Mke Wangu Kutwa Kwenye TV Hapendi Kusikiliza Mawaidha

SWALI:

Mke wangu kashuhulishwa sana na TV,

Mimi na mke wangu sote ni waisilam tunaosali sala tano, lakini mkewangu hataki kusikiliza mawaidha na kashuhulishwa sana na TV yeye anavipindi vingi sana kwenye TV ambavyo anavifuatilia kwa karibu sana na hawezi kuvikosa kabisa, mimi napenda sana kusikiliza mawaidha na ninapoweka mawaidha mkewangu yeye hutafuta shuhuli nyingine yeyote ya kufakunya afanye bali kusikiliza hataki na nikimwambia inakuwa ugomvi tumeshagombana sana kwa sababu hizo, lakini kuswali anaswali vizuri kwa wakati na Quraan anasoma lakini ugomvi wetu ni kusikiliza mawaidha na kusoma tafsiri ya Quraan tu .

sasa naombeni msaada wenu jee nimsaidie vipi mtu huyu? Kwa sababu wakati mwingine huniambia nipunguze sauti mawaidha yangu ili yeye asikilize TV au anaweza akaifunga kabisa Radio ya mawaidha.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa suala lako hili miongoni mwa matatizo ya kijamii. Mara nyingi kufikwa na hayo ni kuwa hatukufuata muongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mas-ala ya ndoa.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia sana tuchague mke mwenye dini, maadili na mengineyo ambayo yanasaidia familia. Mambo haya unayotaka kwa mkeo awe nayo ni lazima ulikuwa umeyatazama kabla hamjafunga Ndoa. Ikiwa wakati huo kabla hujamposa ungeona ana tabia ambayo hutawezana nayo basi ungejitoa katika posa mapema. Baada ya hapo unatafuta yule ambaye anaweza kukuridhi. Huko ndiko kufuata mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyetusisitiza tuchague wake wenye kushika Dini.

Makosa kama haya hupatikana katika maisha ya mwanadamu kwa wakati mmoja au mwengine. Hivyo, katika maisha yetu inabidi tuwe ni wenye kuchukua tahadhari ili tusiingie katika shimo ambalo baadaye inakuwa shida kutoka.

Jambo ambalo unaweza kufanya kwa wakati huu ni wewe kukaa naye na umueleze umuhimu wa mawaidha na Qur-aan, madhara ya runinga (TV) katika maisha yake na pia familia yenu. Japokuwa unasema anaswali na kusoma Qur-aan inawezekana ni katika zile ada alizokulia nazo. Wengi wetu huswali bila kujua umuhimu wake au kusoma Qur-aan bila kujua maana yake. Hii inakuwa ni kama ada kwani mama na baba walikuwa katika mtindo nami nimeinukia katika hali hiyo. Kuswali kwa njia hiyo na kusoma Qur-aan hivyo hakuleti natija wala mabadiliko katika maisha ya mtu na mja.

Kwa kawaida, Qur-aan inatakiwa ikubadilishe uwe ni Muislamu bora zaidi kwa kuacha na kuepukana na maasiya. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake, ni uongofu kwa wamchao Allaah” [2: 2].

Na pia: “Allaah Habadilishi hali za watu mpaka wafanye juhudi kubadilisha yaliyo nafsini mwao” [.

Nasaha zetu kwako, ni utafute nafasi muwe mnasoma pamoja Qur-aan ya tafsiri ili mpate yaliyomo ndani yake kwa kina na kutiana hima katika kuyafuata. Wakati mwengine pia unaweza kuwa unamsomea Hadiyth kutoka katika vitabu ambayo vimefasiriwa. Kwa hilo tafuta nafasi ambayo yeye hana shughuli yoyote ile. Jaribu pia kuwa naye karibu na kuzungumza naye kwa upole, ulaini na mawaidha mazuri yenye kumuhimiza na kumliwaza. Pia fanya ada ya kutoka naye na kutembea naye kwenda sehemu ambazo zitamfurahisha na zisizokuwa na uharamu aina yoyote ile. Kwa matembezi hayo huenda mkapata fursa na mioyo kumfunguka.

Hilo la kukumwambia upunguze sauti ya mawaidha ili apate kusikiliza kipindi katika TV si yeye bali ni zile athari alizozipata katika malezi yake kutoka kwa wazazi. Ada na desturi mbaya kwa kawaida inakuwa ni shida kutoka lakini tuna yakini kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka mkeo atarekebishika. Hilo si gumu mbele ya Allaah Aliyetukuka baada nawe kufanya juhudi yako katika hilo kwa mfumo tuliokunashi kwayo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share