakaporudi kwa mumewe. Na ikiwa kutakuwa na ugomvi wa aina yoyote baina yao itakuwa ni muhimu kusuluhisha baina yao kwa njia ambayo italeta maridhiano na uwiyano ili wakae kwa wema na uzuri na waweze kusaidiana katika kulea watoto kwa njia ambayo ni nzuri. Uislamu umeweka njia ya utatuzi wa matatizo yoyote baina ya wanandoa; kupeana mawaidha, kushauriana baina yao, kuwaleta wazazi wa pande zote mbili ili kusuluhisha mzozo wowote na njia zozote nyinginezo ambazo zinakubalika kisheria ili kurudisha ufanisi baina yao.

2.     Hayo ni maasi ya dhulma, kwani dhulma ni kitu kibaya sana. Na dhulma sio tu baina ya mume na mke hata unapomdhulumu mtu yeyote naye akanyanyua mikono yake kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) basi hairudi patupu, Anamjibu mtu huyo. Sasa dhulma ikiwa baina ya watu wawili ambao wana mafungamano ya kindoa au uhusiano mwengine wowote basi inakuwa ni wepesi zaidi kujibiwa. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dua ya mwenye kudhulumiwa haina kizuizi baina yake na Allaah” (Maalik).

Na katika Hadiyth nyengine, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dua za watu watatu hazirudi: Mwenye kufunga mpaka anapofungua, kiongozi mwadilifu na mtu anayedhulumiwa” (At-Tirmidhiy).

Hivyo, ni nasaha kwetu kwa wanandoa waishi vizuri kwa kuelewana na kupeana na nasaha wala wasiwe ni wenye kudhulumiana kwa njia yoyote ile. Na katika Hadiyth nyengine kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya kwa kusema: “Ogopeni dhulma, kwani itakuwa (kwa mwenye kuifanya) ni giza Siku ya Kiyama” (Muslim).

3.     Qur’an inawasifu wanawake wema, ambao sifa ya wema wao ni kama ifuatayo:

((فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللّهُ))

((Basi wanawake wema ni wale wenye kutii na wanao jilinda hata katika siri kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajilinde)) ().

Miongoni mwa siri ambazo zinafaa kufichwa ni mahusiano ya kimwili na ya kindani baina ya mume na mke. Ni makosa kutoa au kuelezea siri hizo katika vikao au kuwafahamisha hayo jamaa wa mbali au wa karibu na marafiki zako. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Wale ambao watakuwa na daraja ya chini kabisa mbele ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Siku ya Kiyama ni wale ambao anastarehe (kimwili) na mkewe, naye (mke) na mumewe, kisha akaeneza siri zake hizo” (Ahmad, Abu Dawud na al-Bazzaar).

Na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu anhu) anahadithia: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituswalisha na alipomaliza alizunguka nyuma kututazama na kusema: “Kaeni chini. Je, yupo yeyote miongoni mwenu anayekuja kwa mkewe, akafunga mlango wake, na kuteremsha pazia, na baada ya hapo (akiwa) nje husema: ‘Mimi nimefanya kadha na kadha na mke wangu’” Watu wote walinyamaza. Kisha aligeuka kwa wanawake na kuuliza: “Je, wapo miongoni mwenu wanaofanya hivyo?” Msichana mmoja alijinyanyua kwa magoti yake ili Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amuone na apate kumsikiliza atakayoyasema. Alisema: “Ndio, WAllaahi! Wanaume wanazungumza kuhusu hilo na wanawake nao pia”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Je, mnajua wale wanaofanya hivyo wako wapi? Wanaofanya hivyo ni kama mfano wa shetani mwanamme na mwanamke wanaokutana barabarani na kujitosheleza uchu wao wa kimwili wakiwa wanatazamwa na watu (hadharani)” (Abu Dawud, at-Tirmidhiy, an-Nasaai na Ibn Maajah).

Kwa hakika huu ni mfano mbaya sana wa kufananishwa na shetani. Hivyo hili ni onyo kali kwa wenye tabia hiyo waiache ili wasiwekwe katika daraja ya chini Siku ya Kiyama wala wasifanane na mashetani. Jamii zinavunjika kwa tabia hii ambayo imezagaa katika vigaro na mabaraza yetu kwa kuzungumzia mas-ala nyeti na ya ndani kama haya.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

Share