Haki Za Wanandoa Na Kuhusu Mahari Ya Mke Aliyepewa Talaka Bila Kuingiliana Na Mumewe

 

Haki Za Wanandoa Na Kuhusu Mahari Ya Mke Aliyepewa Talaka 

Bila Kuingiliana Na Mumewe  

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

 

Assalaamu alaykum.

Mume kafunga ndoa na mke, lakini kabla hajakutana na mkewe (kimwili), akamtaliki. Je hii talaka itahesabika kuwa katika talaka rejea? Ni yapi yanayoambatana na ndoa hii katika suala la mahari na haki za wanandoa hao?

 

Baaraka Allaahu fiykum

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

Wa 'Alaykumus Salaam wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh

 

Ndoa ikivunjika kabla ya wanandoa kuingiliana au kama mume kampa talaka mke kabla hajamuingilia, anapaswa kumpa nusu ya mahari waliyokubaliana na hakuna eda kwa mwanamke.

 

Na ikiwa mume atataka kumrudia mke, atamuoa kwa ndoa mpya na mahari watakayokubaliana.

 

Lakini ‘Ulamaa wengine wanasema kuwa ikiwa mume na mke wameachana kabla ya kufanya tendo la ndoa kuna hali mbili; hali ya kwanza, ikiwa wameachana bila kuingiliana na hawajawahi kuwa pamoja faragha, basi mke ataachiwa nusu ya mahari.

 

Hali ya pili, ikiwa wataachana bila kuingiliana lakini walikuwa wana faragha kama kulala pamoja au kufanya mapenzi japo hawajafanya tendo la ndoa, basi hali hiyo itamlazimu mume kumpa mahari kamili waliyokubaliana na mke atakaa eda.

 

Hoja yao ni kuwa, kukaa kwao faragha ni sawa na kuingiliana.

 

Kwa mujibu wa Qur-aan, usahihi ni kuwa hakuna eda, ni kama Anavyosema Allaah Ta'aalaa:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا ۖ فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا ﴿٤٩﴾

 

Enyi walioamini! Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu. Basi wapeni kitoka nyumba na waacheni huru, kwa mwachano mzuri. [Al-Ahzaab: 49]

 

Ikiwa hawajawahi kukubaliana mahari, basi mume atatoa kiasi atakachojaaliwa kwa uwezo wake kumpatia mke kama "kitoka nyumba".

 

Na Aayah zifuatazo zabainisha kiwango ambacho mke anapewa:

 

لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً ۚوَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ ﴿٢٣٦﴾

 

Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwabainishia kwao mahari. Wapeni kiliwazo kwa mwenye wasaa kadiri ya uwezo wake na mwenye dhiki kadiri ya uwezo wake. Maliwaza kwa mujibu wa ada, ni haki kwa wafanya ihsaan.

 

وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إِلَّا أَن يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَ الَّذِي بِيَدِهِ عُقْدَةُ النِّكَاحِ ۚ وَأَن تَعْفُوا أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۚ وَلَا تَنسَوُا الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٢٣٧﴾

 

Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia kwao mahari, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha isipokuwa wakisamehe au asamehe yule ambaye fungamano la ndoa liko mikononi mwake. Na mkisamehe ni ukaribu zaidi ya taqwa. Na wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye kuona. [Al-Baqarah: 236-237]

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share