Jini, Shaytwaan Na Mchawi
Jini, Shaytwaan Na Mchawi
Imekusanywa Na Muhammad Faraj (Rahimahu Allaah)
Yaliyomo
Jina Lake.. 2
Imani Juu Ya Ghaibu.. 2
Ushahidi Wa Kuwepo Majini Katika Qur-aan Tukufu.. 2
Ushahidi Wa Kuwepo Kwa Majini Katika Mafundisho Ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi Wa alihi Wa Sallam) 'sunnah' 3
Dalili Katika Qur-aan Kuwa Jinni Ameumbwa Kwa Moto.. 4
Dalili Katika Mafundisho Ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)
Kuwa Jinni Ameumbwa Kwa Moto 4
Majini Wanazaliana.. 4
Wameumbwa Kabla Ya Binadamu
Uhusiano Baina Ya Jinni Na Shaytwaan. 5
Ibilisi Ni Katika Malaika?. 6
Aina Za Majini. 7
Mwahali Wanapoishi. 7
Wanakula Na Kunywa.. 7
Wana Uwezo Wa Kujigeuza..8
Wamo Miongoni Mwao Wanawake Na Wanaume..
9 Wanaowa?. 10
Majini Wanakufa?. 10
Wamo Miongoni Mwao Waislamu Na Makafiri. 11
Waislamu Katika Majini Wataingia Jannah?. 11
Majini Wanawaogopa Wanadamu.. 12
Kuweza Kwa Majini Kusikia Habari Za Mbinguni. 13
Uchawi. 13
Nini Maana Ya Uchawi?. 13
Vipi Utaweza Kumjua Mchawi. 16
Dalili Kuwa Uchawi Upo, Kutoka Katika Qur-aan Na Katika Sunnah (mafundisho Ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi Wa Sallam)
Soma Bahati Yako (nyota Yako) Lucky Stars.. 18
Uchawi Umeanza Zama Za Nabii Sulaymaan?. 19
Uchawi Ni Kufru… 19
Hukumu Ya Uchawi Katika Dini Ya Kiislamu.. 21
Kujikinga Na Shari Za Wachawi Na Majini Wao.. 22
Dua Zinamkumba Shaytwaan. 24
Dhikru Allaah.. 24
Usiingize Ndani Ya Nyumba Yako Vifuatavyo
Jina Lake
Ameitwa JINNI kwa sababu ya kutokuonekana kwake na watu, na hii ni kwa sababu kila kisichoonekana kwa jicho la binadamu katika lugha ya kiarabu jina lake hutokana (hutoholewa) na herufi mbili hizi; (Jiym) na (Nuun).
Kwa mfano; 'Bustani' huitwa 'Janna' kwa sababu ya kuzungukwa kwake na majani kila upande pasiweze kuonekana ndani. Elimu ya uzazi huitwa 'Ilmul ajinna', kwa sababu ya kutokuonekana kwa kile kilichokuwemo tumboni mwa mzazi. Hata mwendawazimu naye huitwa 'majinun' kwa sababu ya kutoweka kwa akili yake. Na Majinni nao wamepewa jina hilo kwa sababu ya kutokuonekana kwao kwa macho ya binadamu.
Ukichunguza utaona kuwa maneno yote hayo; 'Janna, ajinna, majinun, jinni', yana herufi ya 'Jiym na Nuun' ndani yake.
Imani Juu Ya Ghaibu
Kuamini juu ya ghaibu (yasiyoonekana) ni katika misingi ya itikadi ya Dini.
Allaah Anasema:
الم ﴿١﴾ ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٢﴾ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣﴾
"Alif Laam Miym. Hiki ni kitabu kisicho na shaka ndani yake, ni mwongoz kwa wenye taqwa. Ambao huamini ya ghayb na husimamisha Swalaah na katika vile Tulivyowaruzuku hutoa. [Al-Baqarah: 1-3]
Katika aya hizi, Allaah ametaja baadhi ya sifa za wachaji Allaah ikiwemo ikiwemo sifa hii ya kuamini Ghaibu.
Na maana ya neno 'Ghaibu', ni yale tusiyoweza kuyaona tuliyofundishwa na Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa au Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Ushahidi Wa Kuwepo Majini Katika Qur-aan Tukufu
Katika Qur-aan Allaah Anasema:
وَإِذْ صَرَفْنَا إِلَيْكَ نَفَرًا مِّنَ الْجِنِّ يَسْتَمِعُونَ الْقُرْآنَ فَلَمَّا حَضَرُوهُ قَالُوا أَنصِتُوا ۖ فَلَمَّا قُضِيَ وَلَّوْا إِلَىٰ قَوْمِهِم مُّنذِرِينَ﴿٢٩﴾
Na pale Tulipowaelekeza kwako (ee Muhammadصلى الله عليه وآله وسلم ) kundi miongoni mwa majini wakisikiliza kwa makini Qur-aan; [Al-Ahqaf: 29]
Na Akasema:
يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَقُصُّونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِي
Enyi hadhara ya majini na wana Aadam! Je hawajakufikieni Rusuli miongoni mwenu wanakusimulieni Aayaat Zangu.. [Al- An’aam: 130]
Ushahidi Wa Kuwepo Kwa Majina Katika Mafundisho Ya Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihi Wa Sallam) ‘Sunnah’
Katika 'Sunnah', (mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), wameelezea [Imam Al-Bukhaariy na Muslim] katika vitabu vyao vilivyo sahihi kwamba Ibni 'Abbaas (Radhwiya Allaahu anhu) amesema:
"Majinni waliposhindwa kupata siri kutoka mbinguni na wakawa wanafukuzwa kwa vimondo kila wanapojaribu kuzisogelea mbingu, wakarudi makwao. Na jamii zao walipotaka kujua sababu ya kurudi kwao huko na kushindwa kwao kupata siri za mbinguni, maana kabla ya hapo walikuwa wakiweza kupata baadhi ya habari za huko, wakawajibu:
"Pamewekewa vizuizi baina yetu na baina ya (kupata) habari za mbinguni".
Wenziwao wakasema:
"Bila shaka pana jambo kubwa lililotokea, tembeeni ardhi yote Mashariki na Magharibi mtafute ni kitu gani kilichokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni.”
Walipofika mahali paitwapo; “Soko la Akadha”, waislamu walikuwa wakiswali Swala ya Alfajiri, na majini hao wakaisikia Qur-aan ikisomwa, ndipo waliposema:
"Hii (Qur-aan) wAllaahi, ndiyo iliyokuzuwieni msiweze kupata habari za mbinguni."
Wakarudi kwa watu wao na kuwaambia:
"Enyi jamii yetu! “Hakika sisi tumesikia Qur-aan ya ajabu"Allaah Amesema katika Suwrah Jinn aayah ya mwanzo:
قُلْ أُوحِيَ إِلَيَّ أَنَّهُ اسْتَمَعَ نَفَرٌ مِّنَ الْجِنِّ فَقَالُوا إِنَّا سَمِعْنَا قُرْآنًا عَجَبًا﴿١﴾
Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nimefunuliwa Wahy kwamba kundi miongoni mwa majini lilisikiliza; wakasema: ‘Hakika sisi tumeisikia Qur-aan ya ajabu. [Al-Jinn: 1]
Hizi ni dalili zilizo wazi za kuwepo kwa viumbe hawa, na kukanusha kuwepo kwao kwa sababu ya kutokuonekana kwao si hoja maana vitu vingi hatuvioni na tunakubali kwamba vipo kutokana na athari zake. Kwa mfano, joto, baridi, umeme nk. Hivi vyote hatuvioni lakini tunakubali kuwepo kwake baada ya kuona athari zake.
Dalili Katika Qur-aan Kuwa Jinni Ameumbwa Kwa Moto
Ndani ya Qur-aan mna dalili nyingi zinazotujulisha kuwa Jinni ameumbwa kwa moto, na tutazitaja baadhi ya dalili hizo:
Allaah Amesema:
قَالَ مَا مَنَعَكَ أَلَّا تَسْجُدَ إِذْ أَمَرْتُكَ ۖ قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿١٢﴾
(Allaah) Akasema: Nini kilichokuzuia usisujudu Nilipokuamrisha? (Ibliys) Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye Umemuumba kwa udongo. [Al-A’raaf: 12]
Na Akasema:
وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّارٍ ﴿١٥﴾
Na Akaumba majini kutokana na mwako wa moto. [Ar-Rahman: 15]
Dalili Katika Mafundisho Ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Kuwa Jinni Ameumbwa Kwa Moto
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametujulisha pia kuwa Majini wameumbwa kwa moto, na tutataja baadhi ya kauli zake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Wameumbwa Malaika kwa nuru na Majini kwa ndimi za moto na Adam ameumbwa kwa mliyokwisha elezewa (Udongo)." [Muslim]
Majini Wanazaliana
Allaah Anasema:
أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا ﴿٥٠﴾
Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami; na hali wao kwenu ni maadui? Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu. [Al-Kahf: 50]
Kauli ya Allaah katika aya hii pale aliposema 'Na Kizazi Chake'. inamaanisha kwamba majini wanazaliana.
Wameumbwa Kabla Ya Binadamu
Allaah Anasema:
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ﴿٢٦﴾وَالْجَانَّ خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ السَّمُومِ﴿٢٧﴾
Na kwa yakini Tumemuumba insani kutokana na udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyotaghayari. Na majini Tuliwaumba kabla kutokana na moto ulio mkali mno. [ Al-Hijr: 26-27]
Kwa hivyo majini waliumbwa kabla yetu na waliishi katika ardhi hii hata kabla ya kuumbwa kwa Aadam ('Alayhis-salaam), na hii ndiyo maana Allaah alipowaarifu Malaika kuwa anataka kuumba viumbe katika ardhi wakasema:
قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَن يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ
Utaweka humo atakayefanya ufisadi humo na kumwaga damu.., [Al-Baqarah: 30]
Malaika waliuliza suala hili si kwa ajili ya kupinga amri ya Allaah au kwa kumuonea wivu mwanadamu, bali waliuliza kwa ajili ya kutaka kuijua hekima ya kuumbwa viumbe hawa, na hii ni kwa sababu walielewa kutokana na viumbe vilivyotangulia vilivyoishi ardhini, kwamba vina sifa ya ufisadi na umwagaji wa damu.
Anasema Ibni Kathiyr (huyu ni katika ‘Ulamaa na mfasiri mkubwa wa Qur-aan) kwamba kabla ya kuumbwa kwa wanadamu, Majinni na viumbe wasiokuwa wanadamu walikuwa wakiishi ardhini na kwamba walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa pamoja na umwagaji wa damu.
Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"Majinni waliishi ardhini kabla ya wanaadamu na walikuwa wakifanya ufisadi mkubwa na Allaah akawaondoa na kuwaleta wanadamu." Maneno kama haya pia yalisemwa na Hassan Al-Basry (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na akaongeza kusema:
"Hii ndiyo maana Malaika wakamuuliza Rabb wao suali hilo."
Uhusiano Baina Ya Jinni Na Shaytwaan
Shaytwaan na Jinni asili yao ni moja, hapana hitilafu baina ya maulamaa kuhusu jambo hili, isipokuwa wamekhitalafiana katika suala; “Je Ibilisi ndiye baba wa Majinni (asili yao) mfano wa Adam ambaye ni baba yetu na asili yetu ?)”
Majibu:
Iblisi si asili yao, bali yeye ni miongoni mwao.
Allaah Anasema:
إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ
Isipokuwa Ibliys alikuwa miongoni mwa majini [Al-Kahf: 50]
Kwa vile Allaah Amemtaja Iblisi kuwa ni MIONGONI mwa majini, kwa hivyo yeye ni mmoja wao na si asili yao kama mfano wa Adam ('Alayhis-salaam) alivyokuwa asili ya wanadamu.
Tulisema kuwa wameitwa 'Majinni ' kwa sababu ya kutokuonekana kwao na sisi tumeitwa 'Insaan' kwa sababu ya kusahau kwetu, kwani neno 'Insan', asili yake linatokana na neno 'Nisiyaan', na maana yake ni Kusahau.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: "Adam alisahau na vizazi vyake vikasahau."
Ama neno 'Shaytwaan', katika lugha ya kiarabu maana yake ni 'Kila anayeasi na kupinga au kuzuwia au kushawishi viumbe wasiifuate njia ya Allaah', awe Jinni au Mwanadamu.
Allaah Anasema:
وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا ۚ وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُ ۖ فَذَرْهُمْ وَمَا يَفْتَرُونَ ﴿١١٢﴾
Na hivyo ndivyo Tulivyojaalia kwa kila Nabiy maadui - mashaytwaan katika wana Aadam na majini wakidokezana wenyewe kwa wenyewe maneno ya kupambapamba na ya ghururi. Na lau Angetaka Rabb wako wasingeliyafanya hayo. Basi waachilie mbali na wanayoyatunga. [Al-An’aam: 112]
Iblisi si katika Malaika, bali ni miongoni mwa Majinni kutokana na dalili zifuatazo:
Anasema:
فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ
Wakasujudu isipokuwa Ibliys alikuwa miongoni mwa majini.. [Al-Kahf: 50]
Na Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾
Hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahrym: 6]
Kutokana na aya hii, tunapata ushahidi mwingine kuwa; Malaika hawamuasi Allaah. Kwa hivyo Ibilisi angelikuwa Malaika, asingemuasi Rabb wake bali angetenda kama alivyoamrishwa. Lakini yeye alitenda kinyume na hivo. Alimuasi Allaah pale alipokataa kumsujudia baba yetu Aadam ('Alayhis Salaam), akasema:
قَالَ مَا مَنَعَكَ أَلَّا تَسْجُدَ إِذْ أَمَرْتُكَ ۖ قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿١٢﴾
(Allaah) Akasema: Nini kilichokuzuia usisujudu Nilipokuamrisha? (Ibliys) Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye Umemuumba kwa udongo. [Al-A’raaf: 12]
Na hapa pia tunapata ushahidi mwingi pia kuwa Iblisi si miongoni mwa Malaika, kwani Malaika wameumbwa kwa Nuru na Mashaytwaan wameumbwa kwa moto.
Katika aayah iliyotangulia Iblisi alisema:
أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ
Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto…[Al-A’raaf: 12]
Angelikuwa yeye ni miongoni mwa Malaika angelisema;
“Mimi ni bora kuliko yeye umeniumba kwa Nuru".
Kwa sababu Malaika wameumbwa kwa Nuru kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika hadiyth iliyotangulia:
"Malaika wameumbwa kwa nuru na Majini kwa ndimi za moto na Adam (ameumbwa) kwa mliyokwisha elezewa (Udongo)." [Muslim na Ahmad bin Hanbal]
Aina Za Majini
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Majini (wako) namna tatu, namna moja wana mabawa wanaruka na namna (nyengine) majoka na n’ge na namna nyengine hawaishi mahala pamoja na hupenda kuhama." [Atw-Twabaraaniy na Al-Haakim na Al-Bayhaqiy na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy]
Mahali Wanapoishi
Majini wanaishi katika majangwa na katika sehemu za kutupa taka, kwa sababu wao wanakula mabaki ya vyakula vya binadamu.
Zimepokelewa hadiyth nyingi pia kwa njia ya Ibni 'Abbaas na Ibni Masaood (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akienda jangwani na kuwasemesha Majinni na kuwalingania katika dini ya Kiislamu na kuwataka wamuabudu Allaah mmoja wa kweli.
Majinni wanapenda pia kuishi vyooni, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametufundisha dua ya kusoma kabla ya mtu kuigia chooni, akasema:
Mmoja wenu anapoingia chooni basi aseme:
"Allaahumma inniy audhu bika minal khubuthi wal khabaaith."
Na maana yake:
“Allaah najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake.” [Al-Bukhaariy na Muslim.]
Majini pia wanaishi katika Mashimo:
Kutoka kwa Qataadah kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mmoja wenu asikojowe ndani ya shimo."
Na alipoiulizwa kuna ubaya gani mtu kukojoa ndani ya shimo akasema:
"Inasemekana kuwa Majinni wanapenda kuishi humo."
[Annasaiy]
Wanakula Na Kunywa
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mmoja wenu anapokula, basi ale kwa (mkono wa) kulia na anapokunywa anywe kwa (mkono wa) kulia, kwa sababu Shaytwaan anakula kwa kushoto na kunywa kwa kushoto." [Muslim]
Na akasema:
"Mtu anapoingia nyumbani akasema; 'BismiAllaah', na anapokula (akasema BismiAllaah), Shaytwaan husema; 'Hatuna makazi humu (ndani ya nyumba hii), na hatuna chakula cha usiku'. Ama anapoingia asiseme; 'BismiAllaah', Shaytwaan husema; 'Tumepata makazi humu', na asiposema BismiAllaah pale anapokula, basi (Shaytwaan) husema; 'Tumepata makazi na chakula". [Muslim]
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alinipa jukumu la kulinda (chakula cha) zaka ya Ramadhwaan, akaja mtu akawa anaiba katika chakula kile, nikamkamata na kumuambia kwamba nitampeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), akasema: 'Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi na shida nyingi."
Anasema (Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
"Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaniuliza:
“Ee Abu Hurayrah umefanya nini na mfungwa wako jana?"
"Akasema:
"Nikamwambia:
"Ee Rasuli wa Allaah, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha."
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
“Ama huyu amekudanganya na atarudi.”
Nikajuwa kwamba atarudi kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema hivyo. Nikamtegea, akaja tena siku ya pili kuiba chakula, nikamkamata, nikamuambia nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Akaniambia:
“Mimi ni muhitaji na nina watoto wengi sitorudia tena.”
Nikamuacha aende zake, na asubuhi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
“Ee Abu Hurayrah umefanya nini na mfungwa wako jana?”
Nikamuambia:
"Ee Rasuli wa Allaah, alinisikitikia shida zake na watoto wengi nikamuonea huruma nikamuacha."
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Ama huyu amekudanganya na atarudi."
Nikamkamata mara ya tatu akiwa anaiba (tena) chakula, nikamuambia:
"Nitakupeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na hii ni mara ya tatu na kila mara unasema hutorudia kisha unarudia."
Akasema:
"Niache nikufundishe maneno Allaah atakufaa nayo."
Nikamuuliza;
“Maneno gani hayo?"
Akasema:
“Unapokuwa juu ya tandilo lako soma Ayatul Kursy - Allaahu laa ilaaha illa huwal hayyul qayuum - mpaka mwisho na itaendelea kukuhifadhi aya hii na hatokukaribia Shaytwaan mpaka utakapoamka.”
Nikamuacha aende zake.
Asubuhi yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaniuliza:
“Amefanyaje mfungwa wako jana?”
Nikamuambia:
"Ee Rasuli wa Allaah amejidai eti amenifundisha maneno ambayo Allaah Atanifaa nayo, basi nikamuacha huru."
Akaniuliza;
“Ni maneno gani hayo?”
Nikasema:
"Ameniambia:
“Unapokuwa juu ya tandiko lako soma Ayatul Kursy mpaka mwisho na Allaah ataendelea kukuhifadhi nayo na hatokukaribia Shaytwaan mpaka utakapoamka."
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Ama yeye amesema kweli ingawaje ni muongo. Unamjua nani uliyekuwa ukizungumza naye siku tatu hizi ewe Aba Hurayrah?"
Nikajibu:
"La simjuwi".
Akasema:
“Yule ni Shaytwaan.”
[Al-Bukhaariy]
Kwa vile Shaytwaan huyu aliyekuwa akiiba alikuwa akimjia Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa sura ya binadamu, basi hii ni dalili kwamba majini wanao uwezo wa kujibadilisha umbile lao.
Wamo Miongoni Mwao Wanawake Na Wanaume
Katika hadiyth niliyoitaja hapo juu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:
"Anapoingia mmoja wenu chooni, basi aseme: “Allaah najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Wanaowa?
Majini wanaoana na kuzaliana, na ushahidi umo ndani Qur-aan katika kauli Yake Subhaanahu wa Ta’aalaa Aliposema:
ۗ أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ ۚ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلًا ﴿٥٠﴾
Je, basi mnamfanya yeye na kizazi chake walinzi pasi Nami; na hali wao kwenu ni maadui? Ubaya ulioje mbadala huu kwa madhalimu. [Al Kahf: 50]
Hata hivyo ‘Ulamaa wengi hawakubali majini waowane na wanadamu. Pana kisa cha mwanamke mmoja kutoka Yemen alikuwa akidai kwamba anajiwa na jinni na kwamba jinni huyo anataka kumuowa. Alipoulizwa Imam Malik kuhusu jambo hili akasema:
“Sioni kifungu chochote cha sheria kinachoharamisha, isipokuwa nakuogopeeni fitna (Mitihani).”
‘Ulamaa wamesema kuwa kauli ya Imam Malik hii inatujulisha juu ya hofu yake, kwani mwanamke yeyote anaweza kujipatia mimba kwa njia zisizo za halali, kisha akasema kwamba ameolewa na jinni na kwa njia hii uhuni utazidi na fitna zitaenea.
‘Ulamaa wengine wamekataa kabisa fikra ya kuoana baina ya majini na wanadamu wakiegemea kauli ya Allaah Isemayo:
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ
Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake ni kwamba Amekuumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao; [Ar-Ruwm: 21]
Na Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَنِينَ وَحَفَدَةً
Na Allaah Amekufanyieni wake katika jinsi yenu; na Amekufanyieni katika wake zenu wana na wajukuu…; [An-Nahl: 72]
Katika aayah hizi Allaah anatufahamisha kwamba ametuumbia wake zetu katika jinsi yetu, wakati Majinni si katika Jinsi yetu. Na akasema; “Ili mupate utulivu kwao", wakati mwanadamu hawezi kupata utulivu kwa jinni, maana siku zote mtu hupata utulivu kwa kiumbe aliye mfano wake na majini si mfano wetu.
Allaah Anasema:
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾
Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka. [Ar-Rahmaan: 26]
Na Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۘ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ
Na wala usiombe pamoja na Allaah mwabudiwa mwingine. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. [Al-Qaswas: 88]
Inavyojulikana ni kwamba Iblisi yuhai mpaka siku ya Qiyaamah.
Allaah Amesema:
قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴿٣٦﴾قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ﴿٣٧﴾إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ﴿٣٨﴾
Akasema: Rabb wangu! Nipe muhula mpaka Siku watakayofufuliwa. (Allaah) Akasema: Basi hakika wewe ni miongoni mwa waliopewa muhula. Mpaka siku ya wakati maalumu. [Al-Hijr: 36-38]
Kwa hivyo Ibilisi ataishi mpaka siku maalum anayoijua Allaah peke yake kisha atakufa, na majini nao pia wanazaliana na wanakufa kama sisi.
Wamo Miongoni Mwao Waislam Na Makafiri
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesema:
وَأَنَّا مِنَّا الْمُسْلِمُونَ وَمِنَّا الْقَاسِطُونَ ۖ فَمَنْ أَسْلَمَ فَأُولَـٰئِكَ تَحَرَّوْا رَشَدًا﴿١٤﴾
Na kwamba miongoni mwetu ni Waislamu, na miongoni mwetu wakengeukaji haki; hivyo atakayesilimu, hao ndio waliofuata uongofu. [Al-Jinn: 14]
Na Akasema:
وَأَنَّا مِنَّا الصَّالِحُونَ وَمِنَّا دُونَ ذَٰلِكَ ۖ كُنَّا طَرَائِقَ قِدَدًا﴿١١﴾
Na kwamba miongoni mwetu ni wema, na miongoni mwetu kinyume chake; tumekuwa makundi ya njia mbali mbali. [Al-Jinn: 11]
Katika kuifasiri aayah hii, anasema Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
"Kauli ya Allaah; “Tumekuwa njia mbali mbali”, maana yake ni “Makafiri na Waislamu”.
Baadhi ya ‘ulamaa wanasema:
"Dini mbali mbali na madhehebu mbali mbali."
Waislamu Katika Majini Wataingia Jannah?
Katika tafsiri yake Ibni Kathyir amesema:
"Waislamu miongoni mwa Majini wataingia Jannah kama Waislamu katika wanadamu "Na dalili yake pamoja na dalili za maulamaa wengine ni kauli ya Allaah akitujulisha juu ya hali ya wanawake wa Jannah Aliposema:
لَمْ يَطْمِثْهُنَّ إِنسٌ قَبْلَهُمْ وَلَا جَانٌّ ﴿٧٤﴾
Hajawabikiri binadamu kabla yao wala jini. [Ar-Rahmaan: 74]
Na Aliposema:
وَلِمَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ جَنَّتَانِ ﴿٤٦﴾فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٧﴾
Na kwa mwenye kukhofu kisimamo mbele ya Rabb wake atapata bustani mbili. Basi ni zipi neema za Rabb wenu mnazikadhibisha? [Ar-Rahmaan: 46-47]
Allaah Amejaalia jazaa ya majini na binadamu wema kuwa ni jannah, na majini waliijibu aya hii kwa kumshukuru Allaah wakasema:
"Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako."
Hii ni hadiyth iliyosimuliwa na Imam At-Tirmidhiy kutoka kwa Jabir (Radhwiya Allaahu anhu) kwamba amesema:
"Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliisoma Suwrah Rahman mpaka mwisho kisha akasema: ‘Mbona mumenyamaza kimya, Majini wamekuwa bora kuliko nyinyi kwa kujibu kila ninapowasomea aayah hii:
فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٩﴾
Basi ni zipi neema za Rabb wenu mnazikadhibisha? [Ar-Rahmaan: 49]
Wao huijibu kwa kusema:
"Hapana katika neema zako zozote zile tunazozikanusha kwa hivyo shukrani zote ni Zako."
Imesimuliwa na At-Tirmidhiy na Al-Bazaar na Al-Haakim na pia Ibni Jariyr na Shaykh Al-Albaaniy amesema kwamba hadithi hii ni njema.
Dalili inayopatikana kutoka katika aayah hizi ni kwamba; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa Majini mafundisho ya Dini, na kuwafahamisha kwamba pana jaza ya Jannah kwa Mwenye kuogopa.
Kama Majini hawatoingia Jannah hapangekuwa na haja ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwatokea na kuwapa mafunzo ya dini na kuwajulisha juu ya Jannah inayowangoja wale wanaomuogopa Allaah.
Majini Wanawaogopa Wanadamu
Ameeleze Ibn Abi Al Dunya kwamba Mujahid amesema:
‘Usiku mmoja nilikuwa nikiswali akanitokea mfano wa mtoto mdogo mbele yangu nikamshika kwa nguvu zangu zote akainuka na kuuruka ukuta hata nilisikia kishindo cha kuanguka kwake.’ Akaendela kusema: ‘Wao (majini) wanakuogopeni kama nyinyi mnavyowaogopa."
Imepokelewa kutoka kwa Mujahid kuwa alisema:
‘Shaytwaan anakuogopeni kuliko nyinyi mnavyomuogopa akikukaribia usimregezee akakupanda, bali shindana naye na hatimae ataondoka."
Kuweza Kwa Majini Kusikia Habari Za Mbinguni
Imepokelewa kutoka kwa Ibni 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba alisema:
‘Amenihadithia mmoja katika Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa, usiku mmoja walipokuwa wamekaa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) nyota moja ikaanguka na kun’gara. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza:
"Mlikuwa mkisemaje wakati wa ujahilia (kabla ya kuja Uislamu?"
Wakajibu:
"Tulikuwa tukisema; Usiku wa leo amezaliwa mtu mtukufu na amekufa mtu mtukufu."
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia:
"Bali haiangushwi nyota kwa ajili ya kifo cha mtu wala kwa kuzaliwa kwa mtu, lakini Rabb wetu Aliyetukuka anapotoa amri, Malaika wabebao Arshi husabbih (husema Subhana Allaah), na viumbe vya mbinguni vyote humsabihi Allaah pia, kisha husabihi viumbe wa mbingu za chini mpaka habari inapofika katika mbingu ya dunia, majini huzipata habari hizo na huwatupia mabwana zao nazo ni habari za kweli, lakini wao huongeza habari za uongo juu yake.”
Kutokana na Bibi 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), amesema:
"Niliuliza:
"Ee Rasuli wa Allaah, makuhani walikuwa wakituelezea baadhi ya mambo na yalikuwa ni ya kweli."
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Hiyo ni habari ya kweli ameipokea jini akamtupia bwana wake na kuongezea uongo mara Mia."
[Imetolewa na Maimaam Al-Bukhaariy na Muslim na Ahmad na AlBayhaqiy]
Uchawi
Nini Maana Ya Uchawi?
Al Azhari ambaye ni mtungaji wa kamusi maarafu ya kiarabu iitwayo “LisanulArab” amesema:
“Neno “Uchawi”, kwa kiarabu “As Sihr”, maana yake ni kitendo cha kujikurubisha na Shaytwaan na kwa msaada wake (Shaytwaan)”, na akasema pia kuwa; “Uchawi ni kulibadilisha jambo mbali na uhakika wake, nako ni kuwadhihirishia watu jambo lisilo la kweli wakaliona kuwa ni la kweli.” Ama Swahaba Ibni 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"Uchawi ni kuidhirisha batili katika sura ya haki." Hayo ni katika kamusi za lugha.
Amma katika kamusi ya dini, maana ya neno Uchawi (As Sihr), kama alivyofasiri Mwanachuoni mkubwa Fakhruddin Al Razi kuwa:
"Ni kila jambo lililofichika sababu zake, linalotokeza kwa sababu zisizo za kawaida na ndani yake mna hadaa (khidaa)."
Amma Shaykh Wahiyd Abdulsalaam Bali, mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho 'Al Saarim Al Batar fiy muhaarabat Al Saharatul ashraar', na kitabu kiitwacho "Al wiqaya mina l jinni wa shaytan", ambaye pia ni mtaalamu maarufu katika elimu ya majini na Mashaytwaan na uchawi na ambaye pia ni katika maulamaa maarufu wanaotoa majini kwa njia ya kusoma Qur-aan, yeye anasema:
"Uchawi ni makubaliano baina ya mchawi na Jinni akishurutishwa mchawi kufanya mambo ya haramu au ya shirki, na baada ya kufanya hayo, Jinni anashurutishwa kumsaidia na kumtii mchawi huyo kwa kila anachotaka."
Baadhi ya yale ambayo mchawi anatakiwa na Shaytwaan ayatende ili ajikurubishe naye ni:
· Mchawi anatakiwa auvae msahafu miguuni na aingie nao chooni |
· Aandike baadhi ya aayah za Qur-aan kwa damu ya hedhi. |
· Miongoni mwao wanashurutishwa kuandika aya za Qur-aan penye nyayo za miguu. |
· Au aiandike suwrah Al-Faatihah kinyume nyume. |
· Asali bila ya Udhuu. |
· Wengine hutakiwa kuchinja mnyama bila ya kulitaja jina la Allaah kisha amtupe mnyama huyo mahali maalum anapoamrishwa na Shaytwaan. |
· Wamo miongoni mwao wanaozungumza na nyota au kuzisujudia. |
· Au hutakiwa kuandika herizi kwa maneno yenye kufru ndani yake |
Imeelezwa kwamba katika nchi ya Sham kulikuwa na mtu ambaye watu walikuwa wakimpenda na kumheshimu sana wakimdhania kuwa ni mtu mwenye makarama.
Mtu huyu alikuwa kila mwaka katika msimu wa Hajj akiwatumikia watu wa mji wake kwa kuchukua barua zao na vitu vyao na kuwapelekea watu wao waliokwenda Saudia kuhijji. Alikuwa akipeleka na kurudi kwa muda wa siku moja au mbili tu, na watu walimpenda sana na kuamini kwamba alikuwa ni Waliy.
Siku moja mtu huyo aliumwa sana, akamuita mwanawe na kumwambia kuwa kama atakufa, basi ende mahali fulani wakati wa usiku na atamkuta ngamia wa aina fulani na ampande na kufuata amri zote atakazopewa na ngamia huyo.
Alipofariki dunia, mwanawe alifanya kama alivyoambiwa na baba yake, akaondoka peke yake wakati wa usiku na kuelekea jangwani kule alikoambiwa na baba yake kuwa atamkuta ngamia. Akamkuta ngamia kama alivyoambiwa, akampanda na alipokuwa akenda, ngamia akaanza kusema na kumtaka kijana yule ashuke na amsujudie.
Yule kijana alishtuka sana kusikia ngamia akisema na pia akashangazwa na amri zake, akamwambia:
"Vipi nikusujudie, kweni wewe ni nani?"
"Ikiwa unataka nifuate amri zako kama nilivyokuwa kwa baba yako, na nikupeleke popote utakapo duniani, basi unisujudie kama alivyokuwa akinisujudia baba yako."
Yule kijana akajibu:
"Mimi ninamsujudia Allaah peke yake, amma wewe la, siwezi kukusujudia."
Ngamia akamrusha kijana yule kutoka juu ya mgongo wake na kumwangusha chini, na kijana yule akatoka mbio mpaka nyumbani kwa mama yake na kumuelezea yote aliyoyaona na kwamba baba yake alikuwa akimsujudia Jinni ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kusafiri kila anapotaka kwenda kwa kupaishwa na jini yule.
Kwa haya inatubainikia kuwa Jinni hamsaidii wala hamhudumii mchawi wala mtu yeyote isipokuwa naye kwa mkabala wake atumikiwe kwa kutendewa matendo ya kufru, na ‘ulamaa wanasema:
"Kila mchawi anapokufuru zaidi, basi Shaytwaan humtumikia kwa nguvu zaidi, na mchawi akitaka apate huduma ya hali ya juu kabisa kutoka kwa masultani wa majini au kwa kiarabu wanaitwa "Maradatul Jinni", basi inambidi afanye kufuru kubwa zaidi, na kwa ajili hiyo, mchawi anapotaka nguvu juu ya wenzake inamlazimikia akufuru zaidi."
Kutokana na haya tunafahamu kwamba mchawi na Shaytwaan ni marafiki na washirika katika kumuasi Allaah.
Allaah Anasema:
وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ قَدِ اسْتَكْثَرْتُم مِّنَ الْإِنسِ ۖ وَقَالَ أَوْلِيَاؤُهُم مِّنَ الْإِنسِ رَبَّنَا اسْتَمْتَعَ بَعْضُنَا بِبَعْضٍ وَبَلَغْنَا أَجَلَنَا الَّذِي أَجَّلْتَ لَنَا ۚ قَالَ النَّارُ مَثْوَاكُمْ خَالِدِينَ فِيهَا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ ﴿١٢٨﴾
Na Siku Atakapowakusanya wote (Allaah Atasema): Enyi hadhara ya majini! Kwa yakini mmetafuta kwa wingi (kuwapotoa) katika wana Aadam. Na watasema marafiki wao wandani katika wana Aadam: Rabb wetu! Tulinufaishana baadhi yetu na wengineo, na tumefikia muda wetu ambao Umetupangia. (Allaah) Atasema: Moto ndio makazi yenu, ni wenye kudumu humo, isipokuwa Atakavyo Allaah. Hakika Rabb wako ni Mwenye hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. [Al-An'aam: 128]
Vipi Utaweza Kumjua Mchawi?
Zifuatazo ni dalili zitazokuwezesha kutofautisha baina ya mganga na mchawi. Utakapoona mojawapo ya dalili zufuatazo utambuwe kuwa huyo ni mchawi bila shaka yeyote na wala si shekhe au mganga:-
· Mchawi huuliza jina la mgonjwa na jina la mama yake |
· Huchukua baadhi ya vitu vya mgonjwa kama vile nguo za nje au za ndani au kitambaa cha kufutia jasho n.k. |
· Hutaka mnyama mwenye sifa maalum au rangi maalum ili achinjwe na hapigiwi BismiLLaahi anapochinjwa |
· Huandika hirizi |
· Husema maneno yasiyojulikana |
· Humtaka mgonjwa aepukane na watu muda maalum na akae katika chumba kisichofikiwa na juwa |
· Mara nyengine humtaka mgonjwa asiguse maji muda wa siku arubaini hivi (anasema Shaykh Wahiyd Abdulsalaam Bali kwamba akikutaka ufanye hivyo ujue kwamba Jinni anayemtumikia mchawi huyo ni mkiristo) |
· Humpa mgonjwa vitu ili avifukie ardhini |
· Humpa mgonjwa karatasi aziunguze kisha ajifukize na moshi wake |
· Mara nyengine humwambia mgonjwa jina lake na mji anaoishi |
· Huandika maneno katika karatasi na kumwambia mgonjwa azichemshe na kunywa maji yake |
UKIONA DALILI HIZI KWA MGANGA UMJUE HAPO HAPO KUWA NI MCHAWI NA UEPUKANE NAYE |
Anasema Shaykh Wahiyd Abdulasalaam Bali:
"Ukiutizama uso wa mchawi utakiona kiza cha kufru kilivyotanda katika uso huo mfano wa mawingu meusi.”
Anaendelea kusema Shaykh huyo:
“Kwa wale wanaowajua wachawi, wanawaona siku zote wakiwa katika dhiki, shida, matatizo katika siha zao, matatizo na wake zao au watoto wao na siku zote hawana raha wala utulivu.”
Allaah Anasema:
وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا
Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wana Aadam wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu. [Al-Jinn: 6]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا
Na atakayejitenga na ukumbusho Wangu basi hakika atapata maisha ya dhiki.., [Twaahaa: 124]
Dalili Kuwa Uchawi Upo, Kutoka Katika Qur-aan Na Katika Sunnah (mafundisho Ya Nabiy (swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Sallam)
Katika Suwrah Yunus aayah ya 77 Allaah Anasema:
قَالَ مُوسَىٰ أَتَقُولُونَ لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَكُمْ ۖ أَسِحْرٌ هَـٰذَا وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُونَ﴿٧٧﴾
Muwsaa akasema: Je, mnasema kuhusu haki ilipokujeni? Hii ni sihiri? Na wachawi hawafaulu.
Hii ni dalili kwamba uchawi upo na Allaah anatufundisha katika aayah hii kwamba uchawi haufaulu.
Na katika suwrah Al-Falaq Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ ﴿٤﴾
Na kutokana na shari ya wanaopuliza mafundoni.
Katika kuifasiri aya hii, mmoja katika 'ulamaa wakubwa wa tafsiri ya Qur-aan Imam Al Qurtuby amesema:
"Maana ya neno "Naffaathaat", ni wachawi wanapopuliza katika nyuzi huku wakizipiga fundo.”
Na Ibni Kathiyr katika tafsiri yake akinukuu kutoka kwa Ikrimah na Mujahid na Al Hassan Al Basry (Radhwiya Allaahu ‘anhum) amesema:
"Hawa wanaopuliza mafundoni ni wachawi, na Allaah anatuamrisha tujiepushe na shari zao.”
Amma hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) zinazotufahamisha kwamba uchawi upo na kwamba uchawi ni katika madhambi makubwa sana, ni hizi zifuatazo:
Kutoka kwa Abi Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Jieupusheni na (mambo) saba Yaangamizayo.'
Wakasema:
'Ni yepi hayo ewe Rasuli wa Allaah?"
Akasema:
"Kumshirikisha Allaah, Uchawi, kuiuwa nafsi iliyoharimishwa na Allaah ila kwa haki yake, kula riba, kula mali ya yatima, kurudi nyuma (kukimbia) katika vita vya Jihadi (huku ukiwaacha wenzio wanapigana), na kuwasingizia uwongo wanawake wema wasio na makosa." [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ndugu yangu Muislamu, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema kuwa mambo hayo 'Yanayomuangamiza', maana yake ni kuwa yanamuangamiza mtu katika moto wa Jahannam
Ukirudia kuisoma tena hadiyth hiyo utaona kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameutanguliza uchawi kabla ya dhambi ya kuuwa, ingawaje kuuwa ni dhambi kubwa sana, na Allaah Anasema katika Suwrah Al-Nisaa aayah ya 93:
وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا ﴿٩٣﴾
Na atakayemuua Muumini kwa kusudi, basi jazaa yake ni Jahannam, ni mwenye kudumu humo na Allaah Atamghadhibikia na Atamlaani na Atamuandalia adhabu kuu. [Al-Nisaa: 93]
Juu ya ukubwa wa dhambi hiyo ya kuuwa, lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) ameipa uzito zaidi dhambi ya Uchawi kwa kuiweka nafasi ya pili baada ya Shirki na kabla ya dhambi ya kuuwa.
Soma Bahati Yako (Nyota Yako) Lucky Stars
Katika hadiyth ifuatayo iliyosimuliwa na Abu Dawood na Ibni Majah hadiyth ambayo Shaykh Al-Albaaniy ameitaja kuwa ni "hadithi njema", na hadithi hii pia ni dalili kwamba elimu ya kutabiri kwa nyota ambayo huandikwa katika magazeti na watu hupenda kusoma kwa kutaka kujua bahati zao, kitendo hiki ni haramu na yeyote atakayesoma nyota yake, basi swala zake hazikubaliwi kwa muda wa siku arobaini, hii ikiwa anasoma na huku haziamini, amma akisoma na huku anaziamini, basi anaingia katika hukumu ya aliyemuendea mtabiri na kumuuliza jambo, na anakuwa amekwisha kufuru yote aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Atakayejifunza sehemu ya elimu ya nyota (utabiri) amejifunza sehemu ya uchawi, akiongeza atakachoongeza (katika uchawi au nyota)."
Na hii ni kwa sababu wanaosoma elimu ya nyota (utabiri) wanaamini kwamba katika nyota wanaishi majini ambao ni masultani na wakuu, na wanaitakidi kuwa mambo yetu yote husababishwa na harakati za nyota hizo kila zinapotaharaki kutoka mahali kuelekea pengine. Kwa ajili hiyo wao huzingoja nyota hizo masaa mengi ya usiku ili wapate kuandika talasimu zao, na huku ni sawa na kuziabudu nyota hizo. (Pana tofauti baina ya elimu ya anga za juu (Astronomy) ambayo haina ubaya wowote ndani yake, na elimu ya nyota (Astrology) - utabiri - ambayo ni haramu).
Ushahidi Mwengine unapatikana katika hadiyth iliyosimuliwa na Umran bin Hussain (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
“Hayuko pamoja nasi mwenye kuamini juu ya nukhsi (waarabu walikuwa wanapotaka kusafiri humrusha ndege na akielekea upande wa kulia basi husafiri, amma akielekea upande wa kushoto huamini ni ukorofi na kuivunja safari yake), na pia hayuko pamoja nasi mwenye kupiga ramli au mwenye kupigiwa, na atakayemuendea mtabiri na akamsadiki asemayo basi kesha kufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)." [Al-Bazaar].
Katika hadiyth hizi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anatukataza tusiwaendee wachawi wala watabiri wa aina yoyote ile kwa kuwauliza juu ya jambo lolote lile, hata kama atajibadilisha na kujiita AlHajj Fulani au Shaykh Fulani au Maalim Fulani au Mganga Fulani na hii ni kutokana na kufru zao wanazozifanya kwa kuwasujudia majini na kuridhishana nao ili wawatumikie.
Na hii ni dalili kwamba uchawi upo, maana kama haupo, basi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) asingetukataza kufanya kisichokuwepo.
Pia hadiyth hizi zinatufahamisha kwamba mambo haya ni haramu na atakayeyatenda anakuwa amekwishayakanusha yale aliyokuja nayo Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa sababu aliyokuja nayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni kwamba hapana aijuwae ghaibu isipokuwa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa.
Hadiyth ziko nyingi sana, lakini hizi pamoja na aya zilizotangulia zinatosha kuwa ni dalili kwamba yote hayo yametajwa katika Qur-aan na katika mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Uchawi Umeanza Zama Za Nabiy Sulaymaan?
Wachawi wanaposoma talasimu zao huwadanganya watu kwa kuanza kusoma baadhi ya aya au sura ndogo ndogo za Qur-aan na kulitajataja jina la Nabii SULAYMAAN na utawasikia daima wanamnasibisha Nabiy huyu ('Alayhis-salaam) na kufru zao hizo ili wajinga wanaowafuata wadhani kwamba hayo yamo katika dini.
Uchawi haujaanza zama za Nabiy Sulaymaan kama wachawi wanavyozuwa na kumsingizia Nabii Huyu wa Allaah, bali ulikuwepo kabla yake kwa miaka elfu nyingi.
Uchawi ulikuwepo tokea zama za Nabiy Saleh ('Alayhis-salaam) aliyekuja kabla ya Nabii Sulaymaan kwa miaka elfu nyingi.
Allaah Anasema:
قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ ﴿١٥٣﴾
Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa. [Ash-Shu'araa: 153]
Uchawi Ni Kufru
Wachawi na wafuasi wao hupenda kumsingizia Nabiy SULAYMAANI kwa kuinasibisha na kufru yao hiyo na Nabiy huyu mtukufu ambaye Allaah alimpa ufalme ambao hajaupata mwengine baada yake kwa kumpa uwezo wa kuwatiisha majini, upepo, na uwezo wa kujua lugha za wanyama n.k.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
فَسَخَّرْنَا لَهُ الرِّيحَ تَجْرِي بِأَمْرِهِ رُخَاءً حَيْثُ أَصَابَ ﴿٣٦﴾ وَالشَّيَاطِينَ كُلَّ بَنَّاءٍ وَغَوَّاصٍ ﴿٣٧﴾ وَآخَرِينَ مُقَرَّنِينَ فِي الْأَصْفَادِ ﴿٣٨﴾
Basi Tukamtiishia upepo unaokwenda kwa amri yake polepole popote anapotaka kufika. Na mashaytwaan, kila ajengaye na mpiga mbizi. Na wengineo, wafungwao minyororoni. [Swaad: 36-38]
Katika tasfiri yake, Ibni Kathiyr amenukuu kauli ya Ibni 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:
"Asif - alikuwa mwandishi wa Nabiy Sulaymaan na alikuwa akilijuwa jina tukufu la Allaah (Al ismul aadham), na alikuwa akiandika kila kitu katika daftari kwa amri ya Nabiy Sulaymaan na kulificha daftari hilo chini ya kiti cha Nabiy Sulaymaani. Alipofariki Nabiy SULAYMAAN, majini wakayatoa maandishi hayo wakachanganya na kuandika baina ya kila mistari miwili uchawi na kufru yao, kisha wakawaambia watu wao kuwa hayo ndiyo maandishi ya Nabiy Sulaymaan na ndiyo aliyokuwa akiyatenda, na Mayahudi wakayasadiki maneno hayo, wakawa wanamtangazia Nabii huyu kuwa ni mchawi.
Mpaka alipokuja Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kuteremshiwa aya ya 102 katika Suwrah Al-Baqarah:
Allaah Anasema:
وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ ۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ ۚ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ۚ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا بِهِ أَنفُسَهُمْ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿١٠٢﴾
Na wakafuata yale waliyoyasoma mashaytwaan juu ya ufalme wa Sulaymaan; na Sulaymaan hakukufuru lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu sihiri na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika (mji wa) Baabil; Haaruwt na Maaruwt. Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme: Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru. Kisha wakajifunza kutoka kwa hao wawili yenye kupelekea kufarikisha kwayo baina ya mtu na mkewe. Na wao hawawezi kamwe kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah; na wanajifunza yanayowadhuru na wala hayawanufaishi; na kwa yakini walijua kwamba atakayechuma haya hatopata katika Aakhirah fungu lolote, na ni ubaya ulioje walichojiuzia nafsi zao, lau wangelikuwa wanajua. [Al-Baqarah: 102]
Katika aayah hii Allaah anatufahamisha pia kuwa uchawi ulikuwepo kabla ya Nabiy Sulaymaan kwa miaka mingi, tokea zama za ustaarabu wa Babiloni walipoteremshwa Malaika wawili, Haruta na Maruta ili kuwaonyesha watu na kuwafahamisha nini uchawi, wapate kuujuwa mara watakapouona na wasiufuate, na hii ni kwa sababu uchawi ni kufru.
Watu waliacha kufuata nasaha za Malaika hao na wakajifunza yale ambayo yatawadhuru na wala hayatawafaa, ingawaje walikuwa wakijuwa kuwa aliyekhiari haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera.
Wachawi mpaka hivi sasa wanajaribu kuunasibisha uchawi wao na Nabiy Sulaymaan pamoja na Malaika hawa wawili.
Tatizo kubwa hupatikana pale wachawi wanapofanya uganga wao pale wanaposema maneno yao ya kichawi. Wao huchanganya maneno hayo na baadhi ya aayah za Qur-aan na wanaofanyiwa uganga hudhania kwamba Qur-aan ndiyo inayosomwa na kwa ajili hiyo na kutokana na ujinga wao, huhadaika na kujiingiza nao katika shirki.
Hukumu Ya Uchawi Katika Dini Ya Kiislamu
Anasema Imam Maalik (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake AlMuwata:
"Mchawi anayefanya uchawi mwenyewe, hukumu yake ni kuuwawa, ama yule anayemuendea mchawi, huyo hauwawi."
Ibni Qudama naye anasema:
"Hukumu ya mchawi ni kuuawa."
Hukmu kama hizi pia zimepokelewa kutoka Swahaba mbali mbali kama vile Umar, Uthmaan, Ibni 'Umar na wengine (Radhwiya Allaahu anhum).
Hukumu hii ya kuuwawa kwa mchawi pia ameitamka Imam Ahmed bin Hambal (Rahimahu Allaah).
Na imepokelewa kutoka kwa Swahaba mbali mbali kwamba Umar bin Al-Khataab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwaandikia Swahaba kuwaamrisha wamuuwe kila mchawi mwanamke au mwanamume. Anasema mmoja katika Swahaba kwamba baada ya kupata maandishi hayo waliwakamata na kuwaua wachawi watatu."
Amma Imam Shafi (Rahimahu Allaah), yeye anaona kuwa mchawi asiuliwe isipokuwa akikiri mwenyewe kwamba ameuwa kwa uchawi wake.
Kutokana na yaliyotangulia infahamika kwamba Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu) pamoja na ‘ulamaa wengi wanaona kwamba hukumu ya mchawi ni kuuliwa, isipokuwa Imam Ash-Shaafi'y (Rahimahu Allaah), yeye anaona kuwa auliwe tu ikiwa mchawi huyo atakiri kwamba ameuwa kwa uchawi wake.
Kujikinga Na Shari Za Wachawi Na Majini Wao
Zifuatazo ni baadhi ya Njia za kujikinga na waovu hao:
Kusafisha Nia
Ibilisi alipohukumiwa kupotea kwa sababu ya kuasi kwake, aliahidi kuwapoteza viumbe wote isipokuwa wale waliosafika kikweli.
Ibilisi akasema kumwambia Allaah:
إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ﴿٤٠﴾
Isipokuwa waja Wako miongoni mwao waliokhitariwa kwa ikhlaasw zao. [Al-Hijr: 49]
Kusafisha nia (Al-Ikhlas), maana yake ni kuzihusisha Ibada zote kwa moyo wote kwa ajili ya Allaah peke yake, siyo kujionyesha mbele za watu kuwa ni Mcha wa Allaah na unapokuwa peke yako unamuasi.
Al Junaid, mmoja katika maulamaa wakubwa wa wakati wake amesema:
"Allaah ana waja wake wenye akili, walipopata akili wakaifanyia kazi, walipofanya kazi wakaitakasa kazi hiyo na kule kuitakasa kwao kukawaingiza katika milango ya kheri yote."
Kutia Udhu
Katika hadiyth nyingi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametufundisha juu ya umuhimu wa kubaki na udhu kila mtu anapoweza kwa ajili ya kupata thawabu na kwa ajili ya kujikinga na kila shari.
Swala Katika Jamaa
Kuswali swala za jamaa msikitini, maana Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kwamba mbwa mwitu (Shaytwaan) huwala kondoo wanaotembea mbali na wenzao.
Swala Za Sunnah
Swala za Sunnah uziswali nyumbani, usiiache nyumba yako ikawa kama kaburi, na unaposwali nyumbani Shaytwaan hulia na kutoka nje ya nyumba yako huku akisema;
"Sina pa kulala humu, wala sina pa kula humu".
Kumuomba Allaah
Kumuomba Allaah kila mara Shaytwaan anapotaka kukuchezea na kila unapoingia mahali pachafu. Kwa mfano:
Unapoingia chooni uisome dua ifuatayo:
"Allaahumma inniy audhu bika minal khubuthi wal khabaaith). Na maana yake; (Allaah mimi najikinga kwako kutokana na majini wanaume na majini wanawake).
Kabla ya kulala usome Suwrah Al-Ikhlaas, Suwrah Al-Falaq na Suwrah Al-Naas pamoja na Ayatul Kursy, maana hadiyth sahihi tuliyoitaja mwanzo wa darsi hii inasema kuwa anayeisoma aayah hii, Allaah anaendelea kumhifadhi mpaka asubuhi anapoamka.
Ni vizuri pia kuzisoma aya tano za mwanzo za Suwrah Al-Baqarah kisha Ayatul Kursy kisha kuzisoma aya tatu za mwisho za Suwrah Al-Baqarah na Allaah Atakulinda na majini pamoja na uchawi katika siku nzima.
Kuzisoma dua mbali mbali kama vile:
(Audhu bikalimati Allaahi ttaamah min kulli shaytanin wa haammah wa min kulli aynin laammah).
Na maana yake ni;
"Najikinga kwa Allaah kutokana na kila Shaytwaan na (kila) mdudu anayesota (kama vile nge na nyoka nk. na kwa kila jicho linalodhuru).
(BismiAllaahi lladhiy laa yadhuru ma-a smihiy shayun fil ardhi walaa fiy ssamaa wahuwa ssamiyl aliym).
Unapotoka nje ya nyumba usome:
(BismiAllaah tawakkaltu ala Allaah walaa haula walaa quwwata illa biAllaah)
Kusoma Qur-aan
Qur-aan ni kinga kubwa sana, na Muislamu anatakiwa daima awe anaisoma nyumbani kwake.
Hapana kitukufu anachokiogopa Shaytwaan kuliko Qur-aan, dua, pamoja na Ibada zinazokusogeza karibu na Rabb wako. Na kila mtu anapokuwa mbali na Rabb wake anakuwa karibu sana na Shaytwaan.
kupiga mfano:
Mtu anapita njiani akakumbana na mbwa mkali anayebweka huku akiwa amemzuwilia njia. Bila shaka mtu huyo atashindwa na hila ya kumuondosha ili apite na zake; bali ataogopa asitafunwe na mbwa huyo. Lakini mtu huyo mara atakapotambua kuwa mwenye mbwa huyo yupo karibu, na kwamba akimuomba amwondoe njiani basi kwa ukelele wake mmoja tu, mbwa huyo ataondoka taratibu na kumpisha apite, bila shaka atamuomba msaada wake.
Mfano huu ni mfano wako wewe binadamu unapomuomba Rabb wako akukinge na Mashaytwaan.
Dua Zinamkumba Shaytwaan
Kama vile Shaytwaan anavyoweza kuwakumba wanadamu walioghafilika na kumdhukuru Allaah, Shaytwaan naye pia hukumbwa na dua za wanaomdhukuru Allaah:
Imeelezwa na ‘ulamaa kuwa, Shaytwaan anapojaribu kumsogelea mcha wa Allaah mwenye kumdhukuru Rabb wake kila wakati kwa ajili ya kumkumba, basi dua zake humkumba Shaytwaan huyo na kumuangusha chini. Kisha Mashaytwaan wenzake hukusanyika na kuulizana:
"Amepatwa na nini huyu?"
Wenzao huwajibu:
"Amekumbwa na binadamu."
Dhikru Allaah
Kwa kumaliza napenda kujikumbusha nafsi yangu kwanza na pia kuwakumbusha ndugu zangu Waislamu pia kwamba, hakuna kinga kubwa inayomkinga mtu kutokana na kila balaa baada ya Qur-aan kama kumdhukuru Allaah.
Kumdhukuru unapolala, unapoamka, unapotoka nyumbani, unapositushwa na jambo, unapofurashishwa. Katika kila jambo lako jema au lisilo jema, bali hata katika kumuasi Rabb wako unapomkumbuka Allaah na kukumbuka uwezo Wake juu yako na neema Zake juu yako mara utayaacha maasi hayo.
Na ukumbuke kwamba kwa msaada wake Yeye tu Subhanahu wa Ta’aalaa utaweza kujikinga na kila balaa.
Usiingize Ndani Ya Nyumba Yako Yafuatayo:
Mwisho kabisa ningependa kukumbusha kuwa ndani ya nyuma yako usije ukaingiza yafuatayo;
Usitundike picha yeyote ile.
Usisikilize nyimbo.
Usiweke baraza za kusema watu au kutukana watu.
Usitizame filam za sinema nk.
Hayo yote yanakaribisha Mashaytwaan katika nyumba yako na yanafukuza Malaika.
Allaah Anasema:
وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٠٠﴾ إِنَّ الَّذِينَ اتَّقَوْا إِذَا مَسَّهُمْ طَائِفٌ مِّنَ الشَّيْطَانِ تَذَكَّرُوا فَإِذَا هُم مُّبْصِرُونَ ﴿٢٠١﴾
Na pindi utakapokuchochea uchochezi kutokana na shaytwaan; basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. Hakika wale waliokuwa na taqwa inapowagusa pepesi za shaytwaan hukumbuka, basi mara wao huwa wenye kuona kwa utambuzi. [Al-A'araaf: 200-202]
Hivi ndivyo ilivyo, wale wanaoasi daima hawapendi kuona wenziwao wanaokoka na wanajaribu kila njia kuwavutia katika maasi, lakini Mwenye kuomba msaada wa Allaah basi Rabb wake Atamuokoa.